Hotuba ya Rais Magufuli mkoani Simiyu

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame, Waheshimiwa Waziri Hajji kutoka Zanzibar, Mheshimiwa Naibu Waziri Luhaga Mpina, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Simiyu, Waheshimiwa wabunge wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo hili la Bariadi, Mtemi Chenge, Waheshimiwa viongozi wa dini mlioko hapa.

Waheashimiwa madiwani, Waheshimiwa viongozi wote wa vyama mbalimbali mlioko hapa, Waheshimiwa wananchi, Assalaam Aleykum.

Ndugu zangu wananchi wa Simiyu, naomba basi tusikilizane ndugu zangu. Wananchi wa Simiyu kwanza nianze kwa kuwashukuru sana, ninawashukuru sana kwa makaribisho makubwa sana ya leo. Ukweli, Simiyu mmefunika, hongereni sana. Kwa kweli Simiyu mmefunika.

Ndugu zangu wananchi wa Simiyu na Bariadi kwa ujumla, nimeona leo nianzie hapa Simiyu. Lengo kubwa la kuja hapa ndugu zangu kwanza ni kuja kuwashukuru.

Nimekuja kuwashukuru sana wananchi wa Simiyu mwaka tuliopita hapa wakati tukiomba kura, tulikuja watu wengi, na kila mmoja alikuwa anajieleza kwa sera zake. Ninyi ndugu zangu Watanzania pamoja na wananchi wa Simiyu mlikaa mkatusikiliza, mkatupima, mkaamua.

Na katika maamuzi hayo Mungu aliwatangulia, mkaguswa mioyoni mwenu, mkaamua kumchagua Magufuli. Ninawashukuru sana kwa kura mlizonipa. Lakini vile vile, kwa hapa Bariadi mkamchagua Mheshimiwa Chenge, ninawashukuru sana.

Lakini kwa majimbo mengine katika Mkoa huu wa Simiyu, mkachagua wabunge wote wa CCM, ninawashukuru sana. Lakini mkaamua pia kuchagua madiwani wa CCM wengi. Na halmashauri zote za wilaya katika Mkoa wa Simiyu zinaongozwa na wenyeviti wanaotoka Chama Cha Mapinduzi, ninawashukuru sana.

Kwa hiyo, ndugu zangu wa Simiyu, nimefika hapa kutoa shukrani zangu. Katika maandiko yote yanasema shukuruni kwa kila wakati, nimekuja kuwashukuru asanteni sana, kwa kutupa kura nyingi ambazo zimetuwezesha kuunda Serikali ya Awamu ya Tano. Na ninataka niwaahidi, mimi mwenyewe pamoja na viongozi wengine mliowachagua wabunge na madiwani, hatutowaangusha. Tutawafanyia kazi.

Simiyu oyee, jambo kubwa ndugu zangu wa Simiyu ilikuwa ni kuja kuwashukuru, na nafikiri shukrani zangu mmezipokea. Ndugu zangu wananchi wa Simiyu tulipokuwa tukizunguka, tukiomba kura, tulieleza yale ambayo tulikuwa tumepanga kuwatumikia Watanzania.

Yako mengi tuliyoyaahidi, na siku zote ndugu zangu ahadi ni deni. Ukishaahidi wewe kama una hofu ya Mungu, ni lazima utekeleze. Na mimi ninaamini sisi wote mliotuchagua tuna hofu ya Mungu, kwa hiyo tunawajibika kutekeleza.

Tunatambua kwamba cheo ni dhamana, mmetupa dhamana ya kufanya haya ambayo tuliahidi kuyafanya. Nataka niwahakikishie ndugu zangu wananchi wa Simiyu na Watanzania wote, yale yote tuliyoahidi kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi tutayatekeleza kwa nguvu zetu zote.

