“Rozari ni sala nzuri sana na yenye utajiri wa neema, ni sala inayogusa kwa karibu Moyo Safi wa Mama wa Mungu… na ikiwa unataka amani itawale katika nyumba zenu, salini Rozari katika familia.” (Baba Mtakatifu Pius X)

Utangulizi

Kila mwezi Oktoba waamini Wakatoliki wanaalikwa kusali Rozari kwa mwezi mzima. Lengo kubwa ni kumheshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria kwa maombezi yake ya kimama kwetu wanadamu. Oktoba ni fursa nyingine tena ya kumwendea Mama Bikira Maria na kumshirikisha furaha, shukrani, tabu, changamoto na matarajio yetu kwa njia ya Rozari Takatifu ambayo hutupa nafasi ya kutafakari mafumbo ya maisha ya Yesu na Maria katika safari ya wokovu wetu. Hivyo, tukiwa kwenye Mwezi wa Rozari nimeona ni vema nikuletee walau kwa ufupi historia ya Rozari Takatifu.

1. Asili ya neno ‘Rozari’

Neno la Kiingereza ‘rosary’ linatokana na neno la Kilatini ‘Rozarium’ lenye maana ya ‘bustani ya mawaridi’ (rose garden) au ‘taji ya mawaridi’. Kwa kadiri ya desturi ya watu wa Ulaya kupeana maua ya mawaridi ni moja ya matendo yenye lengo la kuonyesha upendo wa hali ya juu kwa mtu fulani, hasa wakati wa furaha au huzuni; mawaridi pia ni zawadi kubwa ya upendo hasa baina ya wapenzi.

Sisi Wakristo Mama Bikira Maria ni mpenzi wetu na zawadi kubwa tunayoweza kumpa ni ‘kusali rozari’ ambayo  ndiyo ‘mawaridi yetu kwake’. Kwa kadiri ya mapokeo, mawaridi hasa meupe yanamwakilisha Bikira Maria asiye na doa, yaani ni mweupe kama waridi jeupe.

2. Historia ya awali ya Rozari

Katika zama za kwanza za Ukristo (karne ya 3 na ya 4) walikuwapo Wamonaki (Monks) na Wahermiti ambao waliamua kuiishi injili kwa ukamilifu, hivyo kuamua kuishi maisha ya upweke, ama mmoja mmoja au kama kikundi. Wamonaki waliamua kuishi maisha ya pamoja huku lengo lao kuu likiwa kusali na kuishi mashauri ya injili ambayo ni usafi wa moyo, utii na ufukara.

Wamonaki kwa kipindi hicho walikuwa ni wasomi ingawa walikuwa wachache. Hivyo, waliamua kama sehemu ya maisha yao ya sala, kusali Zaburi zote 150 kila siku. Hata hivyo, baadaye waliamua kuwa angalau wawe wamesali Zaburi zote 150 kwa wiki.

Ili kuweza kuzihesabu wakati wa kusali bila kuchanganya, waliamua kukusanya, ama changarawe – mbegu ndogo za matunda au kokoto 150 na kila walipomaliza Zaburi moja walichukua changarawe, mbegu au kokoto moja na kuitupa kwenye chombo mfano wa debe au ndoo au kikapu au mfuko ili kujua wamefika Zaburi ya ngapi. Baadaye, ili kuweza kuhesabu vizuri na kwa urahisi zaidi waliamua kutumia kamba ndefu ambayo waliiwekea vifundo 150 sawa na jumla ya Zaburi zote 150.

Watu wa kawaida walioishi jirani na nyumba za Wamonaki walitamani sana kujiunga nao na kusali Zaburi hizo 150. Kwa bahati mbaya wengi wa watu hao walikuwa hawajui kusoma wala kuandika na hata teknolojia ya uchapaji ilikuwa bado ipo chini sana na hata wengi wao hawakuwa na muda wa kutosha wa kuweza kusali Zaburi zote.

Hivyo, ili kuonyesha nia yao ya kusali Zaburi 150 pamoja na Wamonaki, majirani hao waliamua kuwa watakuwa wanasali sala ya Baba Yetu mara 150 wakati Wamonaki wanasali Zaburi zote 150. Mwanzoni, Wakristo hao wasio Wamonaki waliiga pia namna ya kuzihesabu Baba Yetu kwa kutumia kokoto, mbegu za matunda, mawe au changarawe. Baadaye walianza kutumia ushanga uliopitishwa kwenye kamba (string of beads).

