GraphoGame (GG) au GrafoGemu kwa Kiswahili, ni mchezo unaotumia teknolojia rahisi ambao ulibuniwa na timu ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Jyvaskyla cha nchini Finland chini ya usimamizi na uongozi wa Profesa Heikki Lyytinen.

Japokuwa mchezo wa GrafoGemu ulianza katika lugha ya Kifini (ukiitwa Ekapeli), hadi sasa mchezo huu umeweza kutengenezwa katika lugha mbalimbali kama vile Kiingereza, Kispaniola, Kijerumani, Kiswidi, Kichile, Kifaransa, Kichina na kadhalika.

Kwa lugha za Afrika, mchezo wa Grafogemu unapatikana katika lugha za Chinyanja, Chibemba, Kikuyu, Kiafrikana, na Kiswahili (GrafoGemu-Kiswahili au GG-Kiswahili unaotumika Tanzania na Kenya).

Utayarishaji wa toleo la GG-Kiswahili ulifanywa na Mtaalamu na Mtafiti wa stadi za kujifunza kusoma kutoka Tanzania Dk. Stella-Damaris Ngorosho wa SEKOMU, akishirikiana na mtaalamu mwenzake kutoka Kenya, Dk. Carol-Suzanne Adhiambo Puhakka.

Wataalamu hawa walizingatia maudhui yaliyo kwenye vitabu vinavyotumika kufundishia Somo la Kiswahili kwa watoto wa shule za msingi za serikali za Tanzania.

Mtaalamu na mtafiti kutoka Tanzania aliingiza sauti za herufi, silabi na maneno ya Kiswahili kwenye maabara ya Chuo Kikuu cha Jyväskylä. Mchezo huu hauuzwi bali ni mwalimu wa ziada kwa watoto ambao bado wana changamoto ya kujua kusoma.

Hata hivyo, GG-Kiswahili hupatikana kwa ruhusa rasmi ya kuwekewa kwenye simu ya mkononi au kompyuta ya kiganjani (Tablet) kwa ajili ya manufaa ya watoto wengi.

 

GrafoGemu inavyofanya kazi

Mchezo wa GrafoGemu umejengwa katika mfumo unao-oanisha sauti na herufi (letter-sound correspondence). Kimsingi, mchezo wa GrafoGemu ni muhimu katika kujenga stadi muhimu za kujifunza kusoma kwa sababu mchezo huu unalenga kumjengea mtoto stadi za kutambua kwanza sauti katika lugha anayojifunzia kusoma na kuandika katika madarasa ya mwanzoni katika shule ya msingi.

Sauti husikika kupitia kiwambo kabla ya herufi, silabi au neno kutokea kwenye kioo cha simu au kompyuta. Anachotakiwa mtoto au mtu anayejifunza kusoma, ni kuchagua herufi, silabi au neno kati ya herufi/silabi/maneno yatakayokuwa yameorodheshwa (distractors).

Akichagua kwa usahihi, rangi ya kijani hutokea; akikosea, basi, rangi nyekundu hutokea. Kile kilichokuwa sahihi hubakia kwenye kioo ili akitambue anayejifunza.Hata hivyo, kitarudiwa tena ili kuona kama amekitambua. Baada ya muda, kile atakachokuwa alikosea, kitarudiwa kwa mara nyingine hata kama alishajua kukisoma. Lengo ni kumjengea umbo la herufi/silabi/neno katika kumbukumbu. Mtoto akishatambua sauti za lugha kwa usahihi, mchezo wa GrafoGemu huendelea kumpatia ujuzi wa kuunda silabi, maneno na baadaye sentensi fupi.

 

Faida za GrafoGemu-Kiswahili kwa mtoto, mwalimu na wadau wengine wa elimu

Kwanza, GG-Kiswahili ni mchezo rafiki kwa mtoto kwani mchezo huu umetengenezwa kwa namna ambayo herufi zilizojengwa katika mchezo zimeambatanishwa na picha zinazomfanya mtoto kupenda kuucheza bila kuchoka. Kila kipengele kilichorodheshwa kimeabatanishwa na picha ili anayejifunza anapokigusa tu, ile picha ibadilike rangi (kijani 0 kama amepata, au nyekundu kama amekosa).

Pili, GG-Kiswahili humwezesha mtoto kucheza bila msaada mkubwa wa mtu mwingine kwani mtoto husikia sauti na maelekezo kutoka kwenye kifaa anachotumia kupitia kiwambo cha sauti anachokuwa amekivaa masikioni.

Kila hatua ya mchezo huzingatia uwezo binafsi wa mtoto – yaani kadri mtoto anavyoonesha kuelewa kusoma iwe ni kwa haraka au taratibu. Mtoto atakayejua kusoma baada ya muda mfupi, mchezo humpeleka hatua ya mbele kama vile kuunda silabi au maneno.

