Julai 1 na 2 zilikuwa siku za pekee katika historia ya Tanzania. Tanzania ilihitimisha kilele cha ugeni mkubwa kuja hapa nchini ndani ya mwaka mmoja. Katika siku hizi taifa lilikuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Marekani, Barack Obama.

 

 

Rais Obama amekuja ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya ujio wa Rais wa China, Xi Jinping, Machi 24, 2012. Ugeni wa Obama umekolezwa na uwape wa Rais George W. Bush na mkewe, waliotua nchini Julai 2, 2013. Ukitilia maana kuwa Tanzania wakati huo huo ilikuwa na mkutano wa Smart Partnership uliokusanya marais 11 na wakuu wa nchi 5 na wake wa marais wote barani Afrika, basi hakika kilikuwa kishindo.

 

Naweza kusahau, hivyo ni vyema nianze kwa kuwapongeza Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwa kuwezesha ujio wa ugeni huu mkubwa. Pongezi hizi wala sizitoi kimakosa. Ugeni huu mkubwa haukuja hivi hivi; kuna kazi nzuri iliyofanyika.

 

Hapa ndani tunaweza kuwa na siasa zetu, lakini unapofika wakati wa kusema ukweli, basi yatupasa tufanye hivyo. Pengine hapa nimpongeze pia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kukubali kushiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Serikali kwa ajili ya Rais Jakaya Kikwete.

 

Sitanii, mimi ni msomaji wa magazeti. Nilisoma gazeti la Tanzania Daima la Juni 30, likasema Chadema wameamua kususia ziara ya Rais Obama. Sababu zilizotolewa sitazitaja, maana mliobahatika mlizisoma. Namshukuru Mbowe kwa kuwa juu ya siasa changa za kudhani kususia mahindi shambani unawakomoa ngedere wanaorukaruka.

 

Nimempongeza Membe si kwa jingine. Wanaojua historia ya diplomasia na jinsi diplomasia inavyofanya kazi, watakubaliana na mimi kwamba Membe au Waziri wa Mambo ya Nje katika lolote liwalo anakuwa wa kwanza kulifahamu katika nchi, kisha analipeleka kwa Rais kama taarifa au kupewa maelekezo.

 

Maelekezo yoyote anayotoa Rais kwenda nchi yoyote ya kigeni, yanapitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, ambaye naye anayapeleka kwa Balozi wa nchi hiyo, kisha Balozi naye anawasilisha kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake, na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo anawasilisha kwa Rais wake. Mzunguko uko hivyo, kidiplomasia Rais ni Namba 1 na Waziri wa Mambo ya Nje ni Na 2.

 

Kwa mantiki hiyo, ikitokea Waziri wa Mambo ya Nje akabofoa, basi na Rais wake atabofoa pia. Ikiwa Membe amefanya vizuri, basi hata Rais Kikwete ataonekana amefanya vyema. Ndiyo maana nasema ugeni huu huwezi kuutenganisha na Membe na Kikwete.

 

Sitanii, faida za ugeni huu ukiacha za moja kwa moja kama mikataba mbalimbali tutakayoingia, zipo faida nyingine nyingi ikiwamo kukuza utalii. Kwa mfano. Mwaka 2000 wakati Tanzania inatembelewa na Rais Bill Clinton, idadi ya watalii waliokuwa wanakuja hapa nchini walikuwa 450,000.

 

Baada ya ziara ya Clinton, idadi ya watalii iliongezeka hadi 750,000 kwa mwaka. Mwaka 2008 baada ya Rais Bush kuitembelea Tanzania alikuta watalii wakiwa idadi hiyo hiyo, lakini hadi Desemba 2012, idadi ya watalii kutokana na ujio huo na jitihadi nyingine, imeongezeka na kufikia 1,200,000.

