1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliMheshimiwa Jaji Mkuu, nafikiri utaungana na mimi mara baada ya hotuba hizi ambazo zilitangulia inawezekana ikaniwia vigumu sana kutafuta maneno mengine ya kuweza kuzungumza. Lakini niseme tu kwa dhati Mheshimiwa Jaji Mkuu, nimefurahi sana kunikaribisha, ili nije nishiriki na ninyi kwa mara ya kwanza katika siku hii muhimu. Lakini nimshukuru pia Mwenyezi Mungu ambaye alituwezesha kumaliza uchaguzi salama, na niwashukuru ninyi hasa vyombo vya Mahakama na vya kutoa haki, kwa sababu iliwagusa mioyoni mwenu na kutoa haki mimi kuwa rais wenu wa awamu ya tano (makofi).

Kwa hiyo natoa shukrani sana, Lakini pia Mheshimiwa Jaji Mkuu na Mahakama kwa ujumla napenda niwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya. Ukweli kwa ujumla wenu na kwa asilimia kubwa mnafanyakazi kubwa sana ambayo wala haina complication. Tulipokuwa tumekaa pale nilikuwa nakuuliza siku hii na yenyewe inaonyeshwa live, ukasema hapana; nikasema kwanini ninyi hamtaki kuonyeshwa onyeshwa live, ukasema mnataka mzitumie hizo hela za kuonyeshwa live kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania. Hongereni sana.

Kwa sababu hapo nazungumza bilioni tatu kwa ajili ya kushughulikia kesi za uchaguzi, lakini katika vipindi ambavyo tunaonyesha katika kipindi kimoja kwa wiki mbili au zaidi ukionyesha live coverage unatumia bilioni nne, kwa hiyo kwa busara ya kawaida tu ni vizuri uzikate kule milioni nne za kuonyesha live uzipeleke kule zikatoe hukumu kwa kesi za uchaguzi za waheshimiwa wabunge kwa sababu kupanga ni kuchagua.

Na inawezekana mngependa pia hata mnapotoa hukumu zenu kule muwe watu wanaona live, lakini kwa mtu ambaye anajua anazingatia maadili yake, na hasa anatumikia nchi masikini ambayo ina shida nyingi, unakuta wananchi wa Morogoro leo hawawezi wakasafiri kutoka Kilombero kwenda Ifakara kwa sababu hakuna communication. Na ni kwa sababu tu zimekosa shilingi milioni mia tisa za kumlipa kandarasi ambaye anatakiwa kujenga pale.

Umeelezea hapa shida ambapo mnazipata Mahakama kwamba kwenye mwaka 2013 zilitengwa zaidi ya bilioni 26 baadaye zikapandishwa zikafika mpaka bilioni 41 kwenye bajeti  iliyopita, baadaye zikashuka chini kwa asilimia 70 zikawa bilioni 12.3 nazo hamjapata hata senti tano leo.

Kwa kiongozi uliyepewa kuongoza nchi yenye changamoto za namna hiyo ni lazima ukae na kufikiria ni wapi pa kupeleka, ni wapi pa kunyima. Na ndiyo maana nasema kwa dhati kabisa Mheshimiwa Jaji Mkuu na Mahakama mnafanyakazi ya Mungu. Mnafanya kazi kwa ajili ya Watanzania, imagine mtu awe amekaa mahakamani kwa miaka kumi maamuzi hayajatolewa ni kwa sababu tu pamekosekana haki yake na baadaye baada ya hukumu aonekane ameshinda hata kwa malaika tunaweza tusisamehewe; kwa hiyo ndiyo maana nimeanza na kuwapongeza kwa kazi ngumu mnazozifanya katika mazingira magumu, lakini kwa faida ya Watanzania.

