Hoja nzito za Lowassa kuelekea Ikulu 2015

lowassaMgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa, amesema: “Watanzania tuna fursa ya pekee kuuondoa utawala wa CCM madarakani na kuleta mabadiliko ya kweli nchini.”

Lowassa amesema hayo, katika salamu zake kwa Watanzania katika kitabu cha ilani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yenye mtazamo wa pamoja wa vyama shirika vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mbali ya Chadema, vyama vingine vinavyounda umoja huo ni National League for Democracy (NLD), Chama cha Wananchi (CUF) na The National Convention for Construction and Reform – Mageuzi maarufu kwa jina la NCCR–Mageuzi.

Lowassa anasema kwamba hayo yanawezena kupitia sanduku la kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Anasema kwamba ilani hiyo ni dira ya maendeleo na kuondoa umaskini itakayosimamiwa na Ukawa, lakini “Azma hii haiwezi kuhitimika bila ushiriki wa kila Mtanzania anayependa maendeleo na kuitakia nchi yetu heri kuniunga mkono mimi, mgombea mwenza, mgombea wa Urais Zanzibar, wabunge/wawakilishi na madiwani kupitia Ukawa.”

Amewataka Watanzania kumsikiliza na kusoma ilani hiyo kwa makini, kuitafakari na kujiridhisha ikilenga kuivusha Tanzania kutoka mashaka, unyonge, umaskini na kukata tamaa kwa wananchi kulikosababishwa na mfumo mbovu wa CCM inayotawala sasa.

“Utawala wa CCM umejaa rushwa na ufisadi kwenda kwenye serikali itakayojengwa na mfumo wa utawala bora wenye kupelekea kuwa na Taifa lenye neema, matumaini na maendeleo ya kweli,” anasema Lowassa katika ilani hiyo ambayo gazeti hili imechapisha.

Kwa upande wake, Juma Duni Haji, mgombea mwenza wa Urais wa Lowassa anasema kwamba “Zaidi ya miaka hamsini ya Uhuru na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika bado nchi yetu inakabiliwa na matatizo ya kimsingi ikiwemo rushwa na ufisadi.”

Anasema kwamba elimu, mfumo wa afya na miuondombinu duni, umaskini, ukiukwaji wa haki bado ni sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania na kwamba kupitia ilani hiyo Ukawa imelenga kumkomboa kila mwananchi kutokana na hali kandamizi ya utawala wa CCM, kuondoa umaskini, kuleta maendeleo na kusimamia haki na usawa.

“Vilevile tutaimarisha udugu na ushirikiano wa pande zote za Muungano kwa misingi ya haki na usawa,” anasema Haji maarufu nkama Babu Duni na kusisitiza: “Tafadhali soma ilani hii.” Ifuatayo ni neno kwa neno kutoka katika ilani ya Chadema. Fuatilia.

 

UTANGULIZI

Historia inaonyesha kuwa Vyama vikongwe Barani Afrika vimeanguka kutokana na sababu mbalimbali hasa kukithiri kwa  umasikini  na  ukosefu  wa  ajira;  ajira  za  upendeleo; kukua kwa matabaka hasimu kwenye jamii; rushwa, ufisadi, ubadhirifu na matumizi ya anasa serikalini.

CHADEMA inatambua sababu kuu nne zilizosabisha nchi yetu ifike katika umaskini uliokithiri wakati inazo rasilimali za kutosha. Sababu hizo ni:

1. Ukosefu wa katiba ya wananchi ambayo ingewapa mamlaka ya kuwadhibiti watawala.

2. Ukosefu wa uongozi wenye uzalendo, uadilifu na utawala bora ambao umepelekea uzembe na kutowajibika; na kukithiri kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

3. Kufanya uchumi utumikie siasa badala ya siasa kutumikia uchumi – kupuuza ushauri wa kitaalamu katika sera, mipango na utekelezaji.

4. Ukiritimba wa Madaraka wa Chama kimoja.

Viashiria vinaonyesha kwa kiasi kikubwa kuwa tayari serikali ya CCM ni dola inayoanguka. CHADEMA na UKAWA wanadhamiria kuunda serikali itakayoondoa mambo yote hayo ili kujenga upya Taifa imara kwa manufaa ya Watanzania wote.

