Ndugu zangu, DPP, mimi ninafikiri sikutakiwa kusema chochote kwa sababu umekuja kutoa taarifa ya ushauri wangu nilioutoa siku za nyuma kidogo na sikutegemea kama watu wengi watakuwa wamejitokeza.

Watu 467… watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi ndio wameandika barua kwako wakiomba wasamehewe na watalipa kwa awamu, labda analipa nusu kwanza, kadiri mtakavyokuwa mmekubaliana ninyi na serikali, jumla Sh 107,842,112.744 kadiri nilivyonakiri kutokana na taarifa yako.

Labda tu mimi nikupongeze DPP pamoja na watendaji wenzako wanaokusaidia kwenye Ofisi ya DPP. Sifahamu kama umekuja nao. Hebu wasimame wa Ofisi ya DPP wote (wanasimama), safi kabisa, jamani muwapigie makofi kabisa. Haya kaeni.

Ninawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya. Nasema kwa dhati, ofisi yako inafanya kazi nzuri. Tumekuwa tukishuhudia na kusikia jinsi Ofisi ya DPP na vijana wako mnavyofanya kazi nzuri hasa katika kesi mbalimbali na mashauri mbalimbali yanayoihusu serikali na mara nyingi serikali imekuwa ikishinda – mkiwa mnaiwakilisha vizuri.

Nasema kwa dhati kwa niaba ya Watanzania tunaipongeza sana ofisi yako na watendaji wako wote. Tumeshuhudia madini yakitaifishwa, tumeshuhudia mambo mengi, na hii inadhihirisha ni kwa namna gani ofisi yako inafanya kazi kubwa katika kuitetea serikali na kutetea rasilimali za Watanzania.

Pokeeni pongezi zangu kwa niaba ya serikali. Ninaomba tu mwendelee hivyo. Pia nawapongeza PCCB ambao nao wamekuwa wakishiriki kwenye kesi hizi, Jeshi la Polisi nao wamekuwa wakishiriki kupitia kitengo chao cha upelelezi.

Kwa hiyo endeleeni kushikamana kwa pamoja, lakini vilevile tuwashukuru watendaji wote wa Mahakama ambao wamekuwa fear katika kutoa maamuzi kulingana na sheria zinazowahusu. Kwa hiyo kwa ujumla mfikishe salamu zangu vizuri.

Kwenye hili suala la watuhumiwa kwanza nikiri kwamba sikutegemea kama watajitokeza watu 467 mpaka sasa hivi na umeeleza pia kwamba wengine wameshindwa kwa sababu process za kuandika barua kwenye magereza wengine wamecheleweshwa.

Na kuna barua zingine zozote bado hazijafika? Ambazo zimekwama kule magerezani. Kwa hiyo kuna barua zingine za watu wanaoomba msamaha zimekwama kwenye ofisi zako za mikoa na zingine zimekwama magerezani. Ndiyo maana ukachomekea hapa ukasema niongeze siku tatu. Kwanza, hii response (mwitikio) ni mkubwa sana wa watu 467 na kama kweli wapo waliokwamishwa na wamekwama kutokana na distance (umbali) ya kutoka kuja mpaka hapa barua ikufikie na wengine kwenye process (taratibu) ndani ya magereza na umeniomba siku tatu, siku tatu hakuna tatizo.

Leo ni Jumatatu, kesho Jumanne, maana yake Jumatano zitakuwa zimekamilika. Mimi naona nikupe siku saba ili usije ukaniomba siku zingine. Nilitoa siku hizo sita, siku za nyuma kwamba watuhumiwa wote wanaotaka kupata huu msamaha kwa kupitia process za kisheria na wameitikia watu zaidi ya 467 na fedha bilioni 107.842 zitaokolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao.

Mimi nafikiri niwaongezee siku saba zaidi, lakini nitoe tahadhari, baada ya siku hizi ambazo tumeziweka wale wote watakaoshikwa kwenye masuala ya uhujumu uchumi sheria ichukue mkondo wake.