Ndugu zangu, tulipokuwa tukiomba kura, kwa sababu nataka nizungumze na ya jumla halafu baadaye nitakuja na haya mawili tuliyomalizia. Tuliahidi kutoa elimu bure, tulipoingia madarakani ile ilikuwa ni ahadi yetu namba moja. 

Tukaamua kutengeneza makusanyo mazuri katika Serikali, tukaongeza makusanyo ya Serikali kutoka kwa mwezi bilioni 800 hadi trilioni 1.2. Baada ya kukusanya hizi fedha, tuliamua hizi fedha zianze kutumika kwa watoto masikini. Tukawa tunatenga bilioni 18.777 kila mwezi ili ziweze kutoa elimu bure.

Tulijua tusipoanza kutoa elimu bure kwa watoto wetu, watoto wengi walikuwa hawaendi shuleni. Akishaenda shuleni anaambiwa akalete karo, anarudishwa kama yuko karibu na ziwani anaenda kuroa samaki (anaongea Kisukuma) au anaenda kufanya mambo mengine. Kwa hiyo vijana wetu wengi wakawa hawaendi shuleni.

Baada ya mpango ule wa kutoa bilioni 18.777 na zile fedha tukaamua ziende moja kwa moja kwa walimu, kwa sababu zingepitia mkoani mpaka wilayani kwenye hamashauri ndipo zikaende kwa walimu zisingefika. Zingefika zimepungua, nao wangezichuja huko. Tukasema zinaenda moja kwa moja kwa walimu, ili mwalimu akizipoteza anatumbuliwa yeye huko huko moja kwa moja.

Tulifanya hivi kwa lengo la kuhakikisha vijana wetu, watoto wetu wanasoma. Baada ya kufanya hivyo idadi ya watoto wetu waliojiandikisha kuingia darasa la kwanza imeongezeka karibu mara mbili.

Mwaka juzi walikuwa wanafunzi milioni moja mwaka huu wamekuwa milioni 1.98, karibu milion 2. Na tulipoanza wanafunzi wengi kuingia tukawa na tatizo la madawati, tumejitahidi na waimbaji wameimba na kwaya ya walimu wameimba kwaya nzuri sana. Madawati yameanza kupatikana, mpaka sasa hivi katika madawati kwenye shule za msingi na sekondari yameshafika karibu 95% katika mikoa yote.

Ninawashukuru Watanzania, ninawashukuru walimu, ninawashukuru wazazi kwa imani kubwa mliyoitoa kwa Serikali tunayoiongoza.

Ndugu zangu Watanzania yako mengi, tumejipanga. Ninafahamu katika mambo mazuri yaliyopo mabaya huwa yamejitokeza. 

Katika siku nyingi pamekuwa na mtindo wa mambo mabaya mabaya kidogo, ufisadi, wizi. Tuliamua kwenda nao mbele kwa mbele. Kwa kuchukua hatua za pale pale.

Nilipokuwa nikiomba kura ndugu zangu niliwaeleza, kwamba mimi mfanyakazi akiharibu Bariadi, siwezi nikampeleka Maswa. Akiharibu Bariadi, anafia pale pale Bariadi.

Nilizungumza nikiwa ninaomba kura, ili kusudi Watanzania wanielewe nia yangu ilikuwa ni nini, nilikuwa nazungumza kiukweli na sikutaka kuzungumza uongo. Kwamba mtu ukiharibu Mwanza hutoletwa Shinyanga. Ukiharibu Shinyanga hutapelekwa Dar es Salaam.

Ukiharibu Shinyanga, unafukuziwa huko huko Shinyanga. Tumeanza kufanya hivyo, ninafahamu katika hatua zozote unapochukua za kurekebisha nchi, wako watu wanaolalamika. Na hasa waale wachache ambao walikuwa wanafaidi na huo mlolongo wa kula jasho la watu maskini.

