Na. Josephine Majura na Asia Singano, WF- Dodoma
Serikali imesema uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika na kwamba uwekezaji katika sekta mbalimbali, hususani madini, gesi, nishati, kilimo na miundombinu, unatarajiwa kutoa msukumo mkubwa kwa ukuaji wa uchumi.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akifungua mkutano na wataalamu wa Kampuni ya Kimataifa ya Tathmini ya Madeni ya (Fitch Ratings), uliofanyika kwa njia ya mtandao, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kufanya mapitio ya hali ya uchumi wa Tanzania.
Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Mageuzi ya Kodi iliyoundwa na Serikali, jambo ambalo limeendelea kukuza uchumi wa nchi.
‘’Upande wa ukuaji wa uchumi tumetoka asilimia 5, mwaka mwaka 2024, tumekwenda asilimia 5.9 mwaka jana, mwaka huu tunategemea uchumi utakuwa kwa asilimia 6.3 hatujafikia viwango ambavyo vilikuwa kabla ya COVID 19 lakini tunaendelea vizuri’’ alisema Mhe. Balozi Omar.
Alisema kuwa, moja ya maeneo muhimu yaliyojadiliwa na Fitch ni maendeleo makubwa yanayoendelea katika sekta ya madini na uchakataji wa madini, huku akieleza kuwa Tanzania ina miradi mikubwa ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na ikitekelezwa itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi.
‘’Kuna miradi mingine mikubwa ukiwemo wa Nyanzaga wa uchimbaji wa dhahabu Mwanza ambao unatarajiwa kuwekeza zaidi ya dola milioni 500, kuna miradi mingine ambayo inaendelea upande wa aluminiam – Songea, Chuma- Liganga, Chuma -Dodoma, na miradi mingine kwa hiyo kwa ujumla kwenye sekta hii kuna uwekezaji mkubwa ambao unatarajiwa kuleta msukumo mkubwa katika uchumi wetu’’ Alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).
Aliongeza kuwa kwa ujumla sekta ya madini inaendelea kuwa na nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, hasa kutokana na ongezeko la uwekezaji unaotarajiwa katika uchimbaji na uchakataji wa madini hapa nchini.
Alisema Mradi mkubwa wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG), ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuleta msukumo mkubwa katika uchumi, pamoja na mradi wa madini ya niobium ambao tayari umesainiwa na unatarajiwa kuvutia uwekezaji wa takribani dola milioni 442.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza athari za mabadiliko ya bei za mafuta na bidhaa nyingine muhimu kwa kutumia sera na mifumo mbalimbali ya kiuchumi.
Kwa upande wa Fitch, majadiliano yaliongozwa na mchambuzi Mkuu anayeshughulikia Tanzania, Bw. José Mantero, ambapo majadiliano hayo yalilenga kuwapa wachambuzi hao fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, utekelezaji wa sera za kibajeti na fedha, pamoja na mikakati ya Serikali katika usimamizi wa deni la Taifa.
Aidha, wachambuzi hao walijikita katika kutathmini athari za vita kati ya Iran katika uchumi wa Tanzania, hususan mwenendo wa bei za mafuta na mbolea, pamoja na hatua na mikakati inayochukuliwa na Serikali kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Kamishna Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Nuru Ndile, kwa njia ya mtandao.





