Imani yako inaakisi fedha zako

 

Nafahamu kuwa wengi kama si wote, tunakubaliana kuwa fedha zina umuhimu mkubwa katika maisha ya mtu, tunachotofautiana ni imani kuhusu fedha.

 

Mitazamo kuhusu fedha ndiyo huamua kiwango cha fedha alichonacho mtu. Hii ina maana kuwa kila mtu anamiliki kiwango cha pesa sawa sawa na imani ama mtazamo wake kuhusu fedha.

Kimsingi, zipo imani zinazosaidia watu kuwa na fedha za kutosha, zipo imani na mitazamo inayozuia watu kuwa na fedha ama inawafanya waishi maisha ya kupungukiwa nyakati zote!

 

Imani na mitazamo hii kimsingi huzalishwa kutokana na malezi, utamaduni na mazingira. Mtazamo wa mtu kuhusu fedha tunaita Money blueprint (Kila nitakapotumia neno hili la kimombo litakuwa limebeba maana hii).

 

Mathalani, ukiwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuna mivumo (myths) kuhusu kabila la Wakinga (bahati nzuri na mimi ni Mkinga). Watu wengi kutoka kabila hili wanasifika kwa kufanya biashara na matajiri wengi katika mikoa hii. Pamoja na sifa hii, Wakinga wanatajwa kuwa ni mabingwa wa ushirikina katika biashara zao.

 

Hivyo, utabaini kuwa kwa mtu anayewatazama Wakinga na utajiri wao, akiamua kuchukua myth hii, basi ataunganisha fedha na uchawi. Hii itakuwa kichwani kwake kwamba, ili uwe na fedha nyingi (tajiri) lazima uwe mchawi na hii ndio itakuwa, Money blueprint yake.

 

Mfano mwingine unawahusu rafiki zangu Wachagga. Wapo Watanzania wengi ambao wanaamini Mchagga yeyote anayetajirika lazima awe ametumia wizi ama dhuluma. Kwa Watanzania wenye mtazamo kama huu, ni wazi kuwa wanapoitazama fedha wanaiunganisha na wizi ama udhulumaji. Kwao hawa hii ni blueprint yao.

 

Ukiiangalia mifano hiyo utabaini kuwa  ni mitazamo inayozuia mtu kuwa na fedha nyingi (hata kama mwenye mtazamo huo akiwa hajijui). Hii ni kwa sababu watu wengi hawapendi uchawi, wizi na ujambazi.

 

Kwa kuwa wameunganisha fedha na uchawi, wizi na ujambazi, automatically wataichukia fedha bila hata kujijua! Matokeo ya chuki zao dhidi ya fedha yanadhihirika katika kiwango cha fedha wanazomiliki. (Nakuthibitishia kuwa ama wanakuwa ni maskini, au ni watu wenye kuhangaika milele kwa kupata fedha isiyowatosha-hata kama wawe ni wenye vyeo vikubwa).

 

Ingawa mtu kuwa na fedha nyingi si kipimo cha utajiri  lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anaweza kusema ni tajiri ikiwa hana fedha (hata kama iwe katika maumbo mengine). Kwa maana hii tukiongelea fedha kwa namna moja ama nyingine tunakuwa tukiiunganisha na utajiri (ingawa kuna watu hawataki kabisa kuwa matajiri – hawa nao blueprint zao ndivyo zinavyowaelekeza).

 

Kiuhalisia ni kuwa utajiri ama umaskini wa mtu haupo katika wingi ama uchache wa mali, au fedha anayomiliki. Tofauti kubwa iliyopo kati ya maskini na tajiri ni ya kifikra. Masikini huwaza kimaskini, tajiri huwaza kitajiri. Utajiri ama umaskini wa mtu huanzia katika fikra na mitazamo yake.

 

Kwa mfano, fikra za kitajiri  huamini kuwa ukiwa na fedha ya kutosha utaishi kwa furaha, amani na upendo kwa wengine, hivyo utatimiza agizo la Mungu kuwa mpende jirani yako kabla ya kumpenda Mungu. Fikra za kimaskini zitajinenea hivi, “si vizuri kuwa na fedha nyingi, kwa sababu hautampendeza Mungu.”