Hata sisi leo tunatumia Rozari iliyotengenezwa kwa namna hiyo. Inasemekana kuwa Mt. Peter Damiani mnamo karne ya 11 alitoa ushauri wa kusali Salamu Maria 150 badala ya Baba Yetu 150. Kumbe tangu hapo Wakristo wakaanza kusali Salamu Maria 150 huku wakiendelea kutumia kamba iliyowekewa mafundo 150 au shanga 150 zilizopitishwa kwenye kamba ili kuwasaidia kusali vizuri.

Baadaye mnamo mwaka 1365 Mmonaki aitwaye Henry wa Kalkari (1328-1408) alizigawa Salamu Maria 150 katika makundi 15 yenye Salamu Maria 10 kila moja. Pia aliweka Baba Yetu kila baada ya Salamu Maria 10. Hivyo sala ya Rozari ikawa na Salamu Maria 10 zinazorudiwa mara 15 zikiambatana na Baba Yetu kila baada ya Salamu Maria 10. Ingawa sisi leo tunatumia Rozari yenye takriban Salamu Maria 50, bado kuna Rozari ambayo ina jumla ya Salamu Maria 150 kwa wakati mmoja.

3. Mt. Dominiko na historia ya Rozari

Ingawa Mt. Dominiko yeye mwenye hakuwahi kusema au kuandika kuwa ametokewa na Bikira Maria na kupewa Rozari na kufundishwa kuisali ili awafundishe wengine, simulizi zinamhusisha Mt. Dominiko kama chanzo cha Rozari kama tuijuavyo leo.

Mwenyeheri Allan de la Roche katika maandishi yake anadai kuwa alifunuliwa katika ndoto na kumuona Mt. Dominiko akipewa Rozari na Bikira Maria. Mbali na Dominiko kutajwa na Mwenyeheri Allan de la Roche, Mababa Watakatifu wengi wamemtaja pia Mt. Dominiko kama mtu anayehusika na asili ya Rozari katika mwonekano wa sasa.

Inasemekana kuwa wakati huo kulikuwa na kundi la wazushi hasa Ufaransa na Italia waliokuwa wanapita kwa watu na kufundisha mafundisho potofu huku wakikataa fumbo la umwilisho (nafsi ya pili ya Mungu kuchukua mwili na kuwa binadamu), walipinga fundisho la Kanisa juu ya uwepo wa masakramenti na walikuwa wakiyapigia debe matendo ambayo Kanisa lilifundisha kuwa ni maovu. Mt. Dominiko alipambana nao kwa udi na uvumba, lakini juhudi zake hazikuzaa sana matunda.

Kwa mujibu wa Mwenyeheri Allan de la Roche, Bikira Maria alimtokea Mt. Dominiko mnamo mwaka 1214 na kumwambia kuwa ili kuwashinda wazushi hao anapaswa kueneza ibada ya Rozari, hivyo kumfundisha Mt. Dominiko. Mara baada ya kuanza kuisali na kuwafundisha watu wengine kundi hilo la wazushi lilitokomea kabisa kwani wengi wao waliongoka na kurudia mafundisho ya kweli. Hivyo, kwa njia ya Rozari Takatifu Kanisa lilipata ushindi dhidi ya wazushi.

Hivyo, tokea wakati wa Mt. Dominiko hadi mwaka 1930 Rozari ilikuwa na jumla ya sala tano: Kanuni ya Imani ya Mitume, Salamu Maria, Atukuzwe Baba, Baba Yetu na Salamu Malkia. Sala hizi hazikuwekwa siku moja tu na kukamilisha Rozari, bali zilikuwa zinawekwa katika vipindi tofauti vya historia ya Rozari.

Katika tokeo la Bikira Maria kwa watoto watatu (Lucia, Francisco na Jacinta) huko Fatima, Ureno Julai 13, 1917, Bikira Maria aliagiza watoto hao kuongeza maneno “Ee Yesu Mwema, Utusamehe dhambi zetu, Utukinge na moto wa milele, Ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaohitaji zaidi huruma yako” kila baada ya Salamu Maria 10. Sala hii inaitwa Sala ya Fatima. Mwaka 1930 Kanisa lilitamka wazi kuwa Sala ya Fatima itumiwe na Wakristo wote wa Kanisa zima wasalipo Rozari. Sala hii ilifanya Rozari kuwa na jumla ya sala 6.

