Baada ya Gazeti JAMHURI kuchapisha taarifa za kiuchunguzi za mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwa katika hali mbaya kifedha kutokana na deni kubwa linaloikabili kwa Serikali kushindwa kulipa madeni yake, hali inayoifanya baadhi ya mifuko kushindwa kulipa mafao kwa wastaafu, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imetoa ufafanuzi na kueleza hatua ambazo zikichukuliwa mifuko hii itabaki salama. Endelea…

 

Utangulizi

Jukumu la Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ni kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii Ili kutimiza azma hiyo kifungu 135 cha Sheria  Na. 5 ya mwaka 2012 kinaipa Mamlaka jukumu la kufanya tathmini kila baada ya miaka 3. Hivyo Mamlaka iliingia mkataba na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa lengo la kufanya tathmini ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Tathmini hii pamoja na mambo mengine ililenga kutekeleza mapendekezo ya wadau yaliyohitaji kufahamu hali halisi ya sekta, gharama za uendeshaji na kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

 

HALI YA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII

Sekta ya Hifadhi ya Jamii ina mifuko saba ya msingi (Mandatory Social Security Schemes) ambayo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa LAPF, Mfuko wa PPF, Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF pamoja na Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (WCF).

 

Takwimu za Sekta kwa kipindi kinachoishia Juni 2015

• Wanachama milion 2.1

• Rasilimali = shilingi Trilioni 8.78

• Michango = shilingi Trilioni 1.9

• Mafao yaliyolipwa = shilingi Trilioni 1.36

• Uwekezaji = shilingi Trilion7.1

• Wastaafu = 89, 532

Deni la pensheni limepungua kutoka asilimia 58 ya Pato la Taifa mwaka 2010 hadi asilimia 25 mwaka 2015.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inalipa mafao ya muda mrefu kama vile fao la Pensheni ya Uzee, Mirathi na Ulemavu. Kwa upande wa mafao ya muda mfupi, Mifuko inalipa mafao ya Uzazi, Elimu, Afya, Mazishi na Kuumia kazini pamoja na huduma zingine kama vile Mikopo ya makazi, elimu na mikopo ya kuanza maisha baada ya kuajiriwa.

 

MATOKEO YA TATHMINI

UMRI WA KUISHI BAADA YA KUSTAAFU

Tathmini imebainisha kuwa umri wa kuishi baada ya kustaafu umeongezeka kufikia miaka 20.8 kwa wanaume, na miaka 22.2 kwa wanawake. Hali hii itaendelea kuwa nzuri zaidi kadiri miaka inavyoongezeka ambapo kwa kipindi cha miaka 50 ijayo umri wa kuishi baada ya kustaafu kwa wanaume itakuwa miaka 22.9 na wanawake miaka 24.9.

 

VIWANGO VYA PENSHENI

Pensheni imeboreshwa kutoka wastani wa asilimia 67 hadi asilimia 72.5. Hata hivyo, kwa mifuko inayolipa mkupuo wa asilimia 50 viwango vya pensheni kwa mwezi ni asilimia 27 ya mshahara. Hiki ni kiwango cha chini sana, kiwango kinachotakiwa kimataifa ni asilimia 40. Tathmini imeonesha kwamba kutumia mshahara wa mwisho kwenye kukokotoa mafao ni jambo linalohitaji kuangaliwa upya na kwa umakini mkubwa kwani una madhara makubwa kwa wanachama wanaobaki kwenye mifuko. Tathmini imesisitiza umuhimu wa kufanya uthaminishaji (indexation) ili pensheni ziendane na ukuaji wa gharama za maisha. Tathmini inaonesha kwamba kwa kiwango cha mkupuo wa asilimia 50 mifuko haitoweza kuthaminisha pensheni.

 

UIMARA WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Tathmini inaonesha kwamba mifuko imeimarika. Mifuko ina uwezo kwa kustawi hadi kufika mwaka 2085 na 2075 kwa mfuko wa NSSF na PPF. Tathmini inaonesha kwamba Mfuko wa LAPF na GEPF una uwezo wa kufika zaidi ya mwaka 2058 na 2047. Na iwapo vikokotoo vyao vitarekebishwa mifuko hii itaweza kufika mwaka 2085. Hali kadhalika iwapo Mfuko wa PSPF utapokea michango ya kabla ya 1999 na kufanya marekebisho yanayopendekezwa kwa GEPF na LAPF Mfuko huu utadumu hadi mwaka 2075. Vilevile Mfuko huu utaimarika iwapo mafao yatarekebishwa au michango kuongezwa hadi kufika asilimia 28 badala ya asilimia 20. Suala hili litategemea zaidi uamuzi wa wadau.

 

GHARAMA ZA UENDESHAJI MIFUKO

Kwa ujumla, mifuko imeonekana kuwa na gharama kubwa ya uendeshaji. Mfuko wenye gharama ndogo ya uendeshaji ni PSPF. Kuwapo kwa gharama kubwa za uendeshaji kutazorotesha utendaji wa mifuko. Hivyo, kwenye jambo hili Mamlaka imeanza kuandaa kanuni za kushusha gharama za uendeshaji. Mifuko yote haitaruhusiwa kuwa na gharama inayozidi asilimia 10 kuanzia July 2016. Sheria zinazoruhusu mifuko kutumia asilimia 15 zitarekebishwa.