 

Kama Mchungaji Pepe Minambo kutoka Kenya alivyosema, ndivyo na mimi ninavyoamini kwamba ni vigumu kwa maskini kuingia mbinguni. Sababu za uwezekano wa maskini kuikosa mbingu zipo wazi; kwanza, maskini ni mlalamikaji na mnung’unikaji (na Mungu hapendi walalamishi na wanung’unikaji), maskini ana wivu na hajiamini.

 

Msomaji usisahau kuwa hapa siongelei maskini wa roho aliowasema Yesu Kristo, naongelea maskini wa fikra chanya. Ni vema tukafahamu kwamba tajiri huwa tajiri kabla hajamiliki kitu na maskini huwa maskini kabla ya kudhihirika kwa hali yake; kwa vile umaskini na utajiri vyote ni matokeo ya kuwaza.

 

Vile vile nigusie kundi maarufu sana la uchumi wa kati (middle class). Hawa ni watu ambao hawana fedha nyingi na wala si maskini kabisa. Kundi hili ni sumbufu sana kifikra na ndilo husambaza fikra hasi kuhusu fedha. Kundi hili hupenda kuridhika mapema na hupendelea sana usalama (comfort zone).

 

Kinachosikitisha zaidi  ni kwamba kuna wanasiasa wanadai kupigania uwepo wa Watanzania wengi katika kada hii ya watu wa kati; wakati mfumo na uchumi wa dunia unawafuta kwa kasi kubwa. Mfumo wa uchumi wa dunia uliopo (na utakaoendelea kuwapo kwa  mamia ya miaka ijayo) unawabeba watu wa aina mbili; maskini na tajiri.

 

Ni ama uchague kuwa maskini, au tajiri. Kazi ni kwako msomaji kama unaamini na kutamani kuwa mtu wa kada ya kati. Kwa wanaofuatilia duru za uchumi kwa umakini hawashangazwi na hali iliyopo ya matajiri kuendelea kuwa matajiri na maskini kuzidi kuwa mafukara, si Tanzania tu bali ni katika dunia nzima.

 

Kwa  kuwa ninaongelea kuhusu imani kuhusu fedha ni vema nikagusia imani iliyochimbika miongoni mwa baadhi ya Wakristo. Katika Biblia kumekuwa na maandiko ambayo, tafsiri (nasisitiza kuwa ni tafsiri kwa sababu Biblia ipo perfect) zake zimekuwa na Money blueprint ambazo hazimsaidii mtu kutafuta na kumiliki fedha. Nitataja maandiko mawili; la kwanza ni lile lisemalo, “Huwezi kumtumikia Mungu na mali” na la pili ni lile lisemalo, “Kupenda fedha ni shina la maovu yote duniani”.

 

Si kusudio langu kuhubiri (ingawa nina karama ya kuhubiri pia) lakini nifafanue kidogo kuhusu maandiko hayo. Neno mali (ama Biblia nyingine zimeandika fedha) limetafsiriwa kutoka katika neno Mamos linalomaanisha ‘roho inayotawala mali’. Kwa maana hii, kimantiki ilitakiwa kueleweka kuwa, “Huwezi kumtumikia Mungu na roho inayotawala mali”.

 

Kuhusu fedha na maovu ninachoamini ni kuwa ikiwa pesa itatumika vibaya itazalisha maovu na ikiwa itatumika vema inaleta tija. Ni kama kisu kilichopo jikoni, kinaweza kukata mboga na kinaweza kutumika kuua ama kumdhuru mtu. Kusema kisu ni chanzo cha ‘mauji yote ya jikoni’ itategemea umeangalia upande upi wa matumizi.

 

Kwa upande wa malezi na utamaduni wetu nako kumezalisha imani na mitazamo mingi iliyo hasi kuhusu fedha. Kwa mfano; jamii zetu zinaamini kuwa wanaume ndiyo wanaostahili kuwa na fedha kuliko wanawake. Ndiyo maana mwanamke anapotajirika migogoro hutokea ikilinganishwa na mwanaume anapotajirika.

 

Wanawake wengi walio matajiri utasikia habari kuwa  ama hajapata kuolewa, ama aliolewa akaachika, ama ndoa aliyonayo ina mgogoro mkubwa. Unajua tatizo linapoanzia? Nitaeleza hapa chini, lakini kabla nataka niseme jambo hili; imani  ya jamii kuhusu fedha ndio husababisha wanawake wanaotajirika kuonekana kuwa hawapo sawa.

