Kufikia miaka milioni 1.5 iliyopita kulikuwa na ongezeko kubwa la tabia ya kuua wanyama wakubwa kama inavyoonekana kwenye maeneo mbalimbali ya malikale.

Hali kama hii inaonekana pia katika maeneo mbalimbali ya Bonde la Olduvai. Uuaji wa tembo, twiga, viboko, faru na aina ya nyati wenye pembe kubwa kwa ajili ya chakula ni hali inayoonekana kwa wingi maeneo mengi (FLK-Naorth, SHK, TK na BK).

Uchimbuzi wa eneo la Bk la miaka milioni 1.3 iliyopita ulioendeshwa mwaka 2006 uligundua mlolongo wa tabaka walizoishi zamadamu zikiwa na safu 8 za masalia ya kale; na baadhi zikitoa ushahidi wa kale zaidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kwa utaratibu maalumu na mabaki mengi zaidi yanayodhihirisha uchinjaji; na zaidi ya vipande 500 vya mifupa yenye chale zilizosababishwa na binadamu wakati wa kukata nyama.

Kiasi hiki kikubwa kimewezesha kutengeneza mchanganuo wa mambo yaliyotokea katika mizoga ya wanyama hao kutokana na tabia za zamadamu hao wa awali.

Ushahidi huu pia unadhihirisha kuwa tabia ya kula nyama ilikuwa sehemu ya kawaida ya maisha ya zamadamu wa jamii hii ya erectus. Uwindaji ulikuwa ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na hali ya maisha, japo kazi ya kuwinda wanyama hao wakubwa ilikuwa na hatari zake.

Mpangilio wa shughuli katika maeneo haya ya kuishi ni hatua ya maendeleo ya kudhibiti mazingira, tabia ngeni katika jamii hii tofauti na ilivyokuwa katika jamii zilizotangulia.

Kugunduliwa kwa takriban mifupa yote ya mnyama mkubwa jamii ya twiga wa zamani aliyekuwa na uzito wa karibu kilo 2,000 aitwaye Zivatherium; au wa pelerovis aliyekuwa jamii ya nyati, lakini mkubwa zaidi ya karibuni kilo 1,000, inaonyesha kuwa makundi ya wawindaji yalikuwa makubwa kuzidi enzi za Homo habilis. Ukubwa wa makundi ya uwindaji uliwezesha uvunaji wa wanyama hawa wakubwa ufanikiwe hasa kuanzia miaka milioni 1.5 iliyopita.

Utafiti katika tabaka lenye Oldowan na Acheulian Olduvai

Miaka ya 1970, baada ya kufariki dunia kwa Dk. Louis Leakey, Mary Leakey aliendelea kuishi Olduvai kwa karibu muda wote. Baada ya kutumia miaka 10 akitafakari maeneo ya kale zaidi yenye zana aina ya Oldowan katika tabaka la kwanza, aliendeleza utafiti wake kwenye maeneo yenye tabaka la pili na ndipo alipogundua kuwepo kwa pamoja mitindo miwili tofauti ya zana za mawe, Oldowan na Acheulian.

Baadhi yenye maeneo yenye zana aina ya mashoka makubwa ya Ashulian yalikuwa mbali na ziwa, zana hizi zilitumika kwa kazi tofauti na kuchinja wanyama. Wakati huo huo maeneo yenye zana mtindo wa Oldowan ambazo ni ndogo zilikuwa karibu na ziwa zikiwa na ushahidi wa matumizi yake kuchinjia wanyama.

Pamoja na watafiti kutoyapa kipaumbele maeneo ya aina hii ambayo ni ya tabaka ya miaka milioni 1.8 iliyopita, mabaki ya mifupa yanayopatikana ni ya kuvutia na maeneo ni makubwa kuzidi yale ya tabaka la kwanza. Katika eneo la BK, idadi kubwa ya mabaki ya wanyama wakubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na jamii za zamani za nyati, aina za twiga na tembo.

