Watu milioni 15.6 nchini Tanzania wamehama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Felchesmi Mramba, wakati wa Mdahalo wa Nishati Safi uliofanyika Agosti 11, 2026, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Mhandisi Mramba amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kuhakikisha Watanzania wanahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuongeza juhudi za kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu na manufaa ya kutumia nishati safi ya kupikia.
Vilevile, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ili iweze kupatikana kwa gharama nafuu ambazo wananchi wengi watamudu.
Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha nishati hiyo inasambaa na kupatikana kwa urahisi katika maeneo yote nchini, kwa kuzingatia aina ya nishati inayopatikana katika eneo husika.
“Serikali inasambaza nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mazingira na upatikanaji wa nishati katika eneo husika. Kwa mfano, maeneo ambayo gesi inapatikana kwa wingi yanapelekewa mitungi na majiko ya gesi, huku maeneo yenye umeme yakipelekewa majiko yanayotumia umeme,” amesema Mhandisi Mramba.
Sambamba na hilo, amesema juhudi zaidi zinaendelea kufanyika kuhakikisha wananchi wanapata teknolojia na mifumo rahisi na rafiki ya nishati safi ya kupikia ili kila mwananchi aweze kuitumia.






