MOSHI 
 
CHARLES NDAGULLA

Eneo la Njiapanda katika Mji Mdogo wa Himo, mkoani Kilimanjaro linalosifika kuwa kitovu cha biashara ya magendo, hasa mahindi, yanayosafrishwa kwenda nje ya nchi kwa njia za panya, sasa limeongezewa sifa nyingine.
 
Sifa hii ya pili ni utapeli wa viwanja unaosimamiwa na watendaji wa serikali akiwamo Afisa Mtendaji wa Kata ya Njiapanda, Humphrey Kimath ambaye amekuwa akibariki uuzwaji wa viwanja vyenye hati miliki.
 
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa, mtendaji huyo wa kata amejipa jukumu la kusimamia na kuidhinisha uuzwaji wa viwanja akitumia nyaraka za serikali ukiwamo mhuri bila kuzingatia sheria na kuibua migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima.
 
Katika tukio la hivi karibini, mtendaji huyo amesimamia kuuzwa kwa kiwanja namba 1254 Block F kilichopo ndani ya kata yake kinachodaiwa kumilikiwa kihalali na Severine Kazyarua Moshi mwenye  anuwani ya posta 7805, Moshi.
 
Nyaraka ambazo JAMHURI linazo zinaonyesha kuwa kiwanja hicho kilimilikishwa kihalali kwa Mosha kwa barua ya toleo ya muda mrefu (Letter of Offer) ya miaka 33 kwa kumbukumbu namba, MS/254777/1 ya Februari 22 mwaka 1990.
 
Pamoja na nyaraka kuonyesha umiliki wa kiwanja hicho, Mei 16 mwaka huu, mtendaji huyo anadaiwa kusimamia mauzo haramu ya kiwanja hicho uliofanywa na mtu aliyetambuliwa kwa jina la Wilbard Fidelis Mchau.
 
“Mimi Willbard Fidelis Mchau…… muuzaji, ninatamka kwamba kiwanja hiki ni mali yangu halali na kwamba hakina mgogoro au madai na mtu yeyote, endapo kiwanja hiki kitakuwa na mgogoro ndani ya miaka mitano, mnunuzi anijulishe nitafika kuutatua bila gharama zozote kutoka kwa mununzi,” linaeleza tamko la muuzaji.
 
Mchau aliuza kiwanja hicho kwa Sh. milioni 9  kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Joseph Charles Kimaro na mtendaji huyo kubariki uuzwaji huo kwa kutia saini yake na mhuri wa ofisi yake.
 
“Nathibitisha kwamba makubaliano ya muuzaji na mnunuaji kiwanja nimeyashuhudia hatua zote,” inasomeka sehemu ya maandishi ya mtendaji huyo yaliyopo kwenye hati ya makubaliano ya mauziano ya kiwanja yenye kichwa cha habari kisemacho udhibitisho wa ofisi.
 
JAMHURI limezungumza na Willbard Mchau kutaka kujua uhalali wa yeye kuuza kiwanja hicho na katika maelezo yake anadai kiwanja hicho alimilikishwa na baba yake mzazi Fidelis Mchau mwaka 1993.
 
Baada ya kupewa anadai aliamua kuuza eneo hilo ili apate fedha za ada kwa ajili ya mtoto wake na huku akidai ardhi yao ilipimwa na maofisa ardhi na kuuziwa watu bila wao kushirikishwa.
 
“Ni eneo langu halali nilipewa na baba yangu mzazi mzee Fidelis, sijauza eneo la mtu na hao maofisa ardhi walipima ardhi yetu na kuwapa watu bila kujali kama kuna wazawa waliokuwa wakiishi hapo,” amesema.
 
Kwa upande wake Joseph Kimaro anayedaiwa kuuziwa eneo hilo amesema anayelalamikia kiwanja hicho kuuzwa aende mahakamani ambako alidai huko ndiko haki itapatikana.
 
“Haki inapatikana mahamakani siyo mitaani, kama anaona amedhulumiwa haki yake aende huko mahakamani ndiyo itakayoamua ni nani mwenye haki ya kumiliki hicho kiwanja,” amesema.
Ofisa Mtendaji Kata ya Njiapanda, Humphrey Solomon Kimathi amekiri kuhusika kusimamia uuzwaji wa kiwanja hicho alipobanwa na kudai kuwa muuzaji wa kiwanja hicho alitoa taarifa za uongo juu ya uhalali wa yeye kuwa mmiliki wa kiwanja hicho.
 