Kuanzia karne ya 16 hadi mwanzoni mwa karne ya 21 kulikuwa na makundi matatu ya mafumbo ya Rozari: Mafumbo ya Furaha, Mafumbo ya Utukufu na Mafumbo ya Uchungu. Mwaka 2001 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliongeza Mafumbo ya Mwanga. Nia kubwa ilikuwa ni kuwafanya waamini watafakari maisha ya Yesu kati ya kuzaliwa kwake na mateso yako.

4. Kwanini mwezi wa 10 ni mwezi wa Rozari?

Kanisa limeweka mwezi Mei na Oktoba kuwa miezi ya kumheshimu Mama Bikira Maria. Wengi wetu hufahamu tu mwezi Oktoba. Mwezi Mei ni mwezi wa Bikira Maria kwa kuwa Bikira Maria aliwatokea Lucia, Francisco na Jacinta huko Fatima, Ureno kwa mara ya kwanza Mei 13, 1917 ujumbe mkuu ukiwa kuhangaikia wokovu wa roho za binadamu kwa njia ya kusali Rozari na ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria.

Oktoba ni mwezi wa kusali Rozari Takatifu. Kuchaguliwa kwa Oktoba kuna msingi wake katika historia ya Kanisa. Waislamu wa Kituruki miaka ya 1500 waliamua kutumia mwanya wa vuguvugu la kujitenga kwa Waprotestanti kutoka Kanisa Katoliki. Hivyo, waliamua kuvamia nchi za Ulaya ili kueneza dini yao kwa nguvu ya upanga na vita kwa kuwalazimisha Wakristo kuwa Waislamu.

Oktoba 7, 1571 Waislamu wa Kituruki waliamua kuivamia Italia kwa kuanzisha vita ya baharini iliyojulikana kama Vita ya Lepanto (Ugiriki). Baba Mtakatifu wa wakati huo alikuwa Pius V. Baba Mtakatifu alijua wazi kuwa Waislamu walikuwa ni wengi kwa idadi kuliko Wakristo na ya kuwa Waislamu walikuwa na meli nyingi za kivita kuliko Wakristo.

Hata hivyo, Baba Mtakatifu aliamuru jeshi lake likisaidiwa na wanajeshi kutoka Hispania kwenda baharini kupambana na Waislamu. Baba Mtakatifu aliamuru kila askari abebe Rozari na kuisali wanapokuwa vitani majini; pia aliamuru wananchi wa Italia waliobaki majumbani wafanye maandamano makubwa huku wakisali Rozari kuomba msaada wa Bikira Maria ili Wakristo washinde vita.

Yeye mwenyewe alisali Rozari siku hiyo ya Oktoba 7. Muda si mrefu habari zilimfikia Baba Mtakatifu kuwa Wakristo wameshinda vita na kati ya meli 242 za Waislamu zimesalia meli 12 tu; huku Waislamu 30,000 wakiwa wameuawa, na takriban 8,000 wamejeruhiwa au kutekwa. Kwa upande wa Wakristo ni watu 7,500 tu waliokuwa, ama wameuawa, au wamejeruhiwa au kutekwa, ambao baadaye wengi wao walifanikiwa kutoroka.

Baba Mtakatifu Pius V alitamka kuwa ushindi huo haujatokana na weledi wa askari wala ubora wa vifaa vya kivita, bali ni ushindi uliotokana na maombezi ya Bikira Maria wa Rozari. Kutokana na ushindi huo dhidi ya Waislamu, Baba Mtakatifu Pius V alianzisha rasmi Sherehe ya Mama Yetu wa Ushindi mwaka 1572.

Mwaka 1573 Baba Mtakatifu Gregory XIII aliibadilisha jina sherehe hiyo na kuipa jina la Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu. Mwaka 1884 Baba Mtakatifu Leo XIII alitangaza rasmi kuwa mwezi wote wa Oktoba utakuwa mwezi wa kusali Rozari Takatifu akiwa na kumbukumbu ya ushindi ambao Wakristo waliupata dhidi ya Waislamu katika Vita ya Lepanto tarehe 7, Oktoba 1571. Lengo kubwa la kutangaza Oktoba kuwa mwezi wa Rozari lilikuwa kumheshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria ambaye kwa maombezi yake Wakristo walipata ushindi Oktoba 7, 1571.

