Ukiona ndoto yako haiwatishi watu, jua kwamba ni ya kawaida sana. Ndoto ya kwanza ya Yusufu iliwatisha ndugu zake. Ndoto yake ya pili si kwamba iliwatisha ndugu zake tu, bali ilimtisha hadi baba yake, Yakobo.

Tunaambiwa siku moja ndugu zake walikwenda kuchunga kondoo huko Shekemu na Yusufu alikuwa amebaki nyumbani. Baba yake akamtuma aende  Shekemu akawajulie hali ndugu zake na kuona kama kundi lipo salama.

Alipofika hakuwakuta. Mtu mmoja aliyemwona nyikani akamwambia aliwasikia wakisema wanakwenda Dothani. Yusufu akawafuata huko.

Kabla hajawafikia wakamwona kwa mbali, wakasemezana wao kwa wao, “Tazama yule bwana wa ndoto anakuja.” Wakataka wamuue na wamtupe shimoni, lakini kaka yao Reubeni akawasisitiza wamtupe shimoni na wasimuue. Yusufu alipofika wakamtwaa, wakamvua kanzu yake ile ndefu aliyovaa, wakamtupa shimoni. Bahati nzuri shimo lile halikuwa na maji.

Unapokuwa na ndoto utapewa majina ya ajabu ajabu. Ndugu zake Yusufu walibadilisha jina lake na kumwita, “Bwana ndoto.” Majina ya ajabu ajabu unayopewa kwa sababu ya kuwa na ndoto kubwa ni majina yenye nia ya kukurudisha nyuma uachane na ndoto yako

Jifanye huyasikii.

Ni mara ngapi umeitwa kichaa? Ni mara ngapi umeambiwa, “Unatafuta kiki?” Ukiwa shuleni unasoma kwa bidii ili utapate alama za ndoto zako utaambiwa, “Unasomea kijiji au umetumwa na kijiji.”

Ukiwa kazini unafanya kazi kwa bidii utaambiwa, “Unajifanya unajua kufanya kazi sana au unajipendekeza kwa bosi.” Hayo yote yanasemwa ili yakurudishe nyuma.

Wewe si mtu wa kwanza kupewa majina ya ajabu ajabu. Endelea kuishikilia ndoto yako.

Kuna wakati watu walimsema Yesu, “Je huyo si mtoto wa fundi seremala?”

Ukiona watu wamekazana kupinga ndoto yako jua kwamba ndoto yako ni ya kweli na inakaribia kuwa katika uhalisia. Mara nyingi ukiwa na ndoto kubwa watu wanaweza kupenda ufanikiwe, lakini usifanikiwe zaidi yao. Hivyo, watatumia jitihada nyingi kukurudisha nyuma.

Haijalishi umeambiwa ndoto yako haiwezekani na marafiki zako au hata familia yako, ukweli ni kwamba ndoto yako inawezekana kuwa kweli. Hata ukitupwa shimoni kama Yusufu unaweza kutoka na kufanya mambo makubwa.

Wakorea wana msemo usemao, “Usitishwe na kivuli, kinaonesha kwamba jua lipo karibu.” Watu wanaopinga ndoto zako ni dalili kuwa ndoto yako wanaona inaweza kuwa kweli hivyo wanaweka nguvu zao nyingi kukurudisha nyuma. Watu wenye hekima hawakukosea waliposema, “Dalili ya mvua ni mawingu.” Ukiona watu hawapingi ndoto zako jua kwamba ndoto hizo ni za kawaida sana.

Unahitaji kujiamini na kuwa jasiri pale ambako kila mtu anaonesha kuipinga ndoto yako.

Unahitaji kujiamini pale watu ambao ulikuwa ukiambatana nao wanapokuacha peke yako.

Unahitaji kujiamini pale ambako hata mwenza wako wa ndoa  haamini tena katika ndoto yako na amekuacha upambane peke yako. Yusufu alijiamini. “Kujiamini! Kujiamini!

Kujiamini! Huo ni mtaji wako,” alisema John Wanamaker.

Kujiamini huleta ujasiri. Ili ndoto iweze kutimia unahitaji ujasiri wa aina tatu:  Ujasiri wa kwanza kabisa wa kuwa nao ni ujasiri wa kuanza. Watu wengi wana ndoto  kubwa, lakini kuchukua hatua na kuanza kuzifanyia kazi ndoto zao kumekuwa kikwazo kikubwa. Usikae na kusubiri kila kitu kikamilike ndipo uanze. Anza na ulichonacho.

Mungu alipomchagua Musa kuwaongoza wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri kwenda nchi ya ahadi, Musa akaanza kumwambia Mungu kwamba hawatamuamini wala kumsikiliza. Mungu akamuuliza, “Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako.” Akasema “Ni fimbo.” Mungu akaanza na ile fimbo. Anza na alichonacho mkononi.

Ujasiri wa pili unaohitaji ni ujasiri wa kukabiliana na maumivu. Mtaka cha uvunguni sharti ainame. Ukitaka kutimiza ndoto yako kuna maumivu utahitaji kuwa tayari kuyapitia. Mandela aliwahi kusema, “Kwenye nchi yangu, kwanza unakwenda gerezani halafu unakuwa rais,” huyu ni Yusufu aliyekubali maumivu ili kutimiza ndoto yake.

Ujasiri wa tatu unaohitaji kuwa nao ni ujasiri wa kuendelea. Watu wengi hukata tamaa baada ya mambo kutosonga mbele. Ili utimize ndoto yako kushindwa ni mojawapo ya njia sahihi ya kuitimiza ndoto yako. “Kushindwa kunaandikwa na penseli.” Anasema David D. Ireland.

Please follow and like us:
Pin Share