Baada ya kubaini kuwepo na udanganyifu huo aliamuru muuzaji akamtwe na kupelekwa kituo cha polisi Himo kwa mahojiano huku akidai kusitisha shughuli za ujenzi zilizokuwa zikiendelea kwenye kiwanja hicho.
 
 
Naye mmiliki wa kiwanja hicho, Severine Mosha, amedai kuwa Julai 8, mwaka huu alifika kwenye kiwanja chake kwa ajili ya kuendelea na ujenzi lakini alikuta kimevamiwa na kujengwa ukuta huku akidai kuhakiribiwa kwa miti yake iliyokuwa ndani ya kiwanja.
 
Baada ya kushuhudia uvamizi huo aliwasilisha malalamiko yake ofisi ya ardhi kwenye mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo na kuwasilisha nyaraka za umiliki wa kiwanja hicho.
 
Amesema aliongozana na Ofisa Ardhi katika mamlaka hiyo ya Mji Mdogo hadi eneo la tukio ambako shughuli za ujenzi wa uzio zilikuwa zikiendelea na kuagiza mafundi waliokuwa wakiendelea na ujenzi kuwasiliana na bosi wao kwa ajili ya mahojiano.
 
Hata hivyo,  Mosha amelalamikia mchezo mchafu uliofanywa na ofisa ardhi huyo aliyetajwa kwa jina la William Msewe ambaye badala ya kusimamisha shughuli za ujenzi wa uzio, anadaiwa kubariki kuendelea kwa shughuli hizo.
 
Msewe alipotafutwa hakuwa tayari kujibu tuhuma hizo na kutaka mwandishi awasiliane na mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na kwamba yupo tayari kuzungumza endapo mwandishi atapata kibali kutoka kwa mwajiri wake.
“Mimi siyo msemaji wa halmashauri, msemaji ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya naomba taratibu zifuatwe  na kama atakupa kibali niko tayari kuzungumza,”amesema ofisa huyo.
 
Kutokana na hali hiyo, Mosha amewasilisha malalamiko Ofisi ya Mkururenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi akiiomba ifuatilie mgogoro  wa kuvamiwa kwa kiwanja chake ili awe huru kuendelea na ujenzi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo Ndalahwa, amesema ofisi ya ardhi wilaya inamtambua Severine Mosha kuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho na si vinginevyo.
“Huyo anayedai kiwanja ni chake awasilishe nyaraka kuonyesha uhalali wa umiliki wa kiwnaja hicho na sisi kama halmashauri tuko tayari kumsadia mwenye kiwanja halali kupata haki yake,” alisema.
 
Katika hatua nyingine,  Ofisi ya Ardhi Wilaya ya Moshi, imetoa onyo kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Njiapanda kuwa makini na watu wanouza viwanja ndani ya kata hiyo kuepusha mogogoro isiyokuwa ya lazima.
 
Kwa mujibu wa barua ya Juni 8, mwaka huu yenye kumbu kumbu namba MS/LD/25477/06 iliyosainiwa na Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, C. Mwing’uri, pamoja na onyo hilo inamtaka mtendaji kumjulisha aliyeuziwa kiwanja hicho kuwa si mmiliki wa kiwanja hicho.
 
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo nakala yake tunayo, mtendaji anaonywa kuwa umilikishwaji wa kiwanja hicho haukufanyika kwa kuwa kulingana na kumbukumbu zilizopo ofisi ya ardhi, kiwanja hicho kilikwishamilikishwa kwa barua ya toleo la muda mrefu.
 
Barua hiyo inaeleza kuwa, kuanzia Januari mosi  mwaka 1990 mmiliki wa kiwanja hicho amekuwa akilipia kodi ya pango la ardhi kwa miaka yote tangu amilikishwe na kumtaka anayedai kumiliki kiwanja hicho awasilishe nyaraka zake halali za umiliki ikiwamo barua ya toleo.
 
“Tayari imethibitika mauzo ya kiwanja ambapo muuzaji hana haki ya kiwanja hicho, hivyo kwa barua hii unapaswa kuwa makini sana na taarifa unazotoa kwani utasababisha migogoro mingi pamoja na double allocation kama hii uliofanya kupitia barua yako ya utambulisho [si sahihi],“ inaonya barua hiyo.
 
Barua hiyo inakuja siku chache baada ya ofisa mtendaji huyo kuiandikia barua ofisi ya ardhi wilaya yenye kumbukumbu Na. NJP/KT/8/2/35/VOL.V/310 ya  Mei 22 mwaka huu ikimtambulisha Joseph Charles Kimaro kuwa mmiliki wa kiwanja hicho .

By Jamhuri