📍NIRC Katavi
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekabidhi pampu 52 za umwagiliaji zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 500 kwa vikundi 46 vya wakulima mkoani Katavi, ikiwa ni hatua ya kuongeza tija, kupanua eneo linalolimwa na kuimarisha usalama wa chakula.
Hafla hiyo ya ugawaji imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ambapo mkoa huo umekuwa miongoni mwa wanufaika wa awamu ya kwanza ya mpango huo wa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji katika kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amewataka wanavikundi waliobainishwa kutoyabadilisha matumizi ya vifaa hivyo kwa kuanza kufyatua matofali badala ya kuzalisha mazao.
Buswelu amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuona wakulima wanaendesha kilimo kinachozingatia hifadhi na utunzaji wa mazingira badala ya kuchepusha au kuiziba mito.
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkurugenzi Mkuu Bw. Raymond Mndolwa ameeleza kuwa pampu hizo zimetengenezwa maalum kwa ajili ya maeneo yenye maji yanayotiririka na sio za visima.
Bw. Mndolwa ameongeza kuwa ili kulinda mazingira na kuzuia kilimo cha pembezoni mwa vyanzo vya maji, pampu hizo zimewekewa mipira yenye urefu wa zaidi ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji, mifereji au mabwawa, huku akiwasihi wakulima kuzitumia kwa ajili ya kilimo pekee na sio shughuli nyingine kama kufyatua matofali.
Akiwasilisha taarifa ya ya pampu hizo, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Katavi, Mha. Samson Bai, amesema pampu hizo zitasambazwa kwenye Halmashauri zote tano za mkoa huo na zinatarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji kwa takribani ekari 2,080.
Mhandisi Bai amebainisha kuwa kila pampu ina uwezo wa kusukuma maji kati ya mita za ujazo 80 hadi 100 kwa saa, hatua inayoiwezesha pampu moja kumwagilia hadi ekari 40 kwa siku, huku uwepo wa magurudumu ukiwezesha urahisi wa kuzihamisha kutoka eneo moja kwenda jingine.
Sambamba na hayo wakulima mkoani humo akiwemo Tausi Masudi
wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo muhimu katika kuinua kipato cha wakulima kupitia kilimo.
Amesema kuwa pampu hizo zitawaondolea adha ya kutumia majenereta ya zamani yaliyokuwa yakikwama mara kwa mara na kusababisha kero ya kuharibika kwa mipira.
Naye mkulima Chausiku Omary amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mashine hizo, akieleza kuwa zitawasaidia kulima mazao mbalimbali kama vile mboga mboga na mahindi, hatua itakayoinua uchumi wao na kuwawezesha kusomesha watoto.
Mkoa wa Katavi una jumla ya hekta 124,761 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo hadi sasa takribani hekta 110,672 zinaendelezwa kupitia skimu 29 za umwagiliaji zinazochangia uzalishaji wa mpunga, mahindi, maharage na mboga mboga.


