Mimi siyo mwanasheria, lakini ninazipenda sheria. Kwa sababu nafikiri hata Mungu anapenda sheria ndiyo maana aliweka amri kumi. Akampa Musa ili sheria zikatekelezwe ingawaje watu hawataki kutekeleza sheria, lakini sheria ni sheria. Na sheria ndiyo mahali pekee pa kuweza kutoa haki, na ndiyo maana Mheshimiwa Jaji Mkuu, nimeanza kwa kuwashukuru sana kwa kazi ngumu mnayoifanya, lakini siku zote mmekuwa mkimtanguliza Mungu ili haki za Watanzania- watu wa Mungu waweze wakazipata mapema na kwa haraka.

Na ndiyo maana katika takwimu zako umeeleza ni kwa namna gani mmehangaika katika kutoa haki kwa kutoa maamuzi ya haraka na ukatoa hata masharti kwamba katika Mahakama za Mwanzo angalau kwa kila mmoja minimum awe ametoa maamuzi 260, wako waliojitokeza wametoa mpaka 900. Lakini nataka nikueleze Mheshimiwa Jaji Mkuu, kama ni majipu hawa ambao hawakufikia 260 ndiyo majipu yako uliyonayo unatakiwa uyashughulikie.

Kwa sababu ninafahamu ninyi pia siyo malaika, kuna binadamu na katika binadamu pia wanaweza wakajitokeza wengine ambao watakuwa wanaharibu kazi nzuri ya Mahakama mnayotaka kuifanya. Haiingii akilini wewe Jaji Mkuu ambaye hata mimi uliniapisha unatoa maagizo kwamba angalau kesi 260 halafu mtu huyo huyo anapinga agizo lako…na bado unamwangalia tu halafu leo hii unasema umempa siku saba, sasa sina uhakika kama hizo siku saba atazihukumu hizo kesi 260 ninachotaka kukuomba wale waliohukumu kesi 900 hata mimi nawapongeza sana, lakini wale wanaoharibu sifa nzuri ya Mahakama, Mheshimiwa Jaji Mkuu uanze pia kuchukua hatua.

Tusipochukuliana hatua hakuna kitakachofanyika. Hata mimi ninapochukua hatua zingine humu serikalini msifikiri mimi ni mnyama sana, mimi ni mpole kweli, lakini nafikia mahali pengine ni lazima ufanye.bInafika mahali lazima ufumbe macho useme lazima nifanye kwa sababu yanayofanyika ndani ya Serikali ni ya ajabu sana. Niwatolee mfano tu, na ni lazima niseme tu kwa sababu ni lazima ni seme haya tu, ninyi wote hapo inawezekana mnajidai mna vitambulisho vya taifa, lakini hebu mcheki vitambulisho vyenu vya taifa kama vina sahihi zenu.

Kama atasimama hapa hata mmoja mwenye kitambulisho cha taifa chenye saini yake anyooshe mkono, hakuna! Lakini vitambulisho vilivyotolewa na Mheshimiwa Jaji Lubuva vina sahihi zetu. Yeye kwa fedha ambazo ni chini ya bilioni 70 ametengeneza vitambulisho milion 22.7. Huyu kwa fedha bilioni 179.6 ametengeneza vitambulisho havikufika hata million 2.

Kwa hiyo unapoamua kuchukua maamuzi kwa sababu kuna watu walifikia nchi hii ya ajabu sana. Siku naingia madarakani ilikuwa ni shida kulipa mishahara ya watumishi. Lakini kule makontena TPA yanapita bila kulipiwa ushuru na inawezekana hata tukiwaleta mahakamani mtawaachia ninyi waheshimiwa majaji. Na ndiyo maana unaweza ukasimama mahali ukaona namna gani ugumu wa kuongoza nchi ambayo imeingiliwa na wadudu wa kila aina.