Lakini kwa mtoto anayeelewa taratibu, au anayekosea kuchagua jibu sahihi, mchezo humpeleka hatua rahisi kwake (humrudisha nyuma kwenye hatua rahisi) ili asifanye makosa mengi yatakayomkatisha tamaa. Lakini hatimaye watoto wote hupitia hatua zote za mchezo na kuweza kujua kusoma.

Mara zote mtoto au mtu anapocheza, taarifa kuhusu uwezo wa kusoma huhifadhiwa kwenye simu au kompyuta. Hivyo, inakuwa rahisi kwa mwalimu, mtafiti au mdau mwingine wa elimu, kufuatilia maendeleo ya mtoto ya kujua kusoma. Taarifa hizo humwezesha mwalimu kutambua herufi, silabi au maneno yaliyompa mtoto au mtu changamoto ya kujua kusoma na hivyo kuwa rahisi kwa malimu kuandaa mazoezi zaidi ya kusoma kulingana na uwezo na changamoto alizoonesha mwanafunzi.

Aidha, taarifa muhimu hupatikana kwa ajili ya tafiti kuhusu watoto wanavyojifunza kusoma kwani simu au kompyuta ya kiganjani huhifadhi maendeleo ya kila mtoto.

 

SEKOMU kama msimamizi mkuu wa shughuli za GrafoGemu Tanzania

Chuo cha SEKOMU kina Mkataba wa Maridhiano (MoA) na Agora Centre chini ya Chuo Kikuu cha Jyaskyla kwa hiyo kina kibali cha kutumia GG-Kiswahili kwa shuguli za utafiti na kuendeshea mafunzo.

Tangu mwanzo Chuo kiliweka mkazo wa kuandaa wataalamu wa kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto kwenye maeneo mbali mbali pamoja na kujua kusoma na kuandika.

Mchezo wa GG-Kiswahili uliingizwa nchini kwa mara ya kwanza na Dkt. Ngorosho mwaka 2012 kupitia shule za msingi Majengo na Kizuiani, zote za Bagamoyo mjini kama utafiti wa majaribio. Lengo la utafiti huo ilikuwa kuona kama GG-Kiswahili inaweza kutumika na watoto katika mazingira ya shule za msingi za Tanzania.

Hadi sasa mchezo huu umeshatumika katika Shule za Msingi 11 katika wilaya za Bagamoyo na Lushoto. Walengwa wamekuwa ni watoto wa darasa la kwanza waliobainika kuwa walikuwa hawajaweza kusoma hata baada ya kujifunza kusoma kwa muda wa miezi mitano.

Matokeo yameonesha kuwa 97% ya watoto wote waliojifunza kusoma kupitia GG-Kiswahili waliweza kusoma hadi kiwango cha kusoma na kuandika sentensi ndani ya wiki tatu tu.

Vilevile mchezo huu umetumika kufundishia watu wazima kusoma na kuandika katika kituo cha Elimu ya Watu Wazima kilichoko katika kijiji cha Kwemshai-Kibohelo, Lushoto vijijini. Matokeo ya kujifunza kusoma kwa watu wazima kupitia GG-Kiswahili yalionesha kuwa, wote walioorodheshwa na kuhudhuria masomo walijua kusoma hadi maneno yenye silabi mbili au tatu kama vile bibi, mtu, meza, nafaka, waziri, sakafu, darubini, n.k baada ya kujifunza kusoma kwa mwezi mmoja.

Kutokana na matokeo chanya yaliyokwishapatikana, SEKOMU imekusudia kuchukua juhudi za makususdi za kuueneza katika shule zote za msingi nchini Tanzania kwa kushirikisha Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo, Halmashauri za wilaya, miji na manispaa, na ofisi za elimu. Kwa kuonesha nia thabiti, SEKOMU wameanza kuratibu shughuli zote za GrafoGemu-Kiswahili kupitia Senta ya Kuinua Kiwango cha Kusoma na Kuandika Tanzania – CEPROLITA.

SEKOMU imeshawafundisha na kuwaandaa wataalamu 16 waliobobea katika kutumia na kusimamia matumizi ya GG-Kiswahili. Majukumu ya wataalamu hao ni kuwafundisha na kuwatayarisha wanachuo wa Shahada ya Uzamili wanaosoma SEKOMU ambao wamehitimu kusimamia, kukagua, na kutumia GrafoGemu-Kiswahili katika kuwafundisha watoto na walimu wanaofundisha darasa la kwanza katika shule zilizoko kwenye zoezi la kujifunza kusoma kwa kutumia GrafoGemu-Kiswahili.

Wataalamu hao wanapatikana SEKOMU (ambako pia kuna Kitivo cha Kuinua Kiwango cha Kusoma na Kuandika Tanzania – CEPROLITA), katika ofisi za elimu wilaya, kata na katika shule za msingi ambako GG-Kiswahili imetumika.

