Wiki iliyopita wanachama wa unaotajwa kuwa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walisusia kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma.

UKAWA hiyo inaundwa na wanachama wa vyama vya upinzani miongoni mwa wajumbe wanaounda bunge hilo lililokabidhiwa jukumu nyeti la kuwezesha upatikanaji wa Katiba bora ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tumewasikia wana UKAWA. Wametaja sababu za kufikia uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba kuwa ni baada ya kuchoshwa kubaguliwa na kudharauliwa ndani ya bunge hilo.

Hadi jana wana UKAWA walikuwa wanashikilia msimamo wa kutotia unyayo vikaoni licha ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kuwasihi warejee katika meza ya mazungumzo ili waweze kufikia maridhiano kwa manufaa ya umma.

Siyo lengo langu kuelezea mlolongo wa hatua zilizosababisha UKAWA kufikia hatua hiyo. Lengo langu katika mahala hii ni kukosoa ruhusa ya kuunda umoja huo ndani ya bunge hilo.

Kwamba binafsi ninaamini lilifanyika kosa la kuruhu uundwaji wa UKAWA katika Bunge Maalum la Katiba, hasa ikizingatiwa kuwa chombo hicho siyo sehemu mwafaka ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Ni wazi kuwa kitendo cha kuruhusu UKAWA huo kimewabagua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Wajumbe wa bunge hilo kutoka vyama vya siasa vya upinzani tayari wamejibagua kwa kujitangaza kwamba ni kundi linaloshughulikia mchakato wa Katiba mpya.

Kwa tafsiri nyingine ni kwamba UKAWA imewabagua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotoka chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyama visivyo na wabunge na wengine kutoka makundi yasiyo ya kisiasa.

Lakini pia, UKAWA hiyo haikustahili kuhusisha neno ‘wananchi’ kutokana na ukweli usiopingika kwamba haikupata ridhaa ya wananchi nje ya bunge hilo.

Wengi tulitarajia kuona na kusikia wajumbe wa bunge hilo wakiwa wamoja katika kushughulikia mchakato wa Katiba mpya, wakijadili na kujenga hoja zenye maslahi ya taifa letu.

Lakini katika hali ambayo haikutarajiwa, Bunge Maalum la Katiba limegeuzwa kuwa uwanja wa kupimana nguvu za kisiasa, kusuguana na kupigania maslahi binafsi.

Leo UKAWA imeruhusiwa kuwagawa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kesho wajumbe wengine wa bunge hilo kama vile wanachama wa CCM nao wanaweza kuunda umoja wao, wakajiita majina ya kujikweza kisiasa kama vile Jicho la Katiba ya Wananchi (JIKAWA), Watetezi wa Katiba ya Wananchi (WAKAWA), na nakadhalika.

Si ajabu tukaona na kusikia wajumbe wengine wa Bunge Maalum la Katiba kama vile wanaotoka vyama visivyo na wabunge, wawakilishi wa wafanyakazi, watu wenye ulemavu, wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi yenye malengo yanayofanana nao kila kundi linaibuka na umoja wao ndani ya bunge hilo.

Siombi tufike huko, lakini ikitokea tukafika huko, matarajio ya kupata Katiba mpya inayosubiriwa na Watanzania kwa shauku kubwa yatakuwa yameyeyuka na kuiachia nchi yetu makovu yatakayochukua muda mrefu kufutika.

Kinachoonekana kama si kudhihirika wazi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni kasumba za unafiki na utafutaji maslahi binafsi zilizojengeka kwa idadi kubwa ya wajumbe wa bunge hilo. Wachache wenye nia ya kutetea maslahi ya taifa wanazidiwa na nguvu kubwa ya wengi wenye ‘roho mtaka vitu’.

Tangu mwanzo, mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba ulionekana kuwa na upungufu, hasa kutokana na namna wajumbe wengi walivyokosa nidhamu na kutupiana maneno ya kashfa na kejeli. Lakini hili la kuruhusu UKAWA linaweza lisiliache salama bunge hilo!

Kwa sababu hiyo, kuna haja ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kuwafafanulia Watanzania uhalali wa UKAWA ndani ya chombo hicho cha umma anachokiongoza.

Pamoja na ufafanuzi mwingine, Sitta atuhakikishie iwapo umoja huo wa wapinzani hauna taswira ya kuwagawa wajumbe wa bunge hilo katika kushughulikia mchakato wa Katiba mpya, na kama wajumbe wengine nao wanaruhusiwa kuunda umoja wa makundi yao.

Lakini bado ninasisitiza kwamba hakukuwa na sababu ya msingi ya kuunda UKAWA katika taswira inayoonekana moja kwa moja kuwabagua wajumbe wengine wa Bunge Maalum la Katiba. Nitaendelea kuamini kwamba ilikosewa kuruhusu uundwaji wa umoja huo ndani ya bunge hilo.

Mwisho.

1694 Total Views 7 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!