Lengo kuu kwa ujumla katika ilani hii, ni kuhuisha uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika uongozi wa nchi ambao ndio msingi mama wa kuleta maendeleo ya jamii ya Watanzania. Ili tuweze kutoka hapa tulipo tunahitaji uongozi utakaozingatia yafuatayo ambayo ndiyo msingi wa ilani hii:

 

• Kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa

• Kuleta  Katiba  ya  Wananchi  inayosimamia  haki  na usawa

•  Kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa misingi ya usawa

• Kuleta fikra ya Watanzania kujiamini na kujitegemea

kama Taifa huru

• Kuimarisha Uzalendo na Uadilifu

• Kujenga Uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini

• Kuimarisha Huduma za Jamii

• Kuwajengea mazingira mazuri na kuwapa kipaumbele

Walemavu katika sekta zote

• Kujenga Utendaji  bora na Uwajibikaji katika sekta ya

Umma

• Kujenga Ushirikiano wa karibu baina ya Serikali na sekta binafsi

• Kudumisha na kuendeleza uhuru wa mawazo, uhuru wa kutoa na kupata habari na kujumuika na watu wengine

• Ulinzi thabiti na usalama wa raia.

• Ushirikiano wa Kimataifa  wenye tija na Ujirani mwema. 

Ni dhamira ya CHADEMA na UKAWA kuunda serikali makini,

adilifu na inayowajibika kwa umma, katika kuendeleza falsafa

ya CHADEMA msingi wa juhudi zote za maendeleo za uchumi na kijamii zitalenga kwenye kuondoa umaskini na kuelekea kwenye taifa la uchumi wa kati na hatimaye lililoendelea. Vipaumbele wa mwelekeo huo ni kama ilivyoelezwa kwenye sura zinazofuata kwenye ilani hii.

 

Wakati na Fursa ya Kufanya Mabadilikoni ni Sasa

Ilani hii inaainisha maeneo na vipaumbele vitakavyozingatiwa na CHADEMA na UKAWA mara watakapopata fursa ya kuunda serikali. Serikali mpya ya UKAWA inalenga katika kujenga uchumi imara na shirikishi na kuunda serikali ndogo yenye kuzingatia uadilifu, ufanisi, tija, uzalendo, uwajibikaji na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za nchi. Serikali itabadili mfumo wa utawala uliopo kutoka utawala kandamizi, kwenda utawala unaoheshimu wananchi na matakwa yao. Ilani hii sio ahadi bali ni Dira ya Taifa letu chini ya serikali ya CHADEMA/ UKAWA na inayotekelezeka.

Kwa ufupi, Ilani hii inabeba maono na mwelekeo wa CHADEMA na vyama vinavyounda UKAWA kwa lengo la kuomba ridhaa ya wananchi ili kuanza ujenzi mpya wa Taifa letu kwa kipindi cha miaka Mitano (2015-2020).

 

Ndugu Mtanzania,

Safari ya Mabadiliko ya kweli inaanza sasa. Ungana na CHADEMA/UKAWA uwe sehemu ya mabadiliko haya ambayo Watanzania wameyatafuta kwa muda mrefu. Tumia fursa hii adhimu uliyonayo ya uchaguzi kufanya mabadiliko.

 

Kuondoa Umasikini, Chagua CHADEMA/UKAWA.

• Mchague Mh. Edward Ngoyai Lowassa -Rais

• Mchague Mh. Juma Duni Haji- Makamu wa Rais

• Chagua Wabunge/Wawakilishi kutoka UKAWA

• Chagua Madiwani kutoka UKAWA

 

FALSAFA NA MISINGI YA SERA NA ITIKADI YA SIASA ZA CHADEMA

Misingi ya ilani CHADEMA imejengwa juu ya falasafa ya NGUVU NA MAMLAKA YA UMMA na itikadi ya MLENGO WA KATI; na ni kama ifuatavyo:

 

Misingi itokanayo na Falsafa:

• Umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na mwisho kuhusu hatima ya nchi.

• Nguvu na Mamlaka ya Umma vitajenga na kudumisha

Demokrasia kuendana na katiba.

• Nguvu na Mamlaka ya Umma ndiyo msingi wa kuhoji na kuwajibisha uongozi uliochaguliwa kwa uhuru na kwa haki.

• Nguvu na Mamlaka ya Umma ndiyo chombo cha kuwaamsha, kuwahamasisha,    na    kuwaelimisha Watanzania  waimiliki, waitawale, wailinde, waiendeshe na waiendeleze nchi kwa ubunifu ili wanufaike nayo.

Misingi itokanayo na Itikadi:

• Kukuza na kuimarisha uchumi wa soko huru lisilokuwa holela, kupitia rasilimali ili umma unufaike.

• Kuthamini umuhimu wa familia, uzalendo na mila na desturi zilizo nzuri.

• Kusimamia zaidi maslahi ya Taifa kuliko ya vyama vya siasa.