 

KASI KUBWA YA WANAOJITOA KATIKA MIFUKO

Tathmini hii imebainisha kiwango kikubwa cha wanachama kujitoa katika uchangiaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Tatizo hili linajitokeza hasa kwa Mifuko ya PPF na NSSF licha ya ukweli kwamba utaratibu huu haupo kwenye sheria husika. Tathmini inaonesha kwamba Mfuko wa NSSF umelipa zaidi ya asilimia 85 ya malipo ya mafao yote kwa wanaojitoa. Ili kuondokana na tatizo hili Mamlaka inaandaa mfumo wa bima ya kukosa ajira (unemployment insurance benefits) ili kuwezesha wanaokosa kazi kupata bima wakati wakitafuta ajira sehemu nyingine.

 

KUINGILIANA KWA MAFAO

Tathmini imeonesha kuwa ukiacha mafao ya muda mrefu, NSSF wanatoa mafao ya Bima ya Afya pamoja na Fao la Kuumia Kazini wakati huo huo, Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) hutoa huduma za bima ya afya. Vilevile Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) nao unajishughulisha na fao la kuumia kazini, tathmini inashauri mafao haya yaondolewe NSSF na kuacha Mfuko wa Bima ya Afya ushughulike na bima zote za afya. Hii itapunguza gharama kwa waajiri na kuboresha mafao kwa wanachama.

 

UWIANO WA WACHANGIAJI NA WASTAAFU

Tathmini inaonesha kuwa kila mfuko upo katika kiwango chake cha ukuaji. Kiwango cha idadi ya wanachama kufikia 1.95 milioni wakati idadi ya wanaopokea pensheni kufikia 97,428. Hii ni uwiano wa wanachama 20 kwa mstaafu mmoja. Hiki ni kiwango kizuri kwa sekta. Hata hivyo mifuko yenye wastaafu wengi hasa PSPF na PPF inapaswa kuongeza wanachama wake maradufu.

 

KUUNGANISHA MIFUKO

Kwa lengo la kupunguza gharama za mafao, gharama za uendeshaji wa mifuko pamoja na kuboresha huduma, tathmini inapendekeza mifuko yote iunganishwe. Hata hivyo, mtathmini ametahadharisha kwamba jambo hili lifanyike kwa umakini mkubwa na lifanyike kwa awamu ili kuzuia athari zinazoweza kutokana na kuunganisha mifuko hii. Taarifa imependekeza kuunganisha mifuko katika namna ifuatayo; Namna ya kwanza ni kuwa na mifuko miwili yaani ya Mfuko wa Sekta ya Umma (GEPF, PSPF na LAPF) na Mfuko wa Sekta Binafsi (NSSF na PPF). Namna ya pili ni kuunganisha mifuko yote kuwa na Mfuko mmoja tu.Hili linategemea mapendekezo ya wadau na linahitaji ushauri wa kitaalamu zaidi. Tunatarajia kwamba mtathmini atafanyia kazi maoni ya wadau na kushauri njia bora ya kuunganisha mifuko hii.

 

TAARIFA KUHUSU MADENI YA SERIKALI KWA MIFUKO

Hivi karibuni kumekuwa na hofu kubwa kwa wanachama na wadau mbalimbali kuhusu madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

 

MADENI YA MICHANGO

Kuhusu deni la michango ya wanachama kwa PSPF, taarifa zinaonesha tayari Serikali imeanza kulishughulikia. Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwezi kuanzia Novemba 2015 kwa ajili ya kulipa michango iliyocheleweshwa.

Taarifa ambayo Mamlaka imepokea hivi karibuni ni kwamba Serikali inatoa hati fungani (non-cash bond) ya Shilingi Trilioni 2.6 yenye riba ya asilimia 6.5 kwenda PSPF. Hati fungani hii itaiva kwa muda tofauti ili kuwezesha mfuko kukidhi mahitaji yake ya malipo ya mafao. Hati fungani hizi zitaiva kwa vipindi tofauti tofauti. Yaani kuna hati fungani za miaka 3, miaka 5; miaka 7; miaka 10 na kuendelea.

 

MADENI YA MIRADI

Malipo kwa ajili ya miradi ya Serikali nayo yamekamilika na Serikali imeridhia kulipa madeni hayo kwa mifuko yote kadiri ambayo zoezi la usuluhishi (reconciliation) linavyokamilika. Mifuko ambayo imekamilisha ni NHIF, GEPF, PPF, LAPF na NSSF. Mfuko ambao bado haujakamilisha ni PSPF.

Hitimisho

Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa ushirikiano mkubwa tunaopata toka kwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu; Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Afya; Benki Kuu ya Tanzania; Vyama vya Wafanyakazi; chama cha Waajiri; vyombo vya habari pamoja na wadau wote kwa ujumla.

Mwisho, Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii inapenda kuwatoa hofu wanachama na wadau wengine wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwamba sekta ipo imara. Iwapo kuna malalamiko, ushauri au maoni yoyote kuhusiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tafadhali msisite kuwasiliana na Mamlaka ili yapatiwe ufumbuzi mapema iwezekanavyo.

3732 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!