Isije sasa ikawa imejengeka mazoea kwamba kesi ya uhujumu uchumi haipo. Watakaoshikwa baada ya siku hizi ambazo nimeziongeza siku saba na wale ambao ni kesi mpya, kwa sababu kuna kesi leo mtu anaweza akahujumu.

Akihujumu leo tu apelekwe kwenye kesi za uhujumu uchumi – hahusiki na huu msamaha. Kwa hiyo kesi za uhujumu uchumi watakaoshikwa leo, kesho na kadhalika wao waendelee na kesi zao za uhujumu uchumi.

Hizi siku saba zinazokuwa extended (zimeongezwa) ni kwa wale ambao wamekwama – barua zao wameandika ziko magerezani hazijakufikia, lakini najua zimeandikwa. Lakini kwa wale ambao barua ziliandikwa ziko kwenye ofisi zako za mikoani na inawezekana mwingine akawa amejifikiria zaidi katika siku ya leo mpaka siku hiyo ya saba akatoa maamuzi yake.

Ninafahamu wapo wanaodanganywa, wanaambiwa huu msamaha ni wa uongo. Huwa hakuna msamaha wa uongo, ukishatoa msamaha ni msamaha. Huwezi ukatoa msamaha wa majaribio. Huwezi ukatoa msamaha wa kumtega mtu, msamaha ukishatoa ni msamaha otherwise (vinginevyo) wewe unayetoa huo msamaha utaibeba dhambi hiyo kwa Mungu. Msamaha ni lazima uwe msamaha. Ninafahamu wapo wengine wanadanganywa na mawakili wao ili kusudi mawakili hawa waendelee kuwachomoa pesa. Wanawaambia: “Ukiomba msamaha maana yake umeshajishitaki mwenyewe”. Hao ni shauri yao.

Wachague kuwasikiliza mawakili wao au wachague kukusikiliza wewe DPP na kusikiliza ushauri wangu nilioutoa. Na ndiyo maana ninasema nimetoa hizi siku saba nyingine sitatoa tena. Sitatoa tena, lakini niwapongeze hawa 467 ambao documents zao mnazichambua na mimi ningeomba Ofisi ya DPP mharakishe hizi process. Watu waanze kuwa free (huru), waanze kutoka, wakajumuike na familia zao.

Mtu akishalipa hizo hela na mmeandika na mmefanya hizo process zenu za kimahakama kwa sababu waliingia kwa njia ya mahakama, watatoka kwa njia ya mahakama. Kwa hiyo muwafikishe haraka kwenye vyombo vya sheria ili waanze kuachiwa wakajumuike na familia zao isije tena 467 mtakapochambua.

Labda mtajikuta wamebaki 400 au 300 au…na kadhalika, wakakaa tena wamesubiri, ilikuwa wiki, mwishowe wiki mbili, mwishowe mwezi, mwishowe mwaka, dhana ya msamaha hii itakuwa haina maana. Najua Ofisi yako ya DPP mkijipanga vizuri kwa sababu sasa suala litakuwa ni moja tu kutoa msamaha.

Sifahamu process mnazozitumia ninyi, ndiyo maana mimi nasema nilitoa ushauri na ushauri ule umeukubali na ofisi yako na wataalamu wako mmekubali, mimi nashukuru. Ndiyo maana nasema ninashukuru hata kwa taarifa hii. Umeniomba niongeze siku tatu nimeongeza siku saba, au ni nyingi mno? Nimewaongezea mno nyingi hizi au nipunguze kidogo? Haya zibaki hizo siku saba? Haya.

Kwa hiyo katika siku saba wapo wengine labda walizuiliwa na maofisa wa magereza kwamba: “Sipeleki ombi lako lazima na sisi unatuachaje tuliokuwa tunakushikilia?” Sasa Kamishna wa Magereza yuko hapa, mkafuatilie wote waliomo kwenye magereza ambao wameomba msamaha huu kwa DPP ili msiwakwamishe. Ili watu kwa dhamira yao wala msiwalazimishe, pasitokee mtu wa kulazimishwa kuomba msamaha, kwa hiari yao katika siku hizi. Basi, na mimi nafikiri hicho ni kitu kizuri.