• Kujenga uwiano bora kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma.

• Uhuru wa kuabudu bila kuingiliana na dola.

• Kuwajengea uwezo wananchi kumiliki na kuendesha uchumi.

• Kila mtu kutimiza malengo yake na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake.

 

Kuleta Mabadiliko

Ili tuweze kuleta mabadiliko ya kweli katika uchaguzi huu wa mwaka 2015, kuna mambo mawili ya msingi ya kuzingatia.

• Ni muhimu tuelewe na tuwe wakweli juu ya chanzo cha matatizo yetu na ni kwa namna gani tumefika hapa tulipo leo. CHADEMA/UKAWA tunaamini kwa dhati kuwa tatizo mama lililotufikisha hapa tulipo ni udhaifu wa  kimuundo,  kiutendaji  na  kiuongozi  uliojengwa na Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya miaka 50. CHADEMA/UKAWA tutajenga Taifa letu kwa kufanya mabadiliko makubwa na ya haraka ya kiutendaji, kimuundo na kiuongozi ili kurudisha uwajibikaji katika ngazi zote za utawala wa nchi. Hili ndilo litakuwa lengo kuu la utendaji wa Serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.

• Watanzania tutambue kwamba tukiamua kwa dhati na kuchukua hatua katika uchaguzi huu wa Oktoba

2015 tuna uwezo wa kubadili hali ya kiuchumi na kijamii tuliyo nayo kutoka taifa lenye uchumi mdogo kabisa duniani na kuwa taifa lenye uchumi wa kati na hatimaye taifa lililoendelea kiuchumi na kijamii. Uchaguzi huu ni nyenzo muhimu na ya pekee ya kuweza kubadili hali ya nchi yetu na kurudisha matumaini kwa Watanzania wote bila kujali hali, itikadi, rangi, kabila, dini au kitu kingine chochote ambacho kinaweza kumtofautisha Mtanzania mmoja mmoja au kwa makundi mbalimbali.

 

Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA2015

Maadili na uadilifu

• Tanzania ni nchi yenye historia iliyoundwa na maadili, uadilifu na uzalendo. Waasisi wa Taifa hili walikuwa na ndoto ya Tanzania ambayo ingejengwa katika misingi hiyo.

• Ni matumaini ya CHADEMA/UKAWA kwamba mabadiliko ambayo wananchi wameamua kuyafanya juu ya uongozi wa nchi yao yanarejesha maadili, uadilifu, uzalendo pamoja na nidhamu katika uongozi wa nchi na watanzania kwa ujumla.

• CHADEMA/UKAWA wana jibu la ndoto za watanzania.

Ni dhahiri na ni kweli kwamba tumekosea njia kama Taifa, hivyo ni sisi wananchi tunaotakiwa kujikosoa, kubadili  njia  potofu  na  kurudi  katika  misingi  sahihi ili  kuhakikisha  kwamba  tunakuza  usawa  kati  ya watu wetu chini ya utawala ya sheria na viongozi wanaoongoza kwa mfano. Tumia kura yako kwa usahihi ili uweze kusahihisha makosa yaliyokwisha tokea kwa kuchagua CHADEMA/UKAWA.

• CHADEMA/UKAWA tunaamini   kwamba tunahitaji kurudi katika misingi hiyo upya na tunaona fahari kubwa kuitangaza na kuisimamia kwa niaba ya watanzania wote. Falsafa yetu ni nguvu ya umma na Umma ndio wenye mamlaka ya mwisho katika mustakabali wa Taifa kwani ndiyo wenye mamlaka ya kuweka viongozi madarakani na kuwawajibisha kiutendaji pale watakavyofanya    kinyume    na matarajio yao.

 

KATIBA YA WANANCHI NA MABADILIKO MAKUBWA YA MFUMO WA UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI WA SERIKALI NA KURUDISHA UZALENDO

 

Hali halisi

Katiba ya wananchi

• Kutokuwa na katiba bora kumewanyima Watanzania mamlaka ya kuwajibisha viongozi wao, kukosekana kwa dira, tunu za Taifa, maadili na miiko ya uongozi; na kukosa Muungano ulio imara kimuundo.

• Pia kukosekana kwa katiba ya wananchi kumepelekea mfumo wa serikali kiutendaji kuwa mbovu kwani hakuna vyombo huru kama Taasisi ya kupambana na rushwa, ofisi ya mkaguzi mkuu wa serikali, mahakama na vyombo vya dola.

