Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaan
WANAFUNZI zaidi ya 50 wa shule ya Sekondari Keko ,wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa mbolea mboji kwa kutumia taka za majumbani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea ujuzi wa utunzaji wa mazingira na
kuwawezesha kujiajiri kupitia kilimo.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika Shirika la Active African Women in Research and Development (AAWORD), wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, yakilenga kuwafundisha wanafunzi namna ya kutumia mabaki ya
vyakula na taka nyingine zinazoweza kuoza kutengeneza mbolea asilia isiyokuwa na kemikali.
Akizungumza na Jamhuri, Mkurugenzi wa shirika hilo Idda Swai amesema wameamua kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuthamini taka za majumbani na kuzitumia katika uzalishaji wa mboji kwa ajili ya kilimo.
Amesema utengenezaji wa mbolea mboji una faida mbalimbali, ikiwemo kuboresha mazingira, kupunguza taka katika jamii, kuongeza rutuba ya udongo na kusaidia ukuaji wa mazao.
“Lengo letu ni kuwafundisha wanafunzi kutumia vitu vinavyopatikana katika mazingira yao na kuvigeuza kuwa bidhaa yenye manufaa. Mbolea hii inaweza kutumika katika kilimo na pia kuuzwa, hivyo kuwa chanzo cha kipato,” amesema Idda.
Mbali na mafunzo ya utengenezaji wa mboji, wanafunzi hao pia wamefundishwa namna ya kutengeneza vitalu na kupanda mbegu za aina mbalimbali za mboga.
Kwa mujibu wa Idda, ujuzi huo utawasaidia wanafunzi kuanzisha vitalu shuleni kama walivyofundishwa sambamba na kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika jamii zao huku wakijiongeze kipato kupitia mbolea asilia.
Amesema hatua hiyo pia ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwajengea vijana uelewa wa namna ya kutumia taka zinazozalishwa majumbani kwa manufaa badala ya kuzitupa ovyo.
Kwa upande wake, Mwalimu Rushubilwa Robert amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanafunzi kutokana na umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya mbolea salama katika kilimo.
Amesema shule itaweza kutumia ujuzi huo waliopata wanafunzi kutengeneza mbolea kwa ajili ya bustani za maua na kilimo cha mboga mboga, jambo litakalosaidia pia katika utunzaji wa mazingira .
“Ni muhimu wanafunzi kupata ujuzi wa aina hii kwa sababu wanaweza kuutumia wakiwa shuleni na wanaporudi nyumbani,wanaweza kutengeneza mbolea kwa matumizi yao au kuuza na kujipatia kipato,” amesema.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Tausi Mlela, amesema amekuwa akitoa elimu kwa wanafunzi, wajasiriamali na wanawake waliopo katika vikundi kuhusu utengenezaji wa mbolea asilia kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwa
urahisi.
Amesema mbolea hiyo hutengenezwa kwa kuchanganya mabaki ya vyakula,mkaa, samadi na mabaki mengine yanayoweza kuoza ambapo baada ya mchnganyiko huo inazalisha faiada kubwa kwa jamii.
“Mbolea ya asili isiyokuwa na kemikali ndiyo ninayofundisha. Pia nawafundisha kutengeneza vitalu vya mboga ili waweze kulima wakiwa majumbani na kujipatia kipato,” amesema Mlela.
Amehamasisha wanawake na vijana kutumia fursa za mafunzo wanazopata na kuzifanyia kazi ili waweze kujipatia kipato badala ya kubaki na ujuzi bila kuutumia ili kujikwamua kiuchumia
Mlela amesema mwanafunzi anapopata ujuzi na kwenda nyumbani kuutumia, anaweza kuanzisha uzalishaji wa mbolea na baadaye kuuza, hivyo kujengauwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Mwanafunzi Sabrina Miraji amesema mafunzo hayo yamempa ujuzi wa kutengeneza mbolea isiyokuwa na kemikali, akieleza kuwa ujuzi huo utamsaidia kujiongezea kipato.
Taliq Juma amesema mafunzo hayo aliyoyapata ni muhimu kwa vijana kwa sababu yanawapa fursa ya kujifunza namna ya kujiajiri kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira yao.
Amesema vijana wanapaswa kuwa na uthubutu wa kutumia mafunzo wanayopata kwa vitendo na kubuni njia mbalimbali za kuzalisha mbolea asilia, ambayo mahitaji yake yanaongezeka kutokana na umuhimu wa kilimo salama ndani na nje ya nchi.





