Jumla ya watu 314 wamepata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichomalizika hivi karibuni mjini Njombe ambacho kiliandaliwa na Idara ya Habari – Maelezo.

Huduma hizo zilitolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa lengo la kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kupitia kampeni ya “Jua Namba Zako”.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo Daktari wa JKCI, Samweli Mbilinyi alisema kati ya wananchi waliopimwa watu 201 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi huku 37 wakipewa rufaa ya kwenda kupata matibabu ya kibingwa katika Taasisi hiyo.

“Kati ya watu tuliowafanyia uchunguzi wagonjwa 37 walibainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo ambayo ni kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo yaliyohitaji uchunguzi zaidi pamoja na matibabu ya kibingwa JKCI”, alisema Dkt. Mbilinyi.

Alisema upimaji huo umebaini wananchi wengi bado hawajazoea kupima afya zao mara kwa mara jambo linalochangia baadhi yao kuendelea kuishi na matatizo ya moyo bila kujitambua.

Dkt. Mbilinyi aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, kula lishe bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya tumbaku pamoja na unywaji wa pombe kupita kiasi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

“Ninatoa wito kwa wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula chakula bora na kuacha matumizi ya tumbaku pamoja na unywaji wa pombe uliopitiliza ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo”, alisema.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Maelezo Zamaradi Kawawa alisema kila mwaka wanapofanya kikao hicho hufanya kambi ya upimaji wa magonjwa mbalimbali kwa kushirikiana na JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi wa afya.

“Utaratibu huu tunaufanya kila mwaka kwa nia ya kurudisha kwa jamii kwa kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi wa afya kutoka kwa wataalamu wetu wanaotoa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa mbalimbali”, alisema Zamaradi.

Baadhi ya wananchi waliopata huduma hizo waliishukuru JKCI pamoja na taasisi nyingine za afya kwa kuwafikishia huduma za kibingwa karibu na maeneo yao huku wakisema zimewasaidia kutambua hali zao za afya mapema na kupunguza gharama za kusafiri kwenda Dar es Salaam kwaajili ya matibabu.

Anna Mligo ambaye ni Mkazi wa Njombe Mjini alisema alikuwa akisumbuliwa na mapigo ya moyo kwenda mbio pamoja na uchovu wa mara kwa mara lakini hakuwahi kufanyiwa uchunguzi wa moyo hadi alipofika katika huduma hizo.

“Nilikuwa najisikia kuchoka sana na moyo kwenda kasi mara kwa mara lakini sikuwa najua tatizo ni nini. Leo nimepata vipimo na ushauri kutoka kwa madaktari bingwa jambo ambalo limenipa matumaini makubwa ya afya yangu”, alisema Anna.

Naye John Mwakipesile kutoka Makambako alisema huduma zilizotolewa na JKCI zimewasaidia wananchi wengi kupata elimu ya afya ya moyo pamoja na kutambua umuhimu wa kupima afya mara kwa mara.

“Hizi huduma zimetusaidia sana sisi wananchi wa kawaida ambao wakati mwingine tunashindwa kufika hospitali kubwa kwa sababu ya gharama. Tunaiomba JKCI iendelee kwenda mikoani mara kwa mara ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hii”, alisema John.

Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Modesta Nyagawa akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Revocatus William ambaye ni Mfanyakazi wa Wizara ya Ardhi wakati wa zoezi la uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali lililofanyika katika Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo mjini Njombe.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Mbilinyi akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa Fakii Mjaka ambaye ni Afisa Habari kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa zoezi la upimaji afya lililofanyika hivi karibuni katika Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo mjini Njombe.