 

Katika familia nyingi watoto wanapokua, huwa kuna mazoea ya kuomba fedha kwa mama. Mama zetu mara nyingi tukiwaomba fedha huwa wanasema kauli kama hii, “Msubiri baba yako, akija ndiyo atakupa fedha”. Kinachojengeka katika akili ya mtoto ni kuamini kuwa, wanawake hawana na hawastahili kuwa na fedha! Hii ni Money blueprint hatari sana na imechangia sana wanawake wengi kuwa nyuma katika kujitafutia fedha na kutajirika.

 

Kutoakana na blueprint hii ndiyo maana huwa sishangai ninapoona mabinti wakijiorodheshea vigezo vya wanaume wanaowataka; katika vigezo hivyo hawaachi kuweka, ‘mwenye kazi nzuri (moja kwa moja atakuwa na fedha)’, ‘mwenye fedha za kutosha’, ‘aliye maarufu (umaarufu kwa kiasi fulani huleta fedha)’ na vigezo vya kufanana na hivyo.

 

Zipo imani na mitazamo mingine mingi ambayo imewaathiri watu wengi bila kujijua na imesababisha kuishi katika maisha ya uchache badala ya utele wa kifedha. Kwa mfano, wapo watu ambao wanaamini kuwa haiwezekani watu wote tukawa matajiri. Wanachosahau kujiuliza ni hiki, “Ni wapi imeandikwa kwamba wewe fulani bin fulani utakuwa maskini?” Kama dunia inaendelea kuzalisha matajiri, kwanini usiwe mmoja wao na badala yake unajivisha haki ya umaskini?

 

Wapo watu wengine ambao wanaamini kuwa matajiri ni mabahili; kwao hawa utajiri ni ubahili na wengine wanajiridhisha kuwa fedha haiwezi kununua furaha. Ukweli ni kwamba matajiri wengi wana nidhamu ya matumizi ya fedha (ndiyo maana wanazidi kutajirika) na uhalisia ni kwamba ingawa fedha si kigezo pekee cha mtu kuwa na furaha lakini siku za maskini hutawaliwa na huzuni kutokana na kutopata anavyovitaka. Kupata unachokitaka ni moja ya mihimili ya furaha. Kuna uwezekano wa mtu kupata unachokitaka kwa sehemu kubwa ikiwa utakuwa na fedha.

 

Msingi mwingine wa kupata fedha (na mafanikio mengine yoyote) ni kuzingatia kile unachokipenda na sio kile usichokipenda (focus on what you want and not on what you don’t want). Hii inatokana na kanuni mbili za kiubongo na kiasili; ambazo ni hizi (Nitatumia kiombo kidogo).

 

Kanuni ya kwanza inasema “What you focus expands yaani unachozingatia hukua” na ya pili inasema “Your eyes will see what your mind has prepared to see – macho yako yataona kile ambacho fikra zake zimejiandaa kukiona”. Iko hivi, ukitaka fedha zingatia utele (namna ya kuongeza fedha) na usizingatie uchache (kuishiwa, kufilisika).

 

Nihitimishe makala haya kwa kudurufu mambo machache. Mosi, kila mtu anayo nafasi sawa (equal chance) ya kuwa na fedha za kutosha kumpa uhuru wa kiuchumi. Pili, hakuna raha wala sifa ya kuendelea kuwa maskini, kwa sababu maskini ni mzigo kwa dunia.

 

Maskini na umaskini wake hata awe ni mtakatifu na mwema kiasi gani ni kwamba anaitesa dunia (kwa sababu anahitaji kusaidiwa). Tajiri (ama niseme mwenye fedha za kutosha) hata kama ni mchoyo ama bahili bado ni msaada kwa dunia (kwa sababu anajisaidia).

 

Pamoja na haya yote, si kusudio langu kuwabeza maskini na tena si kusudio langu kuwataka Watanzania wote wawe matajiri (japo ikiwa hivyo nitafurahi pia – maana mimi nitakuwa mmoja wa matajiri); lakini ninataka kila mmoja apokee changamoto ya kutamani kuwa na uhuru wa kifedha na kiuchumi.

 

Hili linawezekana ikiwa mitazamo na imani za wengi kuhusu fedha zitabadilika na kuwa zinazosaidia badala ya kuvuruga nafasi ya mtu kupata fedha. Kila Mtanzania anastahili ushindi wa kifedha!

 

0719 127 901,

[email protected]