Wiki iliyopita tumeshuhudia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya, ikitangaza matokeo ya uchaguzi mkuu. Matokeo hayo yamempa ushindi Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee. Mshindani wake wa karibu, Raila Odinga amekataa kutambua matokeo haya.

Wagombea wakuu – Odinga na Kenyatta – wameonesha ukomavu wa hali ya juu kisiasa. Muda wote wakati matokeo yakisubiriwa na baada ya kutangazwa wanahubiri utulivu na amani. Wanawazuia wafuasi kuingia barabarani. Pia wamehimiza kushangilia ushindi kwa staha.


Jambo jingine, baada ya Odinga kutangaza kutotambua matokeo, amechukua mkondo wa kwenda mahakamani. Tanzania tunaandaa mabadiliko ya Katiba. Kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiishatangaza matokeo kwetu hakuna chombo chochote cha kupinga matokeo haya.


Sisi tunasema huu ni upungufu mkubwa katika Katiba yetu. Kenya wamelibaini hilo na sasa Odinga anaitumia haki hii. Yapo majimbo zilipohesabiwa kura mara mbili na yapo majimbo Odinga anasema waliojiandikisha na idadi ya kura zilizopigwa ni tofauti.

 

Odinga anasema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wakati wa kujumlisha matokeo, iliwafukuza wasimamizi wa vyama vya siasa kushuhudia mwenendo. Upungufu huu ukiachwa unaweza kuwa wa hatari. Mahakama inawapa fursa ya kupitia mwenendo wote wa uchaguzi.


Tanzania tunabadili Katiba tukiamini hii ni fursa kwetu kujiandaa. Habari ya kura kupotea njiani, kuongezeka kwenye vituo na wakati mwingine kuwapo vituo hewa vya kupiga kura, limekuwa suala sugu kwa Afrika.

 

Katiba yetu tunayoitarajia mwakani inapaswa kutoa fursa hii. Tuwape wanasiasa na Watanzania fursa ya kueleza malalamiko yao. Tuvunje usiri unaokuwa ngao kwa aliyetangazwa mshindi hata kama ameiba kura. Ni kwa namna hii nchi yetu itaheshimika kwa demokrasia safi.


Mwisho, tunasema Watanzania tuitunze amani yetu. Kenya waliichezea mwaka 2007/08 imewachukua miaka mitano kurejea hapa walipo. Ikiwa yapo yanayotutofautisha, ni vyema tukayatatua kwa njia ya amani. Utaratibu mpya wa kuhamasishana kutumia nguvu, utatuumiza mwaka 2015.


By Jamhuri