Benki ya CRDB Bank Plc imeendesha droo ya pili ya kampeni yake ya FIFA World Cup 2026 – “Fainali Ndiyo Mpango na Tembo Card Visa”, ikiwapa wateja nafasi ya kujishindia safari ya kwenda kushuhudia fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico.
Katika droo hiyo, mtoto wa Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere, Charles Makongoro Nyerere, ametajwa miongoni mwa washindi watatu waliojishindia safari ya kwenda nchini Canada kushuhudia michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.
Makongoro aliungana na mfanyabiashara maarufu Arun Lodhia pamoja na Abdulraouf Suleiman, ambao wote wameibuka washindi wa safari hiyo ya kihistoria.
Baada ya kupigiwa simu kuthibitishiwa ushindi wake, Makongoro alijibu kwa kifupi akisema, “Asante sana.”
Mbali na zawadi za safari, droo hiyo pia iliwapatia washindi wengine televisheni za kisasa aina ya Janja TV 85 inch. Washindi hao ni Arina Kaswala, Lusekelo Michael na Easter Kabakama.
Akizungumza wakati wa droo hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Karington Chahe alisema kampeni hiyo imeendelea kuwapa wateja wa benki hiyo nafasi ya kutimiza ndoto ya kushuhudia Kombe la Dunia 2026 kupitia matumizi ya Tembo Visa Card.
Alisema droo hiyo inatarajiwa kuhitimishwa hivi karibuni na kuwahimiza wateja wa CRDB kuendelea kufanya miamala na kulipa bili mbalimbali kwa kutumia Tembo Visa Card ili kuongeza nafasi za kushinda zawadi mbalimbali zinazotolewa katika kampeni hiyo.




