Ernest-ManguNamshukuru Mungu kuniamsha salama na mwenye akili timamu. Waraka wangu wa leo unamlenga moja kwa moja Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu. Nia yangu hasa ni kuonya na kukemea tabia ya baadhi ya viongozi wa jeshi hilo kujiingiza katika siasa hasa kuibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM), badala ya kuwalinda raia wanaofanya siasa na mali zao, sintofahamu hii haipendezi kabisa mbele ya jamii yetu.

Kuna ushahidi wa kutosha kwa yaliyojitokeza hivi karibuni ya watu kupigwa mabomu huko jijini Arusha karibu na Uwanja wa ndege na kukatolewa sababu zisizo za msingi juu ya kadhia ile; pia yalitokea huko Mwanza. Hali hiyo ni kinyume na wakati mgombea urais kwa tiketi ya CCM akizunguka nchini na ndege ya serikali, kulishuhudiwa pia maandamano mithili ya hayo yanayokataliwa, lakini zikakosekana sababu za kuyapiga mabomu!

Nikiri kusema kuwa maandamano hayo yameonekana safi, yananukia mithili ya manukato tofauti na ya mgombea wa urais wa Ukawa ambayo yameonekana kunuka mithili ya kenge aliyeoza. Tabia hii isiyo na afya kwa taifa letu inakirihisha na tunawataka iachwe maramoja, isituharibie kipindi hiki cha kampeni.

Ukweli ni kwamba tunaochagua Rais ni sisi wananchi na siyo ninyi viongozi wa majeshi.

Ni vema mkaacha kutuchonganisha na askari wetu kwa kuwapa amri zisizofaa na kuwajengea uadui na watu waliopa kulinda amani na mali zao. Na kumbuka askari hawa ni watoto wa Watanzania hawahawa na  huku uraiani tunaishi nao bila mikwaruzano yoyote. Kuna kipindi tunawaelewa kuwa wanafanya hayo siyo kwa matakwa yao, bali kuagizwa na pengine na hizo sheria na taratibu za kazi zao na ndio maana ninakuandikia wewe mwenye dhamana  ili hali hiyo iachwe.

Kuhusu swala la habari ya baadhi kushinikizwa au kushawishiwa wampigie kura mgombea fulani, hilo halitusumbui kwani wananchi tunaotaka mabadiliko tupo wengi nikiwemo mimi, kuliko baadhi ya askari hao.

Hivyo basi natoa rai  kwa makamanda wako wa mikoani kutoumia na kuamrisha mabomu pindi watakapoiona timu ya Ukawa kwani wananchi hatutaki uonevu wavumilie tu hayo ndiyo mambo ya siasa yalivyo!

Mwisho kabisa kama kuna mgombea mnayemtaka basi mjue si lazima tumtake na sisi wala na askari wenu.

 

Mungu akubariki kwa majukumu yako mazito.

0773-402133

By Jamhuri