Nataka niwahakikishie ndugu zangu wanasimiyu na Watanzania, sitabadilika msimamo wangu uko pale pale. Ninachowaomba, wanasimiyu na Watanzania muendelee kuniombea na muendelee kuiombea Serikali. Tunataka tutengeneze Tanzania mpya. Sio Tanzania ya kudhulumu watu maskini.

Tunataka kila mmoja apate jasho lake, sio wawepo wengine kwa sababu ya vyeo vyao wale jasho la watu wengine. Tanzania hii haitakiwi kuwa maskini. Tanzania ina kila kitu.

Bariadi hii kwa mwaka jana ndiyo inayoongoza kwa kuuza pamba katika Tanzania kwa 55%, Bariadi hii ng’ombe zipo aina zote, Simiyu hii dhahabu zipo. Ukienda mbele kidogo hifadhi ya Taifa ipo kubwa Serengeti wanyama wapo.

Watu wanatoka Ulaya kuja kuangalia wanyama, Tanzania ina kila kitu. Lakini kwanini Tanzania tuwe maskini? Ni lazima umasikini wetu ‘either’ ni wa kujitakia, au kuna watu walitutelekeza tuwe maskini.

Sasa kama kuna watu ambao walitutelekeza tuwe maskini, hao ndiyo mimi ninapambana nao, naomba mniunge mkono. Kwa sababu nina uhakina hakuna Mtanzania yeyote, awe mzee awe kijana, awe mtoto anayependa umaskini.

Kila mmoja anayapenda maisha mazuri, kila mmoja anapenda huduma nzuri, kila mmoja anapenda kula matunda mzuri ya nchi yake aliyopewa na Mungu. Sisi viongozi tuna wajibu wa kuyatekeleza haya.

Na ndiyo maana ndugu zangu ninazungumza kwa dhati na leo ninarudia, Serikali ninayoiongoza, imejipanga kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania hawa Watanzania wanyonge. 

Na ndiyo maana katika bajeti ya mwaka jana, bajeti yote ni trilioni 29.5 lakini kwa mara ya kwanza, tumetenga 40% ya fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo. Haijawahi kutokea tangu dunia iundwe Tanzania kupanga 40% ya fedha kwenda kwenye maendeleo. Mara ya mwisho ilikuwa ni 26% au 27%. Zingine zote zilikuwa zinaenda kwenye chai, kwenye semina, kwenye makongamano, kwenye safari n.k.

Sasa tumeamua kubadilisha mwelekeo huo, kutoka 26% ya fedha za maendeleo kwenda 40%. Ukishaamua kutoka 26% kwenda 40% lazima ujue kuna watu wamekwazika. Wale waliokuwa wamezoea lazima watalalamika.

Kwa hiyo, nataka niwaambie ndugu zangu wanasimiyu na Watanzania kwa ujumla mnaosikia wanalalamika sana ni wale waliokuwa wanafaidi na hizo fedha. Ninyi hamkufaidi na hizo fedha, hizo fedha walikuwepo wachache waliokuwa wanafaidi nazo.

Na mimi nataka walalamike, na wakitaka walalamike sana. Kwa sababu Watanzania wengi wanataka fedha ziende kwa maendeleo yao. Simiyu oyee.

Ninyi hamtaki fedha hizo ziende kwenye maendeleo yenu? Wangapi wanataka hizo fedha ziende kwenye maendeleo yao? Ninawashukuru sana. 

Na kwa sababu hiyo tumeanza, bilioni 18.777 zinaenda kwenye elimu, tunataka ziende kwenye maendeleo ya watoto wetu. 

Bajeti ya mwaka jana, fedha zilizoenda kwa ajili ya kufadhili watoto wa vyuo vikuu ilikuwa bilioni 378, mwaka huu ni bilioni 483. Mwaka jana wanafunzi waliofadhiliwa kwenda chuo kikuu walikuwa 98,000 mwaka huu ni 124,000. Ni kwa sababu fedha zimeongezeka. 

Kutokana na fedha hizo tunataka ziende kwenye maendeleo, Tanzania yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 50 ilifikia mahali hatuna hata ndege. Zinakuja ndege za watu binafsi, wanaamua kupanga bei wanavyotaka. Kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam nauli ilikuwa imefika 800,000 mpaka 900,000 na kwenye sikukuu kama za Krismasi na Mwaka Mpya zingeweza kufika hata milioni moja.

Tukaamua, nchi ya Tanzania yenye watu milioni 50, haiwezi ikawa haina ndege. Tumenunua ndege sita, ndege mbili zimeshaanza zimeshafika, nyingine zitafika mwaka huu na nyingine zitafika mwaka kesho.

Baada ya kuleta tu ndege mbili, bei imeshuka kutoka nauli ya kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kutoka laki 8, laki 9 hadi laki 2. Simiyu oyee. Hayo ndiyo maendeleo tunayoyataka. 

Lakini hakuna nchi yoyote duniani, duniani ambayo iliweza kuleta watalii wengi bila kuwa na shirika lake la ndege. Usipokuwa na shirika lako la ndege watalii watakaokuwa wanakuja nchi yako, lazima wapitie kwenye nchi zenye ndege. Wanaotaka ndiyo wanakuja huku.

Tumeamua kuinua utalii, nilikuwa nazungumza na Waziri  Profesa Mbarawa, tunataka katika mpango ikiwezekana mwaka kesho hapa Bariadi tujenge uwanja wa ndege. Bariadi oyee, Simiyu oyee.

Ili watalii wanapokuja hapa, hapa wataenda tu karibu kwenye mbuga. Na wakishakuja watalii hapa, uchumi wa wananchi wa Bariadi utaimarika. Wenye magesti watalaza Wazungu, Simiyu oyeee.

Anayetaka kuuza maandazi atauza, anayetaka kuuza tikitimaji atauza, hayo ndiyo maendeleo tunayoyataka ya Watanzania wa Simiyu. Simiyu oyee. Hiyo ndiyo Serikali na hivyo ndivyo tulivyoahidi.

Ndugu zangu, katika fedha hizo hizo za maendeleo, tumepanga kuhakikisha miradi ya barabara ambayo ilianza kwa kujengwa kwa fedha zetu tuiendeleze. Ninafahamu, nimekuwa Waziri wa Ujenzi kwa miaka mingi, hata hii barabara wakati ninabomoa nyumba hapa wapo waliolalamika lakini nikasema watacheka siku moja na barabara tulibomoa. Na hilo nasema kwa dhati, kwa sababu tusingebomoa tusingejenga hii barabara.

Lakini wapo hata wahandisi wa TanRoads wanafahamu, Kibea, aliyekuwa Mhandisi wa Mkoa huu, nilimfukuzia hapa hapa Bariadi. 

Katika maendeleo machungu lazima yawepo, hata huyu kandarasi alipokuwa akisuasua tuliwafukuza ‘maproject’ injinia wao watatu wakarudi China. Ukitaka kufanya kazi lazima wawepo wa kuumia. Waliumia kwa faida ya wanaSimiyu.

Niwaombe radhi walioumia lakini wakaumie salama kwa faida ya wanaSimiyu. Nilifanya hivyo kwa sababu nilitaka barabara iwepo, nilifanya hivyo kwa sababu ninafahamu maendeleo ya Simiyu hayawezi kuwepo bila kuwa na barabara ya lami.

Nataka niwahakikishie kwa wale ambao walisimamia vizuri ujenzi wa barabara hii nawapongeza sana. Mheshimiwa Waziri nakupongeza, Katibu Mkuu nakupongeza na TanRoads nawapongeza. 

Baada ya kumleta yule mhandisi nafikiri anaitwa Kent mambo yamebadilika na mradi umekamilika. TanRoads nawapongeza na kwa ufupi ninawamisi kweli. Simiyu oyee.

Nataka niwahakikishie ndugu zangu wanaSimiyu kutoka Lamadi hadi Bariadi kilometa 71.8 zimekamilika, fedha zilizotumika ni bilioni 90.068 na fedha zote 100% zimetolewa na Serikali. Hakuna mkopo, hakuna fedha tuliyoomba nje. Tanzania oyee.

Kama tunaweza tukajenga kwa fedha zetu, hatuwezi tukashindwa kilometa zilizobaki. Tumeshatangaza tenda na kandarasi yupo kwenye zile kilometa 51.3 kutoka Mwigumbi hadi Maswa nako ninakwenda kuweka jiwe la msingi. Zitakuwa zimebaki kilometa 48.9.

Kwa sababu mimi ndiyo Rais, niseme nisiseme? Kwa sababu mimi ndiyo Rais, na ninafahamu mwezi huu Wizara ya Ujenzi nimewapa bilioni 100, za kulipa makandarasi na kwa sababu ninajua tutapata wapi pesa, ninatoa maagizo kwa waziri, natoa maagizo kwa waziri, wa Mawasiliano Uchukuzi na Ujenzi hizi kilometa 48.9 zilizobaki ndani ya wiki moja nazo zitangaze kwa ajili ya ujenzi wa lami, Simiyu oyee.

Msiulize fedha zitatoka wapi, nitatoa fedha. Tangazeni tenda, kwa sababu barabara hii inapunguza zaidi ya kilometa 100 na kitu kwa magari yanayotoka Nairobi. Yalikuwa yanalazimika kutoka Nairobi, yapite Lamadi, yaende Mwanza, yakapite Usagara, yaende Shinyanga ndipo yaende Dar es Salaam.

Kwa sasa hivi, yatakuwa yanatoka Nairobi, au hata yatoke South Sudan yanapita Sirari, yanapita Lamadi, yanapita Bariadi yanaelekea kule yanakoelekea. 

Na kwa njia hiyo, wananchi wa Mkoa wa Simiyu watafanya biashara, mwenye matikiti maji yake atayalima hapa yatakwenda kuliwa Dar es Salaam haraka kabla hayajaharibika, mwenye mahindi yake atayauza haraka yatafika yanakoenda. Kwa sababu ataenda kwenye barabara ya lami haraka. Simiyu oyee.

Nasema uongo ndugu zangu? Na hayo ndiyo maendeleo tunayoyataka. Ombi langu wananchi wa Simiyu muitumie hii barabara. Barabara hii muitunze ili na ninyi iwatunze. 

Imekuwa ni kawaida saa zingine barabara zinapojengwa imekuwa ni chanzo cha ajali. Madereva wanaendesha kwa fujo, kunakuwa na barabara nzuri, badala ya barabara hiyo kuwatunza Watanzania inakuwa ndiyo chanzo cha mauaji ya Watanzania.

Napenda nitoe wito kwa madereva, natoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama simamieni sheria za usalama barabarani. Ili kukamilika kwa barabara hii nisije nikasikia tena baada ya siku chache kwamba imeua watu kadhaa. Iwe barabara ya amani, tumeipata kwa amani, kwa fedha za Watanzania, iwe barabara kwa ajili ya maendeleo. Hilo ndilo ombi langu kwenu wanaSimiyu.

Ombo langu la pili kwa barabara hii niwaombe wanaSimiyu muitumie barabara hii kwa biashara na kufanya biashara kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya biashara kwa kutumia hii barabara aitumie.

Mwenye samaki anayeuza barabarani auze, mwenye matikiti maji anayetaka kusafirisha kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar kwa Mheshimiwa Haji apeleke, mwenye mtama anataka kusafirisha asafirishe. Mwenye ng’ombe wake anataka kupeleka kwenye mnada apeleke kwa kupakia kwenye magari, hapo ndipo tutaiona faida ya barabara hii….

 

>>ITAENDELEA