Home Makala Kuna maisha baada ya maisha

Kuna maisha baada ya maisha

by Jamhuri

Jumapili Februari 12, 2017 saa 4:00 za usiku nilipokea taarifa kifo cha baba yangu mzazi kutoka kwa kaka yangu mkubwa aitwaye John.
Ohooooo!, nilishikwa na butwaa iliyoandamana na huzuni, sikuamini. Moyo wangu haukuamini, akili yangu iliukataa ukweli kuondokewa na baba mzazi, Raphael Bhoke. Hii yote ni kutokana na ubinadamu wangu, binadamu tumeumbwa kutokubali kupoteza bali kupokea tu.

Nilichukua kitabu cha Norman J. Muckerman, kiitwacho ‘Preparation for Death’. Machozi yakiwa yamejaa machoni nilikohoa na kujifuta, nikaanza kusoma.
Wakati nasoma, nilikutana na nasaha ya busara ya Mwanahistoria wa Kiitaliano, Francesco Guicciardin (1485 – 1540). Mwanahistoria huyu alipata kusema ‘ni jambo la uhakika lisilo jipya, kwamba sisi sote tutakufa, na hata hivyo sote tunaishi kama kwamba tunaishi milele.’ Baada ya kuisoma nasaha hii sikuendelea kusoma kitabu kile, nilibaki natafakari fumbo la kifo.
Kifo hakina kalenda, kingekuwa na kalenda ningefahamu mapema kwamba baba yangu mzazi atafariki tarehe 12. Maisha ya binadamu hayaishii kwenye kifo. Dini zote zinafundisha ama zinaamini kwamba, kuna maisha baada ya maisha. Unaweza kudhani kuwa ni jambo baya kuongelea mambo ya kifo, kitu ambacho ni lazima kutokea.

Maisha ya binadamu wakati wote ni safari. Duniani kila mtu anapita, hakuna mwenye hati ya milele ya kuishi hapa duniani. Kama ilivyokuwa katika ile miezi tisa uliyoitumia katika tumbo la mama yako kwamba haikuwa mwisho wa yote, lakini maandalizi kwa ajili ya maisha ya duniani, hivyo maisha haya ya duniani, ni maandalizi ya maisha yajayo.
Ifahamike kwamba, binadamu aliye hai ni marehemu mtarajiwa, sisi sote ni marehemu watarajiwa. Tunatarajia kufa wakati wowote. Tuyahariri maisha yetu na kuyaweka sawa kabla ya kwenda kwa mhariri mkuu. Siku moja watu watakwenda makaburini na kufanya ibada kidogo na kurudi nyumbani.
Wote watarudi nyumbani, na mtu mmoja tu atabaki kaburini, kumbuka huyo mtu ni wewe. Hakuna anayeweza kuyakwepa mauti ya mwili, ipo siku kila mtu atakabiliana nayo. Hebu fikiri kwa kina, ulipokuwa na umri wa miaka mitatu, ulikuwa wewe?

Bila shaka ulikuwa ni wewe, lakini sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, ulipokuwa na umri wa wiki moja, ulikuwa wewe? Ndiyo ulikuwa ni wewe. Lakini sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, ulipokuwa tumboni mwa mama yako, ulikuwa ni wewe? Ndiyo ulikuwa ni wewe. Sasa umebadilika, lakini bado ni wewe. Je, miaka 300 iliyopita ulikuwa wapi? Bila shaka mbele za Mungu ulikuwa ni wazo.
Lakini bado wewe uliyekuwa wazo mbele za Mungu bado ni wewe. Tafakari miaka 200 ijayo hautakuwa hai, lakini bado utakuwa ni wewe. Sote, tukubali kwamba kuna Mungu aliyetuumba kwa sura na mfano wake. Huyu Mungu aliyekuumba kwa sura na mfano wake, anatupenda sana.

Kifo si kushindwa kwa Mungu, ni kurudi kwa Mungu. Swali juu ya Mungu ndilo swali kuu kwa watu wote, halimhusu mchunguzi wa elimu ya teolojia, falsafa, au sayansi. Kwa muda mrefu hata kabla ya watu hawajafahamu elimu ya fizikia na kemia, wanadamu wa kila rangi, na ustaarabu mbali mbali kila wakati walikuwa wakitafuta kumjua muumbaji wa ulimwengu wote.
Watu wa zama za kale waliamini nafsini mwao ya kuwa Mungu yupo. Hawakuwa na shaka yoyote. Kati ya karne ya 19 na 20 mafundisho ya kuwa hakuna Mungu (Atheism) yaliibuka na kushamiri.
Watu wengi walianza kufundisha kuwa hakuna Mungu. Mwanafalsafa Friedrich Nietzsche katika kitabu chake cha ‘Ant Christ’ aliandika Mungu amekufa. Kwa hakika maneno ya mfalme Daudi yatadumu. Maneno hayo ya Daudi yanasomeka hivi; Mpumbavu asema moyoni hakuna Mungu (Zab 14:1).
Lakini mwanafalsafa huyu, Friedrich Nietzsche, kabla ya kifo chake alimwambia rafiki yake mpendwa, B. Von Overback, kuwa angalia usimwache Kristo, kumfikiria ni jambo kuu na lenye nguvu. Mawazo ya Mwanafalsafa Friedrich Nietzsche ni mawazo ya kukimbia na pia ni mawazo ya kupuuza.

