NA ANGELA KIWIA

Serikali imetoa maagizo kwa mashirika yasiyo
ya kiserikali (NGOs) na kuyataka kuyatekeleza
ndani ya mwezi mmoja.
Napenda kuipongeza serikali kwa hatua hii
muhimu. Natambua wapo baadhi ya ndugu zetu
hawatafurahia hatua hii ya serikali kuzibana
NGOs, kwa kuwa walikuwa wanufaika
wakubwa wa mashirika hayo kwa kuyatumia
isivyo.
Baadhi ya mashirika hayo yamekuwa
yakijihusisha na uhamasishaji wa vitendo vilivyo
kinyume cha tamaduni zetu, huku yakipokea
fedha kwa ajili ya uhamasishaji wa mambo ya
ovyo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushoga
nchini.

Serikali sasa imeamka kutoka usingizini na
‘kuyashukia’ mashirika hayo yaliyokuwa
yakisababisha mmomonyoko wa maadili
uliokuwa ukihamasishwa na baadhi ya yale
yanayopata ufadhili kutoka nje ya nchi.
Miongoni mwa maagizo hayo ya serikali ni
kuyataka mashirika hayo kutuma taarifa zao za
kifedha na miradi za kila mwaka kwenye Ofisi
ya Msajili wa NGOs. Hii itasaidia kufahamu
vema kazi za NGOs husika na malengo yake,
kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Nchi yetu iligeuzwa kuwa shamba la bibi na
jalala. Tumekubali kutumiwa kutokana na njaa
zetu huku kizazi chetu kikiishia kupokea kila
aina ya tamaduni kutoka nje.
Tunashuhudia mmomonyoko wa maadili
kutokana na tamaa ya fedha kutoka kwa baadhi
ya wafadhili kupitia baadhi ya NGOs.
Ubinadamu umetutoka kwa tamaa ya kuishi
maisha mazuri huku kizazi chetu kikiangamia.
Ikumbukwe nchi yetu ni miongoni mwa nchi
zinazozingatia misingi ya utawala bora katika
utekelezaji wa majukumu yake, hivyo
uzingatiwaji wa masuala ya uwazi na uwajibikaji
ni jambo la msingi kwa mashirika haya.

Baadhi ya NGOs zimekuwa zikilalamikiwa kwa
kujihusisha na mambo yaliyo kinyume cha
malengo ya uanzishwaji wake. Hata hivyo zipo
ambazo zimekuwa kichocheo cha maendeleo
katika nchi yetu.
Wapo baadhi ya wageni wamekuwa wakipitia
kwenye NGOs na kusababisha kutoelewana
katika jamii zetu, kwa kuwatumia baadhi ya
Watanzania wenzetu kutokana na njaa yao
isiyokwisha.
Naipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuliona
hilo na kuamua kuchukua hatua. Ninaamini
kuwa zoezi hili litakuwa endelevu na lenye tija
kwa taifa.
Vilevile ni imani yangu kwamba huu utakuwa
mwanzo mzuri kwa jamii yetu kuyatumia
mashirika hayo kutimiza malengo husika na
kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja bila
kutumiwa na wasioitakia mema nchi yetu.
Huu utakuwa mwisho wa baadhi ya watu
ambao waliamua kuyapaka matope mashirika
hayo yasiyo ya kiserikali na kuonekana yote
hayafai, jambo ambalo si kweli.
Natambua yapo yaliyokuwa yakiumizwa na hali

hii kutokana na serikali kutochukua hatua. Sasa
nchi yetu itakuwa na NGOs zinazotekeleza na
kutimiza lengo la uanzishwaji wake, huku
zikifurahia uwepo wake.
Vilevile ni wakati muafaka sasa kwa serikali
kuwa karibu na mashirika haya ili kutambua
uwepo wake na kuyaunga mkono, hasa pale
yanapohitaji msaada wake katika kusukuma
mbele gurudumu la maendeleo.
Serikali na mashirika hayo wote kwa pamoja
wanategemeana, hivyo ni wakati sasa wa
kufanya kazi pamoja na kumsaidia Mtanzania
mmoja mmoja anayehitaji kufikia lengo.
Tanzania inajengwa na Mtanzania
mwenyewe.

Mwisho

By Jamhuri