Katika eneo la SHK, mabaki ya aina ya kiboko aliyechinjwa na zamadamu hawa yalipatikana. Hii ni baadhi tu ya hazina kubwa iliyopo katika tabaka za juu. Kutokana na tabaka la 3 eneo la JK, maelfu ya mifupa ikiwemo ya zamadamu (OH34) yamepatikana, na kutoka tabaka la 4 la miaka 800,000 hadi 600,000 kumeongeza maeneo ya kuvutia (HEB, WK, POK) yaliyotoa zama kubwa kubwa, uwindaji wa wanyama wakubwa na baadhi ya masalia ya zamadamu (OH 28).

Mary Leakey alistaafu mwaka 1986 baada ya kutafiti matabaka haya na hakuna aliyeendeleza kazi hiyo. Ni hivi karibuni mradi wa TOPPP (Tanzania Olduvai Paleontology and Paleoecology Project) kwa kushirikiana na mtafiti wa mambo ya kale, Metin Eren, anayetafiti ukanda wa Ziwa Ndutu walipoanza tena kutafiti matabaka haya. Tayari idadi kubwa ya maeneo mapya yameshagundulika na utafiti unaendelea.

Kaskazini mwa Olduvai, umbali wa kilomita 80, mtoto wa Dk. Leakey, Richard Leakey, aligundua eneo la Peninj mwaka 1963. Mwaka uliofuata, yaani 1964, lilipatikana taya zima la jamii ya zinjanthropus.

Richard Leakey na G. Isaac waliendeleza utafiti huu kwa miaka miwili. Baadaye G. Isaac aliendelea na utafiti mwaka 1981-1983. Eneo hili liliachwa mwaka 1985 hadi miaka 10 baadaye pale kundi la watafiti lililoongozwa na Manuel Dominguez-Rodrigo wa chuo kimoja huko Madrid, Hispania walipoendesha utafiti uliochukua miaka 10 kwenye maeneo ya miaka milioni 1.5 hadi milioni 1.2 iliyopita na kugundua kuwepo kwa pamoja zana za Ashulian na Oldowan, huku Oldowan ikiwa na ushahidi wa uwindaji na uchinjaji wanyama.

Pia, katika mojawapo ya maeneo ya Ashulian kuna ushahidi wa kuchonga au kukata miti kwa kutumia zana hizi. Mwaka 2005 utafiti huu ulibadilika na kuwa chini ya uongozi wa Fernando Diez-Martin wa Chuo Kikuu cha Valladolid, Hispania.

Awamu ya pili ya zana za mawe

Acheulian, ni jina la zana za mawe za awamu ya pili, jina lililotokana na eneo zilikoanza kuonekana kwa mara ya kwanza huko Ufaransa (Saint Acheul).

Ni ufundi unaohusishwa na jamii ya zamadamu waitwao Homo ergaster/erectus waliokuwapo Mashariki mwa Afrika kuanzia miaka milioni 1.7 iliyopita. Zana hizi zinaonyesha umahiri wa hali ya juu na kupanuka kwa mfumo wa kiuchumi na kijamii ukilinganisha na awamu ya kwanza iliyoitwa Oldowan.

Wahunzi hawa walikuwa na uwezo wa kubangua vibanzi vikubwa vya mawe vinavyozidi urefu wa sentimeta 10, na kutengeneza aina mbalimbali za zana kama mashoka na sururu za mawe.

Zana zinazojirudia rudia zaidi ni aina ya mashoka yenye umbo kama samaki (bifaces) zilizochongwa kwa umahiri mkubwa na zenye ukingo wenye makali sehemu kubwa ya mzunguko wake. Zana hizi za awamu ya pili (Acheulian) zilitumika kwa shughuli mbalimbali zilizohitaji nguvu nyingi ikiwa ni pamoja na kuchinja wanyama wakubwa kama tembo, viboko na kukatia miti.

Teknolojia ya Acheulian ilishamiri kuzidi mihula yote ya zana za mawe na ikadumu kwa miaka zaidi ya milioni 1.5 ya chimbuko la binadamu bila kubadilika, na kusambaa maeneo mengi ya Afrika, Ulaya na Bara la Asia; na kuweka msingi wa teknolojia za zana za jamii nyingi mbalimbali.

By Jamhuri