Na Mwandishi Wetu

Polisi wanawashikilia wafanyakazi 22 wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART) inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Simon Group, Simon Kisena, JAMHURI limebaini.
Wafanyakazi hao wakiwamo wasaidizi wa karibu wa Kisena wanatajwa kuweka mfumo mbadala wa kuuza tiketi za mabasi ya mwendokasi unaoipotezea mapato Kampuni ya UDART.

“Wengi wameanza kukamatwa kama wiki mbili zilizopita. Uongozi wa UDA ulifanya ukaguzi wa ghafla katika Kituo cha Kimara na kubaini uwepo wa tiketi bandia. Tiketi hizo zilipoingizwa kwenye mashine ikashindwa kuzitambua,” amesema mtoa habari.
JAMHURI limefahamishwa kuwa Kituo cha Kimara ndicho kilianza kuwashitua kwani mapato yalishuka kutoka wastani wa Sh milioni 32 kwa siku hadi 18. “Upotevu wa karibu milioni 14 mfululizo kwa miezi miwili wakati hakuna mvua inayonyesha au ajali au nini, ulishitua kila mtu. Hapo ndipo uchunguzi ulianza,” kilisema chanzo chetu.

Septemba 12, mwaka huu walikwenda katika Kituo cha Kimara kufanya uchunguzi na walipofika hawakubaini lolote, lakini: “Baada ya kukuta hesabu zote zinalingana na tiketi zilizouzwa, kila mtu akawa anajiuliza kuna shida gani? Baadaye mwanafunzi mmoja akaingia na bahasha ofisi za kukatia tiketi.
“Mwanafunzi huyo akasema ameokota hiyo bahasha nje ikiwa na tiketi nyuma ya ofisi ya kukatia tiketi, akaona ni za UDA ikabidi azikabidhi. Msimamizi wa kituo akaona taarifa hiyo aifikishe kwa bosi wake. Hapo ndipo filamu nzima ilianza kuwa wazi.
“Kwenda kuangalia hata wasaidizi wa Mwenyekiti [Simon Kisena] wapo kwenye mchezo huu wa hujuma kubwa kwa kampuni. Kuwakamata hao wasaidizi wake, ikakutwa hata watoto wa wasaidizi wake ndio vinara wa kuchapisha tiketi hewa. Wana mitambo ya kuchapishia.
“Katika mshangao huo, uongozi ukawa unaamini kuwa haiwezekani mtu akawa na mtaji wa kununua mashine za aina hiyo, na ukawa unaamini watu hao wamewezeshwa na washindani wa Kisena kibiashara kuharibu mfumo na kuonyesha kuwa hafai kupewa kazi hii ya UDART kusafirisha watu kwa mwendokasi Dar es Salaam. Wanataka anyang’anywe na kupewa mtu mwingine. Hii ni hatari,” kilisema chanzo chetu.

Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa kati ya Julai na Septemba, mwaka huu kiasi cha fedha zilizoibwa ni zaidi ya Sh bilioni 1, kupitia utaratibu huo wa watumishi wa UDART waliokamatwa na watu wengine ofisini humo kuuza tiketi bandia.
Msemaji wa UDART, Deus Bugaywa, amelithibitishia JAMHURI kukamatwa kwa wafanyakazi hao na akaongeza: “Tulianza kuona mapato yanashuka, tukafanya uchunguzi wa ndani, tukapata suspects (watuhumiwa) wetu, tukaripoti polisi. Kuanzia hapo, polisi wakaendelea na uchunguzi.”

Amesema yamekuwapo matuko mengi yenye sura ya hujuma, kwani wamepata kubaini madereva wanaohujumu magari na hivi karibuni wamefukuza madereva wanane waliokuwa wanafundishwa na wabaya wa UDART jinsi ya kuharibu magari.
JAMHURI limejiridhisha kuwa wafanyakazi hao wamekamatwa, ila limehifadhi majina yao kwa sasa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, hakupatikana kulizungumzia suala hili.

910 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!