 

Leo mwaka 2013 tumepata ujio wa Rais Xi Jinping na Barack Obama, napenda kuamini kuwa watalii wataongezeka na kufika 2,000,000 au zaidi ndani ya muda mfupi. Faida ya watalii si kuona mbuga za wanyama na historia yetu tu, bali pia kuwavutia na kuiona Tanzania kama kituo salama cha uwekezaji. Katika hili nasema fursa zipo mbele yetu, viongozi wetu wazishike sasa.

 

Sitanii, baada ya pongezi hizo, sasa nije kwenye lawama zenye tija. Napenda kumlaumu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, kutokana na kosa aliloitendea tasnia ya habari na kulisababishia aibu taifa letu mbele ya mgeni wetu Rais Barack Obama. Salva ama ameshauriwa na Usalama wa Taifa au viongozi wa Ikulu, lakini kwa kukubali ushauri huo amepotoka.

 

Pale Ikulu Julai 1, ulikuwa Mkutano wa Waandishi wa Habari na Rais Obama na Kikwete. Ule haukuwa mkutano wa maafisa uhusiano au mawaziri au wanadiplomasia. Kwanza nilipata mshangao niliposikia taarifa kuwa watu wa kuuliza maswali tayari walikuwa wamepangwa.

 

Nilijiuliza maswali haya ni yapi? Nilijaribu kuwasiliana na Salva, akasema nisiwe na wasiwasi. Swali la kwanza lililoulizwa na Mwandishi kutoka Tanzania ndilo lililonisikitisha kuliko yote. Naamini swali hili mwandishi alipewa na Salva, kama anabishi aseme.

 

Mwandishi aliuliza hivi: “Rais Obama unaridhika na kiwango cha misaada inayotolewa na Marekani kupitia MCC?” Swali hili lilimshangaza hata Rais Kikwete. Nilimwangalia Obama usoni nikaona lilimkera. Kikwete naye aligundua hilo, ndiyo maana akasema: “Swali hili nilipaswa kuulizwa mimi.”

 

Sisi Watanzania ndiyo tuliopaswa kueleza mafaniko ya MCC. Tulistahili kuwa wa kwanza kumweleza Obama kupungua kwa wagonjwa wa malaria katika hospitali kama Amana, kwa vile  vitanda havina wagonjwa. Tungemweleza habari njema ya Zanzibar kufuta malaria wanaoletwa na mbu katika uso wa dunia. Tungemweleza barabara za Horohoro, Namtumbo na kwingineko. Hii ilikuwa aibu kwetu.

 

Swali la pili lililonikera, eti akapewa nafasi mwandishi kutoka DRC amuulize Rais Obama. Yeye akageuka balozi wa amani. Akatumia nafasi hiyo kuomba msaada wa Obama kuingilia kati mgogoro unaoendelea DRC kuwa wamepigana miaka 20 na watu wanateketea.

 

Sitanii, unaweza kuwahurumia Wakongo kwa vita hiyo, lakini kama ni kuomba msaada wa aina hiyo wanaye Balozi wao nchini Marekani aliyepaswa kufanya kazi hiyo. Hapa pia ndipo nilipokereka nikaamua kusimama na kuomba kuuliza swali la nyongeza.

 

Niliomba radhi na kumuomba Rais Obama atoe kauli juu ya Uganda na Rwanda zinazopeleka majeshi yake DRC, lakini kwa bahati mbaya Obama hakujibu swali langu zaidi ya kuniambia: “It’s turn for the Americans (ni zamu [ya swali] kwa [waandishi] wa Marekani.” Akaendelea hadi mkutano ukaisha.

 

Waandishi waliokuja na Rais Obama wakauliza maswali ya maana. Mmoja kutoka BBC akahoji inakuwaje Marekani inaendelea kutoa fedha za misaada kwa Misri ilhali ikijua kuwa Rais Mohamed Morsi anavunja haki za binadamu. Obama akasema anaguswa na hali hiyo na anafuatilia kwa karibu. Rais Morsi tayari ameshaondolewa madarakani.