Na ndiyo maana siku zote nakuwa nasema ndugu zangu mniombee, na wewe Mheshimiwa Jaji Mkuu pamoja na kwamba una nguvu za kuhukumu na mimi pia uniombee kabla ya kuhukumu. Kwa sababu tuna changamoto kubwa katika nchi yetu ya kuweka maadili yaliyo mema, wako watu wanacheza na pesa kama wanavyotaka na wako watu ambao ni masikini sana katika nchi hii. Wako watu ambapo wakati wa bodi wanapoamua kukaa wanaona hakuna hoteli yoyote hapa Tanzania ya kuweza kukaa. Wakati wa bodi wanakwenda Ulaya kwa ajili ya bodi zao wanazokaa.

Wakati Wilaya ya Loliondo uliyozungumza haina hata Mahakama, wakati hakimu hakuna hata pikipiki, wakati kuna watu hata kupata mlo wa kwanza ni shida. Ndiyo nchi hii tulipofikia. Na ndiyo maana ninaomba Mahakama, watoa haki mahali popote, kwa sababu mwenye uwezo wa kuhukumu humu duniani ni majaji na mahakimu ukiacha ile hukumu inayotolewa na Mungu. Kwa hiyo ninyi mnamwakilisha Mungu katika dunia na katika nchi yoyote.

Toeni hukumu kwa haki, lakini kwa hao ambao wanaweza kuifikisha nchi mahali pabaya toeni hukumu haraka. Na watu wenye hela wana mbinu nyingi ukimwambia kudhaminiwa hata kwa bilioni tano watajitokeza wengi kumdhamini kwa bilioni tano kwa sababu ameiba bilioni maelfu aliyonayo.

Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Majaji, Waheshimiwa Mahakimu, muitangulize Tanzania kwanza. Mkiitanguliza Tanzania kwanza, na hasa tunapoanza mwaka huu mpya wa Mahakama tutaweza kufika mbali, na tutaweza kuwasaidia Watanzania wengi. Leo hapa Mheshimiwa Jaji Mkuu kutoa tu mfano kuna kesi 442 za watu waliokwepa kulipa kodi serikalini. Zile kesi kama zingeamuriwa gharama yake ni trillioni moja. Kesi hizi zimekaa tangu mwaka 2010 mpaka leo 2015 na hili limejenga mazingira TRA wanapokwenda kumtafuta mfanyabiashara kusudi alipe kodi anakimbilia mahakamani, na mahakamani haziamuriwi.

Kwa hiyo Serikali sasa hivi tumekosa trilioni moja, bajeti yako ungehesabu zile bilioni 40 zinaingia ngapi kwa trilioni moja. Lakini trilioni moja hata kama ungeamua Tanzania tuwe na shirika la ndege letu linalojitegemea, ukienda leo mka goggle thamani ya airbus moja mpya lenye kubeba watu kati ya 120 na zaidi ni dola milioni 90.6; kwa hiyo ukizidisha kwa exchange rate ya sasa hivi manake ni bilioni  140.  Kwa hiyo trilioni moja unaweza ukajua tungekuwa na airbus ngapi mpya tumezishusha hapa.

Maana yake tungekuwa na ndege zaidi ya sita mpya na hizi ndege tungeamua sasa badala ya kuwa msafiri anayekuja kutalii Tanzania lazima ateremkie Kenya kwa Mheshimiwa Jaji Mutunga, kule angetelemkia moja kwa moja Kilimanjaro na tukapata utalii. Kwa sababu akishaanza kutelemkia uwanja wa Jomo Kenyatta ataanza kuwaona wanyama wapo wapo pale, hahitaji kuja huku kwa ndugu zangu huku, anarudia pale pale. Na wangekuja moja kwa moja manake uchumi wetu ungepanda.

