Wananchi wa Wilaya ya mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, wameiomba Baraza la Wawakilishi kuangalia upya sheria zinazohusu makosa ya udhalilishaji wa kijinsia, wakidai kuwa katika baadhi ya mazingira watoto wa kiume hawapati haki sawa na wenzao wa kike.
Waliyasema hayo jana, Agosti 10, 2026, katika kijiji cha Kengeja wakati wa kikao cha kubadilishana mawazo kati ya wananchi na ujumbe wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ulioongozwa na Mnadhimu wa Baraza, Profesa Omar Fakih Hamad kupitia Chama cha ACT Wazalendo
Akizungumza katika kikao hicho, Bushra Abdallah Khamis alisema baadhi ya vifungu vya sheria vinahitaji kutazamwa upya ili kuondoa mianya inayoweza kusababisha matumizi mabaya ya sheria au vitendo vya rushwa.
Alidai kuwa katika baadhi ya matukio ya mahusiano yanayohusisha vijana wenye umri tofauti, mara nyingi anayechukuliwa hatua ni mtoto wa kiume pekee huku wa kike akiachwa bila hatua za kisheria.
Naye Abdulatif Muhammed wa Kengeja alisema iwapo sheria haitazingatia usawa kwa pande zote, inaweza kutoa nafasi ya kutumiwa vibaya kwa kutoa taarifa zisizo sahihi au kwa misingi ya visasi.
Kwa upande wake, Muhammed Khamis Juma alipendekeza elimu kuhusu sheria za udhalilishaji itolewe zaidi kwa vijana wa kiume ili kuwajengea uelewa wa wajibu wao na madhara ya makosa hayo.
Mbali na hilo, wananchi hao waliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuacha malumbano na vijembe visivyo na tija wanapokuwa wakijadili masuala ya wananchi.
Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu Wilaya ya Mkoani, Siti Suleyum Dadi, alisema wananchi wanatarajia Baraza kujadili masuala ya maendeleo badala ya mijadala isiyo na manufaa kwa taifa.
Katika kikao hicho pia wananchi walilalamikia huduma ya umeme kisiwani Pemba, wakisema kukatika kwa umeme bila taarifa kumekuwa kukisababisha uharibifu wa vifaa vya umeme ikiwemo televisheni na majokofu.
Muhammed Khamis Suleiman alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara kubwa kwa wananchi, huku akitaka pia kuondolewa kwa tozo ya huduma ya chaji ya umeme ambayo wananchi wanaona haina uhalali.
Kuhusu umiliki wa ardhi, wananchi walitaka sheria ifanyiwe marekebisho ili kuhakikisha wenye ardhi wanapata fidia stahiki pale ardhi zao zinapotwaliwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hata kama hazijajengwa.
“Haiwezekani ardhi niliyoirithi au kununua isilipwe fidia kwa sababu tu haijaendelezwa wakati inachukuliwa kwa matumizi ya umma,” alisema Abdulatif Muhammed Omar.
Katika sekta ya elimu, wananchi walipendekeza mfumo wa ajira za walimu urejeshwe chini ya Tume ya Utumishi wa Walimu badala ya utaratibu wa sasa.
Akihitimisha kikao hicho, Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi, Profesa Omar Fakih Hamad ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Pandani Wilaya ya6th wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema maoni yaliyotolewa yatawasaidia wajumbe kuyafikisha katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi kinachotarajiwa kuanza Septemba 9, 2026.
“Niwashukuru sana wananchi kwa kutoa maoni yenye maslahi mapana kwa Zanzibar. Hoja hizi zitatusaidia katika utekelezaji wa wajibu wetu wa uwakilishi,” alisema Profesa Fakih.
Miongoni mwa wajumbe walioshiriki kikao hicho walikuwa Dkt. Muhammed Ali Suleiman, Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Seif Hamad Suleiman Ole, na Dkt. Nasra Nassor, Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Unguja na Makamu Mwenyekiti wa umoja Wajumbe wa baraza hilo kwa upande wa wanawake, woote kutoka Chama cha ACT Wazalendo.
Mnadhimu huyo ameanza ziara hiyo leo ambapo akiwa na timu yake watawafikia wananchi wa Wilaya zoote 11 za Zanzibar na leo itakuwa zamau ya Wilaya ya Micheweni.