 

Sitanii, wakati sisi tunajipendekeza kwa maswali ya kuchaguana, mwandishi kutoka Marekani akamuuliza Rais Kikwete kwa nini Tanzania inateua mabalozi wanaokwenda Marekani kufanya biashara ya kuuza watu (human trafficking). Nadhani sisi waandishi wa Tanzania tungeuliza swali kama hili, Salva angewaelekeza Usalama wa Taifa au Polisi watufuatilia popote tulipo na kututia adabu!

 

Suala hili ni la ajabu. Balozi anayetajwa kuwa anauza binadamu, Alan Mzengi, kwa kila hali ameonewa. Alimpeleka Marekani ndogo wa mke wake. Akawa anamlipia karo na anamsomesha vyuo. Binti huyu akapewa mafundisho na baadhi ya wanasheria wa Marekani, kuwa adai fidia ya kutumikishwa bila mshahara.

 

Wakamwambia wakati anaishi nyumbani kwa Balozi Mzengi, alikuwa anafanya kazi za ndani na hivyo alipaswa kulipwa mshahara kwa muda wote wa miaka minne aliyokaa nyumbani kwake. Mahakama ikatoa hukumu ya dola milioni 1, sawa na Sh bilioni 1.64.

 

Ilipofika hapo, Serikali ya Tanzania ikaingilia kati binti akalipwa na Serikali dola 170,000 sawa na Sh milioni 278. Balozi Mzengi akaondolewa kazini akaponzwa na huruma ya kumsaidia ndugu wa mke wake. Sina uhakika kama mkewe ndoa bado inaendelea. Kikwete alilifafanua vyema.

 

Katika hili mimi nilitaka kumuuliza Obama, si tu anawakemeaje Paul Kagame anayemtukana Rais wetu kwa kumshauri azungumze na waasi, bali pia kuna Watanzania 207 waliokuwa wameajiriwa na Ubalozi wa Marekani chini ya kampuni ya Ulinzi, ambayo imewanyima mishahara na maslahi mengine, lakini hadi leo wanahangaishwa na Ubalozi ukisema hauwatambui.

 

Sitanii, je, hilo lisingekuwa swali sahihi kwa Rais Obama kwa maoni ya Salva? Nadhani nihitimishe kwa kusema jambo moja hapa. Si kweli kwamba Salva kuwa pale Ikulu ndiye wa kwanza au wa mwisho. Analopaswa kukumbuka, naye alianzia chumba cha habari kama mwandishi wa kawaida, akapanda cheo hadi mhariri kisha akaenda Ikulu.

 

Pale aliwakuta akina Chokala, Nkurlu, Maura na wengine. Ni wazi basi kama utaratibu ndiyo huo, anapaswa kufahamu kuwa kama walivyoondoka akina Kallaghe, hata yeye ipo siku ataondoka pale. Wadau wake namba moja katika sekta ya mawasiliano ya umma ni waandishi wa habari.

 

Kama alijua anayo maswali yake kwenye koti, basi alipaswa kushauriana na waandishi wakayaboresha yakawa maswali badala ya vichekesho. Aibu aliyotutia swali la kwanza, si tu kama waandishi wa habari, bali Watanzania sote ni kubwa.

 

Katika diplomasia ya kimataifa, swali linaloulizwa na waandishi ndilo linalochukuliwa kuwa msimamo wa nchi. Tafsiri ya swali la kwanza kwa Rais Obama ni kwamba msaada unaotolewa chini ya MCC si chochote wala si lolote. Swali hili linaweza kuwa chimbuko la kuzorota kwa uhusiano wa Marekani na Tanzania.

 

Sina chuki na Salva, ila nasema kwa uwazi kuwa utaratibu alioutumia umeharibu heshima ya taifa na siku nyingine ikitokea tuna ugeni mkubwa kiasi hiki, awe wazi. Waandishi akutane nao, wakubaliane aina ya maswali, wayaboreshe kama yana upungufu, kisha tuulize maswali yenye maana badala ya vichekesho.

 

 

By Jamhuri