Safari ya Dk. Magufuli Ikulu (2)

nmb-4Mgombea Mwenza wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amegundua Watanzania wanahitaji mambo mengi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Katika mahojiano maalum yaliyofanyika wiki iliyopita Dar es Salaam, Samia anaeleza kuhusiana na kile alichokiona ikiwa ni pamoja na njia za kuondokana na kero hizo za wananchi wanaoonekana kuhitaji mabadiliko.

Samia anasema kuna kasumba ya wafanyakazi wa Serikali kufanya kazi kwa mazoea, huku wengine wakishindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo, hivyo lawama kuelekezwa kwa Serikali Kuu na chama tawala.

Kwa msingi huo, amewataka wananchi wamchague Dk. John Magufuli ili aingie naye Ikulu, lakini si kwa malengo ya kukaa kwenye kiti kwa muda mrefu, badala yake atakuwa ni mtu wa field (kwenda maeneo ya kazi) zaidi.

“Sitakaa ofisini kusubiri kuletewa ripoti zilizopikwa ambazo hazikufanyiwa kazi ipasavyo, huku miradi mingi ikitelekezwa na fedha za miradi hiyo zikiishia kwenye warsha na makongamano yasiyo na tija kwa Taifa,” anaapa Samia.

“Sitapenda kuwa kiongozi wa kufungua makongamano na miradi mara kwa mara, bali nitakuwa msimamizi na mkaguzi wa kila mara ili kuondokana na tabia iliyojengeka miongoni mwa jamii,” anasema.

Anasema kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja alichozunguka kutafuta kuungwa mkono na Watanzania, amegundua kuwa changamoto kubwa kwa Watanzania ni maji.

“Nitasimamia na kuhakikisha tunaboresha huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 67.7   mpaka asilimia 85 kwa kipindi cha miaka mitano tu,” anasema Samia.

Anasema kwamba Serikali ya Dk. Magufuli ina lengo la kuwapatia wananchi waishio vijijini huduma ya maji safi na salama kama yalivyo malengo ya milenia.

Anasema hii ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

Anakiri fedha nyingi kuhitajika katika kufanikisha hilo, lakini akatoa siri kuwa kuna fedha kutoka Benki ya Dunia ambazo wakiingia Ikulu watazitumia ipasavyo kwa kujenga visima na mabwawa makubwa yatakayohudumia wananchi wengi kwa wakati mmoja.

Mpango huo unakwenda sambamba na kuboresha miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga huku mradi wa maji wa Chalinze awamu ya tatu, Same, Mwanga, Korogwe na mradi mwingine katika mikoa mipya ya Katavi, Njombe, Geita na Simiyu.

Kuhusu afya, Samia anakiri kuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vitendea kazi katika suala linalohusu afya nchini ambavyo ni vifaa tiba.

Anasema hospital yoyote ile, ni lazima iwe na vipimo na dawa siyo kumuona tu daktari halafu “unaambiwa ukanunue dawa, hiyo si hospitali bali ni nyumba ya daktari.”

“Ni lazima kuhakikisha tunaondokana na nyumba za daktari tunakuwa na hospitali. Kila Mtanzania ana haki ya kupatiwa matibabu ya kuridhisha ikiwa ni pamoja na mazingira kuwa rafiki.

“Wizara ya Afya tayari nimeona wametengeneza mfumo mzuri wa kufuata dawa kwenye bohari kisha kuzipeleka moja kwa moja kwa daktari, utaratibu utakaowezesha kila mtu kupata dawa katika hospitali atakayokwenda kutibiwa,” anasisitiza. Anasema kila mmoja wao ameongelea suala la huduma ya mama na mtoto, lakini kwake anajihakikishia kujenga majengo ya kisasa yasiyopungua kumi ya mama na mtoto.

Anatambua kuwa huo ni mradi mkubwa unaohitaji fedha nyingi ambazo atatafuta wafadhili wa ndani na nje, ili kuigeuza ndoto yake katika uhalisia kwa malengo ya kumkomboa mama na mtoto – wanakuwa salama.

Katika eneo hilo la afya, anazungumzia pia Watanzania kutibiwa kwa kutumia bima kama zilivyo nchi nyingine, kwani kila raia atakuwa na uhakika wa matibabu bila kuhofia gharama za matibabu kwa watu wa kipato cha chini.

“Ili kufanikisha kila mmoja anapata matibabu yanayostahili kwa kutumia bima za afya, ni vituo vyote vya afya kuanzia ngazi za chini kuwa na vifaa vyote vya tiba bila kujali ukubwa wala udogo wa kituo hicho au hospitali hiyo,” anasema.

Anasema hatua hiyo itaondoa msongamano mkubwa katika hospitali za wilaya na mikoa huku zile za rufaa zikishughulika na magonjwa ya rufaa.

Kuhusu gharama za ujenzi ambazo zimetofautiana kutoka eneo moja na jingine, Samia anasema baada ya kuzunguka katika mikoa mbalimbali amepata fursa ya kuona gharama za ujenzi nafuu na imara unaofanywa na Watanzania.

