Dk. John Magufuli, wiki hii anaapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anaanza kazi ngumu aliyoiomba kwa ridhaa yake mwenyewe, ya kuwatumikia Watanzania wote.

Kwenye kampeni zake, Dk. Magufuli, aliomba kura huku akiahidi kuwa endapo atachaguliwa, atahakikisha anatumia nguvu na vipawa alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania wote bila kujali kanda, dini, makabila, jinsi, rangi wala itikadi zao.

Hii ni ahadi nzito na njema ambayo bila shaka yoyote iliwaongezea imani wapigakura.

Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, amepata kura zaidi ya milioni 6. Hizi ni kura nyingi. Kwa maneno mengine ni kuwa watu waliompiga Dk. Magufuli, wapo; na njia pakee ya kuwafanya wampe ushirikiano ni kuhakikisha anatekeleza ahadi zake, zikiwamo hizo za kuwapa wananchi maendeleo bila upendeleo wowote.

Tunampongeza Dk. Magufuli, kwa sababu amepata nafasi kama Mtanzania, ya kuwatumikia Watanzania wenzake. Utumishi wa aina hii ni wa kuomba, na kwa kweli malipo yake ni kutekeleza matakwa ya wananchi.

Rais Magufuli, anashika madaraka nchi yetu ikiwa imeathiriwa na mambo kadhaa yakiwamo yaliyotokana na kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Kwa mfano, uchaguzi huu umeibua vimelea hatari vya ukanda na hata udini. Tumeona wagombea wa makabila fulani wamepata kura nyingi katika maeneo fulani, na wengine wamekosa kura katika maeneo kadhaa kwa sababu si wa maeneo hayo kwa asili.

Huu ni ufa mbaya kwa Taifa letu. Ni wajibu wa Rais Magufuli, kuhakikisha anavunja vunja vimelea hivyo kwa kuwafanya Watanzania warejee na wajione kuwa ni wamoja.

Nchi yetu bado ni ya kupigiwa mfano kwa suala la amani na mshikamano. Haikushangaza kuona wageni waliokuja wakati wa uchaguzi wameondoka wakishangaa namna amani na utulivu vilivyotamalaki.

Ndiyo maana tunamuomba Dk. Magufuli, kwa hekima na busara aendeleze hali hii bila kusahau kulishughulikia suala zito la mgogoro wa uchaguzi Zanzibar.

Hali ya mambo ilivyo Zanzibar inatia shaka, hasa pale inapoonekana kuwa katika pande zote mbili zinazoshindana, hakuna ulio tayari kukubali kushindwa.

Dk. Magufuli, Watanzania wana kiu kubwa ya kuona akiendeleza mema yote ambayo mtangulizi wake ameyaacha, na kuyatupa kabisa yale yote wanayoamini kuwa hayana tija kwa nchi yetu.

Tunampongeza kwa ushindi wake, na wakati huo huo tukiwapongeza wale wote walioshiriki kuhakikisha amani na utulivu wetu vinaendelea kudumu hata baada ya kuwa wameshindwa. Mungu akubariki Dk. Magufuli, na uhakikishe Serikali yako inakuwa Serikali ya waadilifu kweli. Watanzania wanataka mabadiliko. Kupitia kwako, bila shaka watayapata. Hongera sana.

1224 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!