Na ndiyo maana Mheshimiwa Jaji Mkuu ninazungumza kwa dhati kabisa na kwa uchungu mkubwa. Mahakama pia mtusaidie. Ninatoa mfano, kwa hapa tu Kisutu ambapo ni Dar es Salaam kuna kesi 26 ambazo wahusika walishikwa wakiwa na nyara za Serikali, wengine meno ya tembo, wengine kadhalika, redhanded kesi zile zimechukua zaidi ya miaka mitano hazijapata maamuzi, na katika maelezo yanayotolewa ni kwamba upelelezi bado unaendelea. Wapelelezi polisi wapo, DPP yupo, na wameshikwa watu redhanded lakini upelelezi bado unaendelea…upelelezi unaendelea…upelelezi unaendelea, kwa hiyo unaona dhahiri kwamba inawezekana yule jaji alitaka kutoa hukumu, lakini DPP na polisi wanaohusika kila siku wanasema upelelezi unaendelea atatoa judgement gani?

Kwa hiyo unaweza ukaona tatizo napo lipo mahali gani. DPP uko hapa, upelelezi uishe, ukimshika mtu redhanded mpeleke mtu siku hiyo hiyo akafungwe. Unahitaji upelelezi gani umemshika na meno ya tembo anayo mkononi, umemshika redhanded bado unazungumza kupeleleza, unapeleleza nini au unatafuta rushwa?

Ninayazungumza haya ili vyombo vyote vinavyohusika katika kutoa haki vitimize wajibu wao. Vikifanya hivyo vitaisaidia hii nchi, hata malalamiko haya Mheshimiwa Jaji Mkuu unayoyatoa ya kukosa development fund. Mimi nikuombe basi leo katoe huku ya hizo kesi 422. Robo ya fedha hizo nitazileta mahakamani. Kafanye oparesheni hiyo trilioni mojauifanyie maamuzi watu walipe hizo fedha, ninakuahidi na ninasema kwa dhati jua linawaka katika trilioni moja hiyo, bilioni 250 nitazileta mahakamani ili kusudi tubaki na bilioni 750 tukanunue ndege za Serikali kwa ajili ya kuwa na Air Tanzania yenye uhakika, lakini wale wafanyakazi wa Air Tanzania wale wote 200 tuwaondoe- waondoke moja kwa moja.

Ninazungumza hivi waheshimiwa kwa sababu ninataka mabadiliko. Haiwezekani nchi kama Tanzania ina kila kitu. Haiwezekani ikawa nchi masikini, we are suppose to be donor country, tumebaki kuomba misaada wakati kila kitu tunacho, Tanzanite ipo Tanzania tu, lakini wauzaji wakubwa wa Tanzanite duniani ni India wakifuatiwa na Kenya. Tuna ugonjwa gani, shetani gani huyu ambaye tukaombe angalau aondoke kwa Watanzania? Kama ni kushindwa, basi ashindwe akalegee moja kwa moja ili Watanzania tuweze kufaidi na nchi yetu tuliyopewa na Mungu. Mheshimiwa Jaji Mkuu inawezekana naingia kwenye direction ambayo hukuitaka sana, lakini nataka niseme tu, kwenye Mahakama za ardhi kuna kesi zaidi ya 556 ambapo Msajili ameshindwa tu kuandika barua kwamba haya mafaili nayaleta kwenye Mahakama Kuu na kesi hizo zingine zimechukua miaka 10. Waziri wa Ardhi yupo, Katibu Mkuu wa Ardhi yupo, Kamishna wa Ardhi yupo, Msajili wa Ardhi yupo, hiyo ndiyo Tanzania.

