Na Mwandishi Wetu
Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeendelea kuimarisha uwezo wa kitaalamu na utafiti katika masuala yanayohusu bioanuai, pamoja na kujenga na kuimarisha mfumo thabiti wa kisheria na utawala ili kuwezesha uhifadhi na matumizi ya rasilimali za bioanuaii nchini kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu mkakati na mpango kazi wa Taifa wa hifadhi ya bioanuai, taarifa aliyoiwasilisha Bungeni Agosti 11, 2026.
Amesema, wadau mbalimbali zikiwemo Wizara za Kisekta, Taasisi za serikali na zisizo za serikali, makampuni binafsi, wadau wa Maendeleo na makundi ya Kijamii, huhitajika kuutekeleza mkakati huu.
“Mkakati huu hutekelezwa kwa kuhuisha masuala ya bioanuai kwenye mipango ya kisekta, ikiwemo Kuandaa programu maalumu ya hifadhi ya bioanuai kwa sekta husika, pamoja na kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu hifadhi ya bioanuai.”
Utekelezaji wa Mkakati huu unachangia utekelezaji wa mikakati mingine ya Mazingira ikiwemo; Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), Sera na Mkakati wa Uchumi wa Buluu (2024).
“Matokeo ya utekelezaji wa Mkakati huu utachangia katika kuimiarisha hali ya uhifadhi wa mazingira nchini kufikia asilimia 25 na kufanya jumla ya asilimia 65 ya uhifadhi nchini ifikapo mwaka 2030.
“Kiasi hicho kitachangia nguzo ya tatu ya Dira 2050 katika eneo la hifadhi ya bioanuai ambapo tunatarajia kwamba ifikapo mwaka 2050 Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi kumi (10) bora Afrika katika kuhifadhi mazingira.”
Mkakati wa Taifa wa bioanuai (2025-2030) umeshirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa uaandaji wake. Wadau hao ni pamoja na Wizara za kisekta; Taasisi za serikali na zisizo za serikali; na Makundi ya jamii.
Mkakati na Mpangokazi wa Kitaifa wa Bioanuwai (2025 2030) ni mwongozo wa kitaifa unaotoa mwelekeo na umeainisha mikakati ya inayopaswa kutekeleza ili kuwezesha uhifadhi na matumizi ya rasilimali za bioanuaii nchini kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Jackson Kiswaga amesema kwa kutambua kuwa suala la mazingira ni mtambuka, Ofisi ya Makamu wa Rais iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha programu ya elimu kwa umma kuhusu mazingira inawafikia wadau wengi zaidi.




