Kuungua kwa soko la kimataifa la Kariakoo ni pigo kwa uchumi wa Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla, ingawa kwa hakika ni msiba mzito kwa mfanyabiashara mmoja mmoja aliyewekeza katika soko hilo.

Kwa miaka mingi eneo zima la Kariakoo limekuwa kitivo cha biashara cha Tanzania, likiwakusanya wafanyabiashara kutoka mikoa yote nchini pamoja na wale wa kutoka mataifa jirani.

Aghalabu, wafanyabiashara wa Malawi, Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya hufanya ununuzi sokoni Kariakoo au maeneo ya karibu na soko hilo ambalo wikiendi iliyopita limeteketea kwa moto.

Kariakoo ni eneo lenye msongamano mkubwa wa watu kuliko eneo jingine lolote nchini. Ni hapa ndipo mahitaji karibu yote hupatikana na inaaminika kuwa upatikanaji wake ni wa bei rahisi kabisa.

Umuhimu wa eneo hilo kibiashara umesababisha kukua kwa kasi ya ajabu; majengo makubwa makubwa na ya kisasa yameinuka kama uyoga katika miaka ya karibuni na kubadili kabisa mwonekano wa Kariakoo.

Ni bahati mbaya kwamba kukua kwa eneo hilo ama hakukuzingatia ramani ya mipango miji au kulikiuka kabisa kanuni za utunzaji wa mazingira, miundombinu na hata afya na usalama wa wakazi wa hapo na mali zao.

Ingawa mitaa ya Kariakoo inaweza kuonekana kuwa ipo na imenyooka, bado kuna ukweli kwamba miundombinu yake si bora, tofauti kabisa na thamani ya eneo lenyewe.

Barabara za Kariakoo hazipitiki kwa urahisi pamoja na kwamba kwa sasa zote zimejengwa kwa kiwango cha lami kutokana na wingi wa watu pamoja na magari yanayoegeshwa pembeni.

Hali hii huwa ni kikwazo kwa watoa huduma za uokoaji kama Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi na hata magari ya wagonjwa na hilo limethibitika mwishoni mwa wiki wakati moto ulipolipuka kwenye Soko la Kariakoo.

Eneo la Kariakoo kwa sasa halipumui. Limejaa kupita kiasi. Hakuna sehemu ya watu kukusanyika iwapo kuna janga limetokea, iwe la moto au tetemeko la ardhi. Yote hii ni kutokana na ubovu wa mipango miji.

Kikosi cha Zimamoto kinalaumiwa kwa kuchelewa kufika mapema eneo la tukio na hii si mara ya kwanza. Lakini je, miundombinu rafiki kwa kikosi hiki ipo jirani? Maji yanapokwisha kwenye magari yao, wana uwezo wa kwenda haraka kunyonya maji mengine na kurejea kwa wakati kabla moto haujashika kasi upya?

Maswali haya hayana majibu sahihi kwa sasa, ndiyo maana tunapendekeza kuwa sasa ni wakati wa wataalamu wa mipango miji kubuni namna sahihi ya kuwasaidia watu wa uokoaji kuyafikia maeneo yenye majanga kwa urahisi.

Miji mipya inayojengwa iwekewe tahadhari ya majanga ya kibinadamu na yale ya kiasili ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wataalamu wa uokoaji na wale wa miundombinu ya maji, ili kuwe na mabomba maalumu ya magari ya zimamoto kunyonya maji badala ya sasa kulazimika kurejea kituoni kwao kufuata maji.

Tunatoa pole kwa wafanyabiashara wote walioathiriwa na janga hili kubwa kuwahi kutokea tangu kujengwa kwa soko hili lenye mvuto wa kipekee Afrika Mashariki.

By Jamhuri