Kwa hiyo ninyi Mahakama Kuu mnashindwa kutoa hukumu huku kwa sabababu mafaili hayajaletwa na Msajili wa Wizara ya Ardhi. Kuleta tu yale mafaili ili yachukuliwe na haki itendeke… hii ndiyo Tanzania. Hii ndiyo Tanzania. Juzi nilikuwa nazungumaza, tuna mabenki zaidi ya 54 hapa katika nchi hii, ma-chief excutive wa wizara mbalimbali wanakaa na fedha katika fedha ambazo wanazikusanya zingine ni za serikali. Zile fedha wanaziweka kwenye akaunti za benki za kibiashara. Ukichukua fedha zote zile zilizowekwa ni zaidi ya trilioni 1.6.  Yale mabenki yanachofanya ni kuchukua fedha hizo za Serikali zilizowekwa kule, wanaenda kukopa treasury bills kwenye BoT kwa hiyo Serikali inafanya biashara na fedha zake. Tanesco wana bilioni 169, TANAPA wana bilioni sijui ngapi, TCRA and so on, and so on. Na fedha zilizowekwa kule kwenye mabenki, kuna fedha zilizowekwa wala haziingizi interest, kwa hiyo wanakaa watu wanagawana kwa kuzungumza kwao, na ndiyo maana kuna watu wanajilipa mishahara mikubwa mahakimu huku wanahangaika hawana hata pikipiki. Wapo watu wanaolipwa mishahara mpaka milioni 35 kwa mwezi to the same country, the same country, the same people. Kwa hiyo kinachofanyika haya mabenki wala hayajali kukopesha watu wa kawaida ili business iende kama kawaida kwa sababu they do big business in the BoT kwa kutumia treasuary bills. Kwa hiyo ikihitaji hela kuuza kwenye mabenki haya, au mabenki haya yakihitaji kununua fedha BoT yanatumia hizi hizi hela zilizowekwa na ma-chief executive kama ni za TANAPA hizo hizo zinatolewa zinakwenda kununua huko wanapata interest, Serikali ina- move from their its own money.

Nilisema hizi hela zote zinafunguliwa akaunti moja kwenye BoT, full stop. Na hata mawaziri, Mheshimiwa Mwakyembe anafahamu, zipo wizara zilizokuwa na fedha nyingi za ration, nikamsikia waziri mmoja analalamika na mwingine hivi …nikamwambia alete barua yangu ya ku-resign, aondoke. Hela hizi tunazishika, na akileta barua ya ku-resign manake amekubali hela hizo ziwe monitored na BoT ili kusudi hela yetu tuielewe, itumike kulingana na maslahi ya Watanzania. Kuna shirika moja sitaki kulitaja hapa lina bilioni 338, limegawanya kwenye mabenki benki mbalimbali. Sasa kwa utaratibu  huu na kwa sababu they have money wanaweza kufanya lolote na kuiyumbisha Serikali, na ndiyo maana nilipokuwa nikifungua Bunge nilisema tafadhali sana my dream ni kuwa na Mahakama ya hawa watu. Sasa sina uhakika kwa vile hawa ni mamilionea sana kama hawa wata wa-corrupt  kule watakaokuwa wanahukumu.

Lakini angalau nina imani na wewe Mheshimiwa Jaji Mkuu, harakisheni kuunda hii Mahakama, wala hatuhitaji kwenda mpaka kwenye Bunge na kufanya mabadiliko. Kama tuna Mahakama ya Kitengo cha Ardhi, kama tuna Mahakama ya Kitengo cha Biashara, kwanini tusiwe na Mahakama ya Kitengo cha Mafisadi?

Twende haraka huu muda tunaochelewa  wanaichezea hii nchi. Mmenichagua kuwa Rais wenu, niliahidi nitasema ukweli, na huo ndio ukweli ninaousema kwenu. Huu mkate mdogo unaopatikana kwa ajili ya Watanzania ni vyema uwanufaishe wote, bila kujali dini zetu, makabila yetu, vyama vyetu, wote wafaidi na hii raslimali ya Watanzania tunayoipata.

Kwa hiyo ninapojaribu kuchukua hatua ndugu zangu Mheshimiwa Jaji Mkuu na Waheshimiwa Majaji, mimi siyo kichaa, mimi siyo dikteta, lakini angalau nataka nifanye sadaka yangu kwa kipindi nitakachokuwa naishi hapa duniani. Inawezekana hata baada ya kufa naweza kuwa hata rais kule wa malaika kidogo kidogo nasumbua. Kwamba ulitimiza wajibu wako.