• Kutokuwepo kwa ugatuzi wa kweli wa mamlaka ya serikali kuu kwenda karibu na wananchi  kumepelekea watanzania kutoshiriki katika maamuzi ya vipaumbele vyao na kutoshirikishwa katika kupanga na kuisimamia bajeti za maendeleo yao kikamifu na hivyo kuzorotesha

maendeleo.

 

Utendaji na Uwajibikaji

• Pamoja na uwepo wa sheria na miongozo thabiti ya utumishi wa umma, poromoko kubwa la maadili katika uongozi na jamii kwa ujumla limepelekea watumishi wachache kutimiza wajibu wao kwa ufanisi na kwa muda  stahiki  huku  kukiwepo  na  ongezeko  kubwa la uzembe, rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma miongoni mwa viongozi wa kisiasa  na  watumishi wa umma. Hii inachangia rasilimali kubwa ya nchi kutonufaisha wananchi wengi badala yake wachache hasa walio kwenye madaraka. Vile vile ukosefu wa umakini, nidhamu, ubunifu na uthubutu katika utendaji kazi kumesababisha utendaji mbovu wa serikali na kutowajibika  kwa  watumishi  wa  umma.  Sababu  hizi kwa pamoja kwa kiasi kikubwa kumechangia kudorola kwa uchumi wa Taifa letu.

• Kutokokuwepo  kwa  uhuru  wa    vyombo  vya  habari na hivyo kupelekea kutoibua na kuwajuza wananchi maovu ya serikali ikiwemo rushwa na ufisadi.

• Watumishi hasa sekta ya umma kutohamasika kufanya kazi kwa bidii kunatokana na maslahi duni na mishahara isiyo na uhalisia na hali ya maisha kwenda na ujuzi, nafasi na vyeo kazini.

 

Fursa iliyopo

• UKAWA iliyoanzishwa  kutetea  katiba  ya  wananchi ilisusia bunge la katiba lililokuwa chini ya wingi wa CCM ambalo lilitupa maoni ya wananchi. Sasa umoja huu umeimarika na sasa unaingia katika uchaguzi ukiwa kitu kimoja na lengo kuu likiwa ni kushinda uchaguzi ilikuwaletea   Watanzania   katiba   bora.   Upinzani unaunganishwa na kutaka kupitishwa katiba mpya  ya mabadiliko ya jinsi tunavyoongozana kama vile kuwa na muundo wa serikali tatu yaani serikali ya Zanzibar, serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano yenye usawa ambayo itaimarisha muungano, bunge na baraza dogo la mawaziri la serikali ya Muungano.

• Uimara  wa  upinzani  wa  kusimamia  hoja  za  kitaifa bungeni na nje ya bunge unatoa fursa kwa UKAWA kuunda serikali itakayosimamia sheria na miongozo ya serikali yenye kufuata haki kwa kila mtanzania ili kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa serikali na wananchi kwa ujumla.

 

CHADEMA itafanya nini

• Katiba ya  wananchi  ni  kipaumbele  namba  moja, hivyo serikali ya CHADEMA itaanzisha tena mchakato wa katiba uliozingatia maoni ya wananchi. Lengo ni kuhakikisha kwamba vifungu vinavyohusu tunu, maadili na miiko ya uongozi vinakuwa kwenye katiba mpya ili sheria na kanuni mpya ziweze kutungwa na kudhibitiwa

• Kujenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku

• Kuimarisha  nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika

Sekta ya Umma

• Kuimarisha mchango wa Wataalam katika uendeshaji wa nchi

• Kusimamia ukusanyaji na matumizi mazuri ya kodi na mapato ya serikali na kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi

• Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa watumishi wa

Umma

• Ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi kwa wafanyakazi ili kupunguza ukali wa maisha

• Kwa mtumishi atakayependa, atalipwa mshahara wa mwezi kwa awamu mbili katika mwezi ili kwendana na uhalisia wa hali ya maisha na kupunguza kukopa kopa kusiko kwa lazima

• Kudhibiti  na  kupunguza  matumizi  ya serikali ikiwa  ni pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku matumizi ya magari ya anasa serikalini (mashangingi)

• Kudhibiti  deni  la  Taifa  kwa  kuanza  na  ukaguzi wa madeni ya serikali ili kuhakiki  jinsi yalivyotumika

• Kuimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za serikali  na  kuweka  bayana  mikataba  yote  ya  nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia ili watanzania waweze kuihakiki na Bunge lao liikubali kabla ya kupitishwa na serikali

• Kuzingatia na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari kwa kuhakikisha kwamba tunafuta sheria zote ambazo zinaingilia uhuru wa vyombo hivyo

• Kuimarisha serikali za mitaa ili wananchi washiriki kikamilifu katika maendeleo yao.