Wiki iliyopita nimepata msukosuko. Haukuishia kwangu tu, bali hata wafanyakazi wenzangu – Edmund Mihale na Manyerere Jackton – nao yamewakuta sawa na yaliyonikuta mimi. Jumatano ya Julai 17, 2013 nilipokea simu ya wito kutoka Polisi Makao Makuu, Dar es Salaam.

Naibu Kamishna wa Polisi alinipigia simu akinitaka nifike kwa mazungumzo. Alinieleza kiungwana tu, kuwa angependa tuzungumzie habari tuliyoichapisha katika toleo Na. 91 iliyokuwa na kichwa cha habari ‘UFISADI UJIO WA MARAIS’. Niliitikia wito na kufika polisi saa 5:30 asubuhi. Nilikaa pale hadi saa 8:30 mchana.

 

Nilipofika nilikuta jopo la wataalamu. Alikuwapo Mwanasheria wa Ikulu, Afisa Mwandamizi wa Ikulu, Inspekta Msaidizi wa Polisi na maafisa upelelezi watatu ndani ya chumba kile. Mimi nilisindikizwa na Manyerere. Tulianza mazungumzo na baada ya kuanza tu, Mwanasheria wa Ikulu akaniambia mambo mawili.

 

Jambo la kwanza alitaka kujua nani aliyenipa taarifa za ufujaji wa fedha katika Mkutano wa Smart Partnership, lakini la pili alitaka kujua kwa nini gazeti JAMHURI lilifikia uamuzi wa kuchapisha barua yenye mhuri wa SIRI. Nilimjibu kiungwana tu, kuwa suala la nani aliyenipa taarifa asipoteze muda maana sitamwambia.

 

Nilisema sitamtaja leo, kesho, keshokutwa au hata siku nikiwa gerezani au mbinguni. Nilimweleza kuwa sawa na polisi wasivyoruhusiwa kutaja watoa taarifa wao unapotokea uhalifu, vivyo hivyo wanahabari hawaruhusiwi kutaja vyanzo vyao milele. Namshukuru alinielewa na hakuendelea kuuliza swali hilo.

 

Mjadala mpana ulijikita juu ya kwa nini tumechapisha barua ya siri. Kwanza nilimwambia mhuri wa ‘Siri’ unatumiwa vibaya. Barua tuliyoichapisha iliyokuwa imegongwa mhuri huo ni ya mwaliko kwa wajumbe kwenda kwenye mkutano wa kujadili mipango mbalimbali ya mkutano wa Smart Partnership. Haina zaidi ya hapo.

 

Sitanii, msomaji fikiria. Barua ya kuita mtu kikaoni imegongwa mhuri wa ‘Siri’. Kwa hiyo, hoja ya siri ipi inastahili kugongwa mhuri wa ‘Siri’ ikabaki imesimama. Pili, nikamwambia kuwa kama gazeti, tuliitumia barua hiyo kuonesha maajabu ya kiburi cha baadhi ya watumishi wa Serikali. Hivyo tuliichapisha kuthibitisha yaliyotokea mkutanoni na ndiyo habari yenyewe.

 

Katika Mkutano huo wa Juni 17, 2013 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwakatalia watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wasipitishe ununuzi wa bidhaa kwa mafungu, bali kwa kubainisha kiasi cha kila kinachonunuliwa. Kwa kiburi cha ajabu, baada ya mkutano kumalizika wakakaidi maelekezo ya Balozi Sefue.

 

Kwa kiburi hicho, ambapo kampuni zimejipatia hadi Sh milioni 400, kampuni tatu kati ya nane zilizopewa zabuni ni hewa. Tumewasiliana na Msajili wa Kampuni (BRELA), ametafuta kwenye orodha ya kampuni zake, hakuna majina hayo!

 

Kampuni zilizopewa zabuni na hazipo kwenye orodha ya msajili ni pamoja na The True Colours Entertainment Group (sh milioni 50), Big Mama’s Woodworks (sh milioni 29.6) na Wild Cat Publishing (sh milioni 278.4). Kampuni nyingine zimepewa mafungu ya mamilioni yasiyo na mchanganuo.

 

Kilichonifurahisha, Mwanasheria wa Ikulu na wote waliokuwa kwenye kikao hicho, walikiri kuwa kila tulichoandika ni cha kweli, ila wakaendelea kuhoji kwa nini tulichapisha mhuri wa SIRI? Niliwafafanulia kuwa tulichapisha barua hiyo, kwa nia njema ya kuonesha jinsi kivuli cha mhuri wa ‘Siri’ kilivyotumika kuchota mamilioni ya fedha wahusika wakijua hakuna mtu atakayehoji kwani wana kinga ya mhuri wa SIRI.

 

Sitanii, niliamini na naendelea kuamini kuwa Sheria ya Usalama wa Taifa ya Mwaka 1970 na Kanuni zake zinazosema aliyechapisha nyaraka za SIRI anaweza kufungwa hadi miaka 20 jela, haikutungwa kulinda wabadhirifu wa fedha za umma.

 

Napata shida kuamini kwa nini Ikulu ihangaike na sisi kama JAMHURI, maana jana Manyerere na Mihale nao walitarajia kuhojiwa na kuandika maelezo sawa na mimi, wakati ikikiri kuwa ni kweli umetokea ubadhirifu. Ubadhirifu huu haukufanywa na Ikulu wala Wizara ya Mambo ya Nje kama taasisi, bali watu wachache wanaofanyia kazi taasisi hizi.

 

Nawaza na kuwazua, kuwa hivi nchi yetu imefika mahala watu waliokwapua fedha za umma – tena kwa kuvunja sheria, wakikaidi maagizo halali ya Katibu Mkuu Kiongozi  – wanapaswa kupata kinga na waliofichua ubadhirifu huu ndiyo wasulubiwe? Ikiwa hivyo ndivyo, Tanzania tunaandika historia mpya na kanuni mpya ya uwajibikaji. Naamini Watanzania hatutalikubali hili.

1178 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!