Mheshimiwa Jaji Mkuu, najua mengi ambayo nilitaka niyazungumze leo, lakini nataka nikuhakikishie kuwa yale maombi yote uliyoyatoa hapa nitayazingatia. Umezungumza mengi ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wako, umezungumza kutaka kupata fedha za development za kutosha  ili ufanye kazi na kwa sababu wewe umejipanga kwa ajili ya ‘Hapa Kazi Tu’ ni lazima niku-support.

Lakini na wewe Mheshimiwa Jaji Mkuu naomba unisaidie kitu kimoja; katika Mahakama mna kitu kimoja ambapo huwa mnatumia fedha kwa ajili ya kuwasomesha wafanyakazi wenu. Ni kitu kizuri, lakini inawezekana pia mnajipa mzigo ambao siyo wenu, kwa sababu kwa sasa hivi mnasomesha karibu wafanyakazi 540. Ukisomesha wanafunzi 540 na wengine uwapeleke chuo kikuu wakati kuna bodi ya mikopo ambayo ninaipelekea hela mimi kwa ajili ya kusomesha Watanzania, ni matumizi mabaya ya pesa.

Wale wenye qualification wanaotakiwa kwenda kusoma leta orodha yao wakasomeshwe kwa mkopo wa bodi ya shule ili hizi fedha unazozitumia wewe kidogo kwa ajili ya kuwasomesha hawa ukazitumie kununua magari kwa hao mahakimu wanaopata shida. Ukatumie kubadilisha system badala ya kutumia mafaili halafu mtu mmoja karani akitaka kupoteza faili anabadilisha tu direction analitoa hapa analiweka hapa chumba ni hicho hicho mtalitafuta mwaka mzima hamtaliona. Sasa hizo fedha ambazo ninyi mnazitumia kwa ajili ya kusomesha na inawezekana wengine ambao si watu wema anaamua kumsomesha mtu mwingine anaweza kumsomesha kuanzia darasa la saba, akampeleka mpaka form four, akamaliza akampeleka mpaka chuo kikuu wakati nje ya Mahakama kuna watu waliomaliza chuo kikuu wenye degree za law na masters wanazunguka wakitafuta kazi wamekosa, wapo na ungetangaza leo.

Wewe niruhusu Mheshimiwa Jaji Mkuu niseme tu hata leo wnaotaka ajira wenye degree, first degree, second degree ya law utaona ofisini pale watajaa. Kwa hiyo hata wale walioshindwa kuhukumu, kufikia lengo uliloliweka wewe, mtoa haki, ulisema 260 na wao wengine wakakomea less than 100 unawabakiza wa nini?

Huruma hii ndiyo inaipaka matope Mahakama. Nimeenda Arusha watu wanalalamika… nina nanihii yangu ya mirathi, watu wanateseka na hasa kwenye Mahakama za Mwanzo. Mahakama za Mwanzo ni kilio, lakini inawezekana tumeweka watu ambao hawana qualification tunawabeba-beba tu. Wakati kwenye field wako wengi waliosoma hatutaki kuwaajiri na vijana wanalalamika hawana employment  wewe  umekaa na watu kule ambao unawabeba-beba tu. Na hata kuhukumu hawawezi kuhukumu kwa sababu they don’t have qualification, up stairs they are not fine, nitaburarasa. Sitaki kuingilia Mahakama kwa sababu mtaanza kusema ameingilia Mahakama, mimi ninasema yanayonigusa kwenye moyo wangu, na msemakweli ni mpenzi wa Mungu.

Ni lazima tufike mahali tuamue kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu, nchi yetu ni muhimu kuliko kitu chochote, na ndiyo maana inafikia kila siku tunaahidiwa vi-ahadi vya ajabu ajabu na vyenye masharti ya ajabu ajabu. Nimeamua nchi iende, na itaenda, anayefikiri ataikwamisha atakwama yeye kwa sababu Mungu yuko pamoja na mimi. Na watu ninaowategemea sana ni Mahakama, Mahakama unafunga kila mmoja, hata rais nikitaka kufungwa na Mahakama nafungwa. Mbunge anafungwa, nani anafungwa, ninyi ndiyo wenyewe, na ndiyo maana nguo zenu labda nyekundu maana yake damu damu hivi. Na mimi leo nimejaribu kuigaiga hivi nikavaa angalau tai nyekundu.

