Baba wa Taifa, Mwalimu Juliua Kambarage Nyerere, aliliasa Taifa kuendelea kuchunguza kuwapo kwa nyufa na kuziziba zitokeapo katika kuta za ‘Nyumba’ ya Taifa.

Sasa twaweza kusema kwamba hadhi ya polisi miongoni mwa jamii imeteremka, kiasi kwamba tuzibe nyufa kwa kupitisha sheria ya kubadilisha wajibu wa kuthibitisha katika kesi za jinai, uwe kwamba mtu akifa mikononi mwa polisi, ichukuliwe kwamba polisi huyo au hao wamesababisha kifo hicho kwa nia mbaya, yaani ama kwa kusudi, kutokujali au kwa purukushani mpaka ithibitishwe na polisi vinginevyo bila shaka yoyote.

 

Wajibu na madaraka kwa jumla ya polisi vimeainishwa katika vifungu Na. 5 na 27 vya Sheria ya Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322 ya Sheria za Tanzania, 2002. Sheria hiyo inaagiza kwamba polisi wataajiriwa kutoka upande hadi upande mwingine wa Tanzania kwa ajili ya kuhifadhi na kudumisha, amani, kuzuia na kupeleleza jinai, kukamata wahalifu na kulinda mali.

 

Polisi watachukuliwa kuwa kazini wakati wote na wanaweza wakati wowote kuagizwa kufanya kazi popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lililokuwa maalum ni kwamba kifungu Na. 29 cha sheria hiyo kinawezesha polisi kubeba silaha katika mazingira yaliyoainishwa, wakiwa na misingi ya maana.

 

Pia, kifungu Na. 28 kinatamka kwamba polisi atachukuliwa kuwa askari jela katika mazingira yaliyoainishwa, akiwa na madaraka, ulinzi na marupurupu ya askari jela.

 

Yaliyotajwa hapo juu ni ya kinadharia, ya kuandikwa ubaoni, tofauti na polisi wanavyotenda au kukosa kutenda kinyume wakati mwingine na kuonesha picha ambayo inatukumbusha tahadhari ya Mwalimu kuhusu nyufa katika kuta na paa za nyumba Tanzania.

 

Kifungu Na. 90 cha Sheria