Mwanasayansi Mfaransa, Louis Pasteur (1822 – 1895), anapuuza falsafa ya wakana Mungu na kusema; siku moja walimwengu wataucheka upuuzi wa falsafa ya kisasa isadikiyo kuwa hakuna Mungu. Kadri ninavyoendelea zaidi kuchunguza elimu ya viumbe ndivyo ninavyoendelea zaidi kushangazwa na kazi ya Muumbaji.
Mungu aliyeumba sayari, nyota, wanyama mbalimbali ndiye Muumbaji wetu. Kila binadamu ana uraia wake mbinguni hivyo ni jukumu lako kuulinda uraia wako kwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu na jirani yako. Mungu anapenda kila mtu arudi kwenye makazi yake ya asili ambapo ni mbinguni.
Matendo yako ya sasa ndiyo mwamuzi wa maisha yako baada ya kifo chako. Naomba kukunong’oneza jambo hili; Mungu anakupenda sana na anakutaka ufuate utaratibu uliojiwekea wa kuishi. Kumbuka siku moja moyo wako utaacha kudunda. Huo ndiyo utakuwa mwisho wa kuishi maisha yako ya hapa duniani. Swali la kujiuliza ni umejiandaaje?
Safari ya kifo ni safari ya furaha na shangwe kwa wale wote walioishi maisha ya kumtumainia Mwenyezi Mungu. Pia ni safari ya majuto, masikitiko, majonzi kwa wale wote walioishi maisha ya kumsahau Mwenyezi Mungu.
Maisha ya binadamu ni kama maua ya kondeni yanachanua na kunyauka. Kumbuka sifa za maua, maua hutoweka upesi, mengi huchanua muda mfupi. Maua ni mazuri kwa macho, ni chakula cha macho, maua hutoa harufu nzuri.
Nasi maisha yetu yatoe harufu nzuri mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya binadamu wenzetu. Matendo yetu yatoe harufu nzuri. Kuona uso wa Mungu ni lazima maisha yetu yawe yamepambwa na fadhila za upole, upendo, msamaha, unyenyekevu, uvumilivu na huruma.

Tuishi maisha ya uadilifu, ili siku atakayokuita Muumba wetu, iwe siku ya furaha timilifu. Mshairi wa Hispania, Cesar Vallejo, aliandika ujumbe huu katika kitabu chake cha kumbukumbu; Siku niliyozaliwa Mungu alikuwa na furaha, bila shaka siku nitakayokufa atakuwa na furaha zaidi.
Tuepuke kuishi maisha yanayotawaliwa na dhambi, dhambi ni kama doa jeusi juu ya karatasi nyeupe, dhambi ni kama magugu shambani, yasipong’olewa huharibu mazao. Dhambi hututenganisha na Mungu. Mungu anaichukia dhambi, Mungu yu karibu nasi, lakini dhambi inakuwa ukuta unaotutenganisha naye.
Hatujachelewa kubadilisha historia ya maisha yetu. Bado tunayo fursa ya kuwa watakatifu kuanzia sasa. Camillo de Lellis alikuwa mcheza kamari na karata. Aliishi maisha mabaya na ya ulaghai sana.
Siku moja akiwa amelewa pombe alimwona Mnomaki (Mnomaki ni jina la watawa wa Kanisa Katoliki waliojitenga na jamii na kuishi maisha ya useja, ufukara na usafi wa moyo). Camillo de Lellis alipomwona Mnomaki huyo alisema; Hata mimi naweza kuwa wa tofauti.

Kuanzia siku hiyo Camillo de Lellis aliongoka na kuanza kuishi maisha matakatifu. Camillo de Lellis aliipenda aya ya Mwinjili Yohane inayosema, “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lolote” (Yoh 15:5). Camillo de Lellis aliamini kwamba bila Kristu yeye hawezi kufanya lolote. Kanisa Katoliki linamheshimu Camillo de Lellis kama Mtakatifu.
Ndugu msomaji, Camillo de Lellis alikuwa mlevi, mcheza kamari na mlaghai, lakini akaamua kubadilika. Hata wewe leo unaweza kuyarudia maneno ya Camillo de Lellis, kwa kusema; Hata mimi naweza kuwa wa tofauti. Tafakari hatima ya maisha yako itakuwaje. Piga picha. Vuta hisia na kumbukumbu.
Kuna wakati utafika utajiri wako hautakuwa na msaada kwako. Kuna wakati utafika marafiki zako watashindwa kukusaidia. Huu ni ule wakati ambao roho yako itakuwa imesimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.
Wakati huo hautaruhusiwa kuuliza maswali. Wakati huo hautaruhusiwa kujitetea. Huo ndiyo wakati utakaposikia sauti ya mbali ikikukumbusha maneno haya; “Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?” (Mt. 16:26).

Kama tunaishi maisha ya uadilifu, kifo na maisha baada ya kifo vitakuwa ni tukio la furaha isiyo na mwisho. Mwandishi H. Milton alipata kusema, “Kifo ni ufunguo wa dhahabu unaofungua mahali pa maisha ya milele”. Kwa upande wake, Mtume Paulo anasema; “Kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida”(Fil 1:20).
Starehe na fahari za ulimwengu zisiufunike ukweli kwamba kuna maisha baada ya maisha. Maisha tunayoyajua yatakoma, ila maisha ya utukufu yako tayari kwa watoto wa Mungu. Tumo safarini kwa muda mfupi, tunapita katika maisha haya na tunaelekea nyumbani kwetu mbinguni.
Mbinguni ni mahali palipokamilika kwa upendo na furaha, amani isiyo na mwisho, ni mahali palipojitosheleza mno, na ni pa ajabu kiasi kwamba hatuwezi kuanza kupaelewa. Hakuna dhambi, kifo, uovu, fujo, chuki, huzuni, au kutengana. Hakuna shetani wa kusumbua, hakuna mateso wala maumivu. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.

Na WILLIAM BHOKE, Mwanza

0719 700446

You may also like