Lakini Mahakama zetu tukisimama imara kwa ajili ya maslahi ya nchi yetu tutakwenda. Na mimi nakuhakikishia Mheshimiwa Jaji Mkuu kweli nasema fedha za development nitawapa na Mheshimiwa Mwakyembe uko hapa leo. Katika bajeti ya mwaka huu lazima tuweke fedha nyingi kwa ajili ya Mahakama, halafu washindwe wao mwaka kesho nitasema hapa hapa niliwapa hela kiasi hiki, tena nitawapa kuliko bajeti zote ambazo mmepewa. Kwa sababu makusanyo yapo, wakwepa kodi lazima walipe. Hata kwenye maandiko yanasema ya Kaisari mpe Kaisari ya Mungu mpe Mungu.

Hata Marekani wanalipa kodi. Leo nilikuwa naangalia kwenye taarifa ya habari mchezaji mmoja sijui wa wapi   amekwepa kodi amehukumiwa kufungwa. Sisi wakwepa kodi hawafungwi. Akitoka anatoka kule halafu anaanza kutamba na fedha zake. Ifike mahali Mahakama mtusaidie muwafunge wakwepa kodi. Ni lazima tubadilike, lakini pia kama mtu amekwepa kodi mmoja halafu wengine wanalipa kodi na wanauza bidhaa hiyo hiyo its not fair kwa sababu hata competition ya wafanyabiashara inakuwa unfair. Yeye ameleta kwa kukwepa kodi, halafu mwingine amelipa kodi, aliyekwepa kodi bidhaa zake atazishusha chini, akishashuka chini huyu mwingine hatafanya fair competition.

Kama hataki kufanya biashara aache, wafanye wanaotaka kufanya biashara, lakini na Serikali ikusanye kodi yake. Kwa hiyo mimi nawategemea sana Mheshimiwa Jaji Mkuu na Mahakama, kweli nawategemea. Maslahi yenu mimi wala sina tatizo, sijui magari, sijui mshahara kupandisha sijui nini is not an issue kwa sababu si ninyi ndiyo mtatusaidia kuzipata? Kwa mfano hiyo trilioni moja nikiipata baada ya siku tano ikapatikana una bilioni 250 mimi nakupa, hukumu tu haraka haraka walipe, document zipo mtu anakwepa kwepa. Kwa hiyo saa zingine tunajiumiza sisi wenyewe. Panakuwepo na mtu mmoja kesi kila siku inapigwa tarehe, mara hakimu anaumwa, leo hajisikii, leo ana family problem, DPP naye ‘bado tunaendelea kupeleleza’, polisi naye hivyo hivyo; tunabaki kuwasumbua tu watu wa magereza kila siku kuwabeba kuwapeleka na kuwarudisha halafu tunatumia hela kwa sababu kila mwezi lazima nitenge bilioni 1.7 kwa ajili ya chakula cha magereza.

Thi is our country, tunatakiwa tuibadilishe sisi, tusitegemee mtu mwingine kutoka nje wa kuibadilisha Tanzania. Kila mmoja aji-commit katika mahali pake alipo, kama ni jaji toa hukumu kweli haraka haraka. Kwa mfano wale waliohukumu wakatoa maamuzi ya kesi zaidi ya 900 niletee majina yao na mimi niwaandikie barua ya kuwapongeza, na hiyo ndiyo motivation, na hata kama ni kuwaongezea mshahara hao ndiyo wa ku promote. Nchi yetu hii tuna majaji wazuri mno, lakini saa zingine tuna wa-discourage, akishamwona mwenzake anafanya ya ajabu, yeye kila siku anahukumu kwa msimamo mzuri mwenzake anafanya mambo ya ajabu.