5. Kwanini Bikira Maria anajishughulisha na wokovu wa wanadamu?

Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho na kufanywa Malkia huko mbinguni. Kwa nini asikae huko akatulia na kuendelea kufurahia kumwona Mungu ana kwa ana? Kwanini anawatokea watu duniani? Jibu ni rahisi sana: Kwanza, Bikira Maria, kwa kumuona Mungu kama alivyo, anafahamu furaha isiyo kifani ya kumwona Mungu na anataka kila mtu apate furaha hiyo; na ndiyo maana hawezi kutulia mbinguni kwa kuwa anatamani kila mmoja aionje furaha hiyo hasa wakosefu.

Ndiyo maana anapowatokea watu duniani anatoa ujumbe kwa watu kufanya toba, kusali Rozari, kupokea mateso kama njia ya kupata wokovu, kuombea marehemu wa toharani na kuonya wakosefu kubadili matendo yao. Pili, Bikira Maria anajishughulisha na wokovu wa wanadamu kwa kuwa alikabidhiwa jukumu hilo na mwanaye Yesu Kristo. “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” (Yoh. 19:26)

Sisi sote tunawakilishwa na Yohane; sisi sote ni  wana wa Maria. Hivyo, Yesu hapa anamaanisha: “Mama! Tazama, watoto wako”. Neno “Tazama” lina maana kubwa sana: kututunza, kutushughulikia na kutuangalia kwa namna ya pekee. Hivyo, Bikira Maria anaendelea siku zote kututunza, kutushughulikia na kutuangalia kwa namna ya pekee kwa maombezi yake ya kimama, kwa kutuelekeza nini tufanye pindi anapotokea kwa baadhi ya watu.

6. “Tazama, huyu ndiye mama yako.” (Yoh. 19:27)

Yesu anamwambia Yohane amtazame mama yake (Bikira Maria). Yohane anatuwakilisha sisi sote. Sisi sote tumekabidhiwa kwa Bikira Maria kama Mama yetu. Je, tumtazemeje Bikira Maria? Tutamtazama Bikira Maria kwa kumpenda, kumheshimu na zaidi ya yote kwa kusali Rozari Takatifu ambayo kiini chake ni tafakuri ya mafumbo juu ya maisha ya Yesu na Bikira Maria. Kwanini tusali Rozari? Je, Rozari ina faida gani?

• Rozari inatuwezesha kuwa na ufahamu kamili kuhusu Yesu siku kwa siku.

• Rozari inatakasa roho zetu.

• Rozari inatupatia ushindi dhidi ya adui zetu.

• Rozari inatuwezesha kuishi maisha ya fadhila.

• Rozari inawasha ndani yetu moyo wa mapendo kwa Bwana Wetu Yesu Kristo.

• Rozari inatutajirisha kwa neema na mastahili.

• Rozari inatuwezesha kupata yale tunayohitaji kutoka kwa Mungu.

• Rozari inawezesha kufunguliwa kwa roho zilizopo toharani.

• Rozari inatutia nguvu tuwapo katika madhaifu na changamoto za kimwili na kiroho.

7. Matokeo ya kusali Rozari

Kwa hakika Rozari ni sala yenye nguvu sana. Ukijiwekea mazoea ya kuisali utaona uzuri wa Rozari na kamwe hutaiacha. Zamani niliona kusali Rozari ni mzigo, ni kupoteza muda na kama kero tupu. Lakini kila siku ninazidi kuonja uzuri na nguvu ya Sala ya Rozari. Muda mzuri wa kusali Rozari ya binafsi, kwa kadiri ya uzoefu wangu binafsi, ni alfajiri, kwani akili huwa imetulia sana. Hata hivyo, kila mtu anaweza kutenga muda wake atakaoona unafaa kwake. Kwa njia ya kusali Rozari:

• Wadhambi wanasamehewa.

• Roho zenye kiu zinaburudishwa.

• Magumu yanafanywa kuwa mepesi.

• Wanaopitia majaribu wanapata amani.

• Maskini wanapata msaada.

• Wenye mahangaiko wanapata faraja.

• Roho za marehemu toharani zinapunguziwa mateso na zingine kufunguliwa.

Ee Mama Mpendelevu sana, utujalie nguvu ya kuweza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya wokovu wetu na wa dunia nzima. Amina.

Mwandishi wa makala hii, Padri Kelvin Onesmo Mkama, yuko Jimbo Kuu Mwanza. Anapatikana kwa simu: 0753 266 330.

By Jamhuri