Anasema nyumba zinajengwa kwa matofali ya kuchoma, zinavutia na hata nchi zilizoendelea katika sekta mbalimbali wanautumia nyumba zilizojengwa kwa aina hiyo ya matofali yanayoandaliwa kwa ubora wa juu ili yadumu.

Ili kufanikisha mpango huo, Samia anasema Serikali yao itaunda vikundi vya vijana watakaopatiwa mafunzo kwa ajili ya kazi hiyo ya kuandaa matofali.

“Hii itasaidia mambo mengi. Itapunguza hata pengo la ajira kwa vijana. Tutajenga mabweni ya shule za sekondari nchini kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili kuwaepusha na mambo mengi wanayokumbana nayo na kujikuta wakishindwa kuendelea na masomo,” anasema.

Mbali ya maeneo hayo, kadhalika Samia anazungumzia kilimo na wakulima nchini, akirejea hata kwenye nembo ya jembe kwenye alama kuu za bendera ya CCM. Alama za bendera hiyo ni jembe na nyundo zinazoleta tafsiri ya wafanyakazi (nyundo) na jembe kwa wakulima.

Anasema kitakachofanywa na Serikali yao ni kuwaunganisha wakulima ili kuwa na nguvu na sauti ya pamoja na kuwasogezea viwanda vidogovidogo ambavyo watavitumia kwa kuboresha mazao yao na kutouza malighafi.

“Tunaweza kupeleka viwanda hivyo na kuhakikisha hakuna mtu atakayeuza tena mahindi bali watauza unga,” anasema Samia na kuongeza: “Hayo yote chini ya Dk. Magufuli yanawezekana.”

Anasema kutakuwa na mamlaka maalum kwa ajili ya kurasimisha biashara ndogondogo ambazo kazi yake ni kuhakikisha utaratibu wa kuuza malighafi hauendelei.

Samia anasema kwamba hilo na hayo mengine atayasimamia na yeyote (waziri au wizara husika) atakayepewa mamlaka hayo atabanwa kuhakikisha anatimiza majukumu yake ipasavyo.

Anasema malengo ya CCM ni kufufua vyama vya ushirika kwa kuwaondolea wakulima kero zote zilizopo katika vyama vilivyopo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua stahiki wale wote waliofanya ubadhirifu katika vyama hivyo.

Anasema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri kwa sababu umeweza kuwasaidia watu wengi nchini Ethiopia, lakini kwa Tanzania hauendeshwi kadiri inavyohitajika hivyo kuonekana kuwa mfumo mbovu.

“Haiwezekani mkulima akopwe kila uchao, huku ni kumkatisha tamaa,” anasema Samia ambaye alipata kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba chini ya Mwenyekiti, Samuel Sitta.

Kuhusu kutimiza hayo yote kwa kipato cha ndani, Samia anafarijika akisema “Ukweli Mwenyezi Mungu ametubariki kuwa na rasilimali nyingi. Hilo ni la kujivunia.”

Anaendelea kusema kuwa CCM ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanaziba mianya yote ya upotevu wa mapato za umma.

“Mfano mzuri ni Bandari ya Dar es Salaam ambayo ina madudu mengi ila masuala ya uchumi namwachia rais wangu, Dk. John Magufuli,” anasema.

Kadhalika, Samia anazungumzia mazingira ambako Serikali imeunda wizara iliyo chini ya Makamu wa Rais, akisema “katika ofisi yangu wimbo wa kila siku utakuwa utunzaji wa mazingira kwa vitendo.

“Nimezunguka na kuona ni kwa jinsi gani kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nchini. Nilikuwa na alama ya kunionesha nimefika Mkoa wa Morogoro baada ya kuona maji yakitiririka kutoka milimani, lakini hivi sasa hayaonekani tena, hii ni hatari, lazima turudishe hali ilivyokuwa.”

Anasema hakuna budi kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji ambako yeye atasimamia kwa vitendo siyo kuishia kudanganywa.

Anasema atakwenda kushiriki kupanda miti na mchakato huo hautaishia hapo tu bali kufuatilia miti hiyo na kuhakikisha inatunzwa kila mji, kila wilaya, kila mkoa.

Anakiri kuwako kwa tatizo kubwa la watu maarufu kujenga kwenye mkondo wa maji hasa katika miji mikubwa. Wapo watu wamejenga majumba yao makubwa ufukweni ambako hakuruhusiwi, wanapotakiwa kuvunja nyumba zao wanakimbilia mahakamani.

“Nakuhakikishia wale wote waliojenga nyumba zao kwenye vyanzo vya maji, kwenye mkondo wa bahari, maeneo yote yasiyoruhusiwa wajiandae maana sitakuwa na huruma.

“Tutazivunja tu hizo nyumba zao. Haiwezekani watu wengine wavunjiwe mtu mmoja au wawili wakimbilie mahakamani nyumba zao zisiguswe, wakati wanajua kabisa kuwa wamevunja sheria.”

Anasema kila mwananchi ana haki ya kufuata sheria za nchi bila kujali madaraka na umaarufu wake, na hivyo atafuatilia na kusimamia mwenyewe kujiweka kando na kunyenyekeana na kubembelezana katika kufuata sheria zilizopo.