Na ndio maana hata hawa majaji waliostaafu ukiwaona ni wembamba wembamba tu kama mimi, namuona Jaji Msumi yuko hivyo hivyo, jaji yaani hivyo hivyo,  Jaji Bomani yuko hivyo hivyo nywele zinaondoka tu, hata ukimwangalia Jaji aliyesimamia Uchanguzi wa Tanzania alimtanguliza Mungu uchaguzi ulikuwa wa ajabu wakamwwekea maneno mengi kwenye mdomo, lakini akasimama imara. Na mimi nikapenyeza nikawa rais, Who I am?

Ingawaje najua nakipata cha moto kwa sababu kazi hii ni ngumu kweli, Mheshimiwa Jaji Mkuu nisingependa nipoteze muda wenu kwa wingi, lakini nasema kwa dhati nina imani kubwa na Mahakama, nina imani kubwa na wewe. Ninafahamu changamoto zilizopo, ni nyingi, ni nyingi lakini nataka kukuhakikishia tutazitatua wote pamoja. Naomba watendaji wote wa Mahakama mniamini, sitawaangusha, sitawaangusha na nitafanya kazi kweli na ninyi. Kuna watendaji wazuri, ninajua wataziwasilisha shida zenu. Na kwa sababu hizo fedha hamjapata zozote kwenye mgao unaokuja, waziri unikumbushe lazima nitoe pesa na inawezekana zikasaidia hata kutoa hukumu za kuzipata hizo trilioni moja zinazokwepwa.

Si umesema bilioni 12? Bilioni ngapi, 12.3. Nikuahidi kitu? Nataka nikuhakikishie ndani ya siku tano nitakupa zote hizo bilioni 12.3 ila hizo kesi za watu waliokwepa zile in five days ninakupa hizo fedha na Chief Secretary kwa sababu uko hapa, Chief Secretary toa instruction kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha zipatikane hizo fedha ikiwezekana hata kesho hata keshokutwa wapelekewe. Halafu kazi ibaki ya… ndiyo faida ya kuwa rais mzee wangu.

Mheshimiwa Jaji Mkuu, Waheshimiwa Majaji wote mliopo hapa, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa viongozi sana mliopo hapa niliona nizungumze haya ambayo nilitaka kuyazungumza. Mnisamehe sana kama kuna mahali nimewakwaza, lakini nilitaka nizungumze yaliyomo moyoni mwangu. Hotuba yangu iko hapa sikuyaweka sana, unajua ukifuata sana yanayoandikwa humu utasoma hotuba ya yule aliyekuandikia-siyo hotuba yako.

Na mimi nilitaka nitoe hotuba yangu ili mhimili huu muhimu wa Mahakama unielewe ili twende pamoja. Tuna lengo moja kubwa la kuijenga nchi yetu, kuijenga Tanzania mpya, Tanzania yenye maendeleo, Tanzania isiyo na kero, Tanzania yenye amani, Tanzania inayozingatia sheria kwa  sababu hata kauli yangu ya ‘Hapa Kazi Tu’, hata kwenye maandiko wanasema asiyefanyakazi na asile. Na asipokula si maana yake afe kwa hiyo ninaamini kwamba ushirikiano wa Serikali yangu ninayoiongoza nataka niwahakikishie na nikuhakikishie Mheshimiwa Jaji Mkuu tutakupa support yote ili hii mikwamo mikwamo iweze kuisha, lakini na mimi yale niliyoyasema basi na mimi unizingatie hayo angalau kwa kuyatekeleza ili twende pamoja kwa faida ya nchi yetu. Mwisho, napenda kuwatakia watumishi wote wa Mahakama na wadau wote wa utoaji haki kazi njema mnapoanza shughuli za Mahakama kwa mwaka huu wa 2016.

 

Mungu Ibariki Tanzania,

Mungu wabariki wafanyakazi wote wa Mahakama

Ahsanteni sana. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.

By Jamhuri