Ni kutokana na mafanikio haya ndiyo sababu teknolojia hii ya GG-Kiswahili imeingizwa pia katika tafiti kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili. Katika mwaka wa masomo wa 2016, wanachuo watatu (3) walifanya tafiti kama sehemu ya kuhitimu shahada yao ya uzamili.

Tafiti hizo zilihusu ufanisi wa kutumia GG-Kiswahili kufundishia kusoma watoto wa darasa la kwanza pamoja na watu wazima. Shule zilizohusika katika tafiti zilikuwa Shukilai, Mabughai, Mkuzi, Kwebalasa na kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Kwemishai, Kibohelo, Lushoto Vijijini.

 

Faida ya GrafoGemu-Kiswahili kwa wadau wa elimu

Mara zote mtoto au mtu anapocheza, taarifa kuhusu uwezo wa kusoma huhifadhiwa kwenye simu au kompyuta. Hivyo, inakuwa rahisi kwa mwalimu kufuatilia maendeleo ya mtoto ya kujua kusoma. Pia mwalimu huweza kutambua herufi, silabi au maneno yaliyompa mtoto au mtu changamoto ya kujua kusoma.

Aidha taarifa muhimu kwa ajili ya tafiti kuhusu watoto wanavyojifunza kusoma huweza kupatikana kwani imu au kompyuta kiganjani huhifadhi kumbukumbu kuhusu maendeleo ya kila mtoto.

Ili kudumisha uwezo wa kusoma kwa watoto ambao wameshajenga stadi sahihi za kujifunza kusoma, walimu wanaofundisha darasa la kwanza na maafisa wa elimu katika wilaya, wamejifunza kutumia Grafogemu Kiswahili kupitia kompyuta ya kiganjani (Tablets) ili kujifunza mbinu bora na ya ziada ya kufundishia kusoma Kiswahili na hasa kwa kutumia njia ya kifonetiki (synthetic phonetic approach).

Hii ndiyo mbinu na njia sahihi na inayokubalika kufundishia lugha zanye tahajia uwazi (transparent orthography) kama Kiswahili. Wadau hawa wanafundishwa pia jinsi ya kuutumia mchezo kutambua herufi, silabi na maneno yanayompa mtoto changamoto ya kujua kusoma.

Halikadhalika, wamefundishwa jinsi ya kuandaa hadithi, nyimbo, vitendawili, na misemo ili kudumisha uwezo wa kusoma ambao watoto wanakuwa wameshajenga. Mpango huu wa uandishi wa hadithi fupi fupi umehusisha pia wanafunzi wa darasa la sita au darasa la saba kwenye baadhi ya shule za msingi Lushoto mjini kama vile Shule ya Msingi Kitopeni.

Afisa Mdhibiti Mkuu wa Ubora wa Elimu wa Wilaya, A. Mosha alianzisha mpango huo wa utunzi wa hadithi shuleni hapo akishirikiana na walimu wa Kiswahili wa shule ya Kitopeni na kwa sasa wanafunzi wa darasa la tano na la sita wanavyo vijitabu vidogo vidogo vyenye hadithi, nyimbo na ngonjera vinavyoweza kusomwa na watoto wa darasa la 1 hadi la 3.

 

Ushirikishwaji wa wazazi katika juhudi za kuinua kiwango cha kujua kusoma na kuandika

SEKOMU na shule zote ambako GrafoGemu-Kiswahili kimetumika, wazazi na walezi wa watoto walio kwenye mradi wa kujifunza kwa kutumia GG-Kiswahili wanaruhusiwa kukagua na kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanapokuwa katika kipindi cha kujifunza kusoma.

Madhumuni ya ushirikishwaji wa wazazi ni kueneza taarifa kuhusu uwezekano wa watoto ambao walifikiriwa kuwa na changamoto ya kutojua kusoma na kuandika kabisa kuwa wanaweza kusaidiwa kupitia teknolojia rahisi na bora ya GG-Kiswahili ambayo hutolewa bure kupitia shuleni au katika kituo cha kujifunzia kusoma.

Kinachotakiwa ni upatikanaji wa vifaa vya kupakulia mchezo wenyewe ambavyo ni simu za kupangusa (Smart Phones) au kompyuta za kiganjani (Tablets). Shule au wazazi wanaweza kushirikishana wakapata vifaa hivyo ambavyo vitakuwa ni mali ya shule ili watoto wengi wenye uhitaji wa kujifunza kusoma kupitia GG-Kiswahili waweze kunufaika.

 

Kwa taarifa zaidi kuhusu uendeshaji wa shughuli zinazohusiana na GrafoGemu-Kiswahili wasiliana na:

Mratibu wa shughuli za GrafoGemu Tanzania kupitia: sngorosho@yahoo.com au kwa simu ya kiganjani: +255754316339

Au tembelea tovuti zifuatazo: http://www.graphogame.com; http://www.CeProlita.co.tz; au fuatilia kiungo cha GraphoGame Kiswahili Tanzania kwenye http://www.youtube.com.

1718 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!