Hizi bilioni 107 zitatumika hata kujenga mahospitali, kutengeneza barabara, kulipa mishahara ya wafanyakazi, kufanya mambo mengi tu makubwa kwa ajili ya taifa. Lakini pia na wao walikuwa na shughuli zao zilikuwa zimekwama, walikuwa na biashara zao zilikuwa zimekwama. Waje washiriki pamoja na serikali katika kuendeleza sasa biashara zao. Lakini si tu biashara zao, katika biashara zao serikali itakuwa inakusanya kodi. Lakini pia watu, wafanyakazi wao wataendelea ku-create opportunity ya creation ya job katika maeneo yao. Lengo letu ni kuijenga nchi yetu na kuijenga Tanzania.

Mimi nilifikiri DPP, niwashukuru tena vyombo vingine vinavyohusika vikishirikiana na Ofisi ya DPP kama hiyo kesi ilikuwa inasimamiwa na Ofisi ya TAKUKURU, basi mkashirikiane vizuri na hawa wahusika.

Kwa vile DPP amesharidhia kwamba anataka awasamehe kwa mujibu wa sheria na taratibu, basi mshirikiane nao kuwezesha. Kama ni suala la upelelezi Jeshi la Polisi, mkashirikiane nao Ofisi ya DPP katika kutatua. Kama ni magereza hivyo hivyo, ili muwezeshe hili suala. Napenda nitoe wito kwa Watanzania wenzangu na Watanzania ambao walikuwa wana tuhuma za uhujumu uchumi ambao wana nia ya kutaka kutubu na kurudisha hicho na kukiri wala wasiwe na wasiwasi kwamba ukishakiri, basi kesi ndiyo ushahidi huo. Siwezi nikafanya kazi ya kitoto ya namna hiyo, si kwa wakati huu. Ukishasema nimetoa msamaha maana yake ni msamaha kweli.

Kwa hiyo wasidanganywe, hao wanaowadanganya wanataka waendelee kukaa gerezani na kadiri watakavyokuwa wanakaa wasije wakamlaumu mtu yeyote.

DPP amesharidhia, naye ameguswa; na Watanzania wengi wangependa kuwaona hawa watu wakirudisha na kutuba dhambi zao, lakini hatuwalazimishi. Lakini nitoe angalizo DPP, kwa wale wanaoshikwa kesi za uhujumu uchumi hata kuanzia leo ukimshika huko anahujumu uchumi usifikiri anahusika na msamaha huu. Kashughulike naye kisawasawa.

Siyo kwamba sasa kesi za uhujumu uchumi nimezifuta, au zimefutwa. Zile ziliundwa kwa mujibu wa sheria, zipo pale ila kwenye hili nilitoa ombi na ombi langu linaonekana limekubalika kwako na wasaidizi wako. Na mtu mwenye mamlaka ya kufuta kesi yoyote ni DPP wala si mtu yeyote pamoja na mahakama ambayo inaweza ikatoa hukumu. Kwa hiyo mimi nakushukuru, nakushukuru sana na ofisi yako naishukuru.

Nendeni mkaendelee kutenda haki. Nikiri kwa kweli sikutegemea kama watajitokeza watu 467 na inawezekana kadiri na hao wengine waliochelewa kidogo inawezekana wakafika 500 au mia ngapi.

Ninyi wapitieni, pitieni majalada yao, lakini fanya fast track ya kuhakikisha zoezi hili la hawa watu waliokiri wao wenyewe wanasamehewa na mimi nitafurahi sana hata nikianza kuwasikia hata leo au kesho, keshokutwa watu wanatoka na wanakwenda kuungana na jumuiya zao.

Nawashukuru sana, asanteni sana DPP nakushukuru sana, asante sana. 

5828 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!