Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana imeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kubaini wafanyakazi raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini bila vibali.

Wiki iliyopita, viongozi wa wizara hiyo walivamia ofisi za kampuni ya mawasiliano ya Huawei zilizopo eneo la Victoria na Makumbusho jijini Dar es Salaam, na kubaini wafanyakazi raia wa kigeni 50, kati yao ni wanane pekee waliokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Ziara hiyo ya ghafla iliongozwa na Kamishna wa Kazi nchini, Hilda Kabisa, akiwa na maofisa wanne na askari polisi wanne kutoka Kituo cha Oysterbay.

Wakati kazi hiyo ikiendelea, baadhi ya raia wa China walijificha vyooni kukwepa kukamatwa.

Kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wasamaria wema, juu ya utitiri wa raia wa kigeni katika kampuni ya Huawei hapa nchini, wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Kumekuwa na juhudi za makusudi za wawekezaji wengi kujaribu kurubuni kutoandikwa, au kutangazwa habari za wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini bila vibali.

Katika ofisi za Huawei Tigo Project zilizopo Makumbusho ndiko walikobainika raia hao 50 wasiokuwa na vibali kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana. Maofisa walioshiriki kwenye kazi hiyo ya kuwabaini raia wa kigeni walichukua nyaraka za wageni hao.

“Pale tumebaini mambo ya ajabu kweli kweli, maana wenye vigezo ni wanane tu kati ya zaidi ya 50. Lakini tumeambiwa kuwa tumekwenda muda mbaya, tungewapata wengi zaidi. Ila tatizo kubwa lipo Idara ya Uhamiaji ndiyo wanaotuangusha,” alisema mmoja wa maofisa wa wizara hiyo.

JAMHURI imeelezwa kuwa wafanyakazi wa Huawei wamekuwa wakiingia na kutoka kazini kwa zamu; jambo linaloashiria kuwa idadi yao ni kubwa. Imeelezwa pia kuwa wanaoingia mchana walau wana vibali, lakini wanaoingia usiku karibu wote hawana vibali vya kufanya kazi nchini, hivyo wanaingia muda huo wakitambua kuwa si rahisi vyombo vya dola kuwafuatilia.

Baadhi yao wamebainika kutumia vibali vinavyowatambulisha kuwa ni wafanyabiashara, badala ya vibali vya kazi. 

Tangu Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana ipige marufuku vibali vya kazi vya muda (CTA), Huawei wamekuwa wakibadili mbinu. 

Uchunguzi unaonesha kuwa raia hao wa China miongoni mwao hufanya kazi za kiofisi wakiwa katika makazi yao kwa kutumia njia ya VPN (Virtual Private Network) nyakati za mchana, na kwenda ofisini usiku; hiyo ikiwa ni mbinu ya kukwepa vyombo vya dola.

Huawei ni miongoni mwa kampuni zinazotajwa kwamba zina wafanyakazi wasio na vibali, lakini maofisa wa Uhamiaji, hasa Mkoa wa Dar es Salaam, wamekuwa wamelifumbia macho suala hilo licha ya kulifahamu.

“Pale (Huawei) huwezi kutia mguu kama kweli unaipenda kazi yako. Tulishawakamata sana na kuwaleta mpaka ofisini kwetu, lakini mkuu wetu anajua ana siri gani na hii kampuni. Kwa sisi ambao bado tunataka watoto wetu waendelee kupata ugali hatuthubutu kuweka mguu hapo. Ila nakwambia yapo makampuni na hoteli ambazo huwezi kuzigusa labda kama unataka kibarua kiote nyasi,” anasema mmoja wa wafanyakazi wa Uhamiaji.

Idara ya Uhamiaji imewapatia viza ya biashara kwa kile kinachoelezwa kuwa ni ugumu wa sasa kwa raia wa kigeni kupewa vibali vya kazi. Viza ya aina hiyo muda wake ni miezi mitatu, lakini wamebainika kuwapo Wachina waliozitumia kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya raia hao wa kigeni hati zao za kusafiria zimegongwa mhuri wa mpaka wa nchi jirani ya Kenya na Tanzania (Namanga), walipoulizwa iwapo wamewahi kufika nchini Kenya na Namanga walikana kupafahamu au hata kufika huko. Huu mchezo unafanywa na baadhi ya maofisa wa Uhamiaji Mkoa ambao wana maslahi na hii kampuni,” anasema mtoa habari wetu.

Anasema kuwa hapo awali kulikuwa na mtindo wa kuwagongea CTA zaidi ya mara tatu kwa wageni hapa nchini, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu. Baada ya Wizara ya Kazi kuzuia CTA, sasa kumeibuka mtindo wa kuwagongea ‘business visa’ kwa malipo ya dola 1,000 hadi 2,000. Gharama halisi ni dola 250 za Marekani.

Inaelezwa kuwa hati za wageni hao huchukuliwa na kupelekwa hadi maeneo ya mpakani kama Namanga ambako hugongwa mihuri na kisha kuwarejeshea wenyewe.

Kamishna wa Operesheni na Mipaka, Abdullah Abdullah, ameiambia JAMHURI kuwa Huawei iliwahi kukaguliwa na wapo baadhi ya wageni walikuwa wametuma maombi ya vibali Wizara ya Kazi, hivyo walikuwa wakisubiri majibu. 

Lakini amesema wapo ambao walikuwa hawana vibali, hivyo waliamuriwa kuondoka nchini. 

Anasema Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam alishamwandikia barua akimweleza kuwa wameondolewa nchini.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, alivitoza faini ya zaidi ya Sh milioni 60 viwanda vya Lodhia Plastic Industries Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka taratibu za kazi na kudharau Mamlaka ya Usalama Mahali pa Kazi (OSHA).

Akiwa katika kiwanda cha Sunflag, alibaini kuwapo wafanyakazi wasio na mikataba ya ajira na vitendea kazi vya kutosha, hivyo afya zao kuwa hatarini.

Alibaini kuwapo wafanyakazi 41 raia wa kigeni, wakifanya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na Watanzania.

Katika kiwanda cha Lodhia Plastic, alifuta kibali cha raia mmoja wa kigeni na kumuagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Raju Singh, kupeleka vibali 38 vya raia wa kigeni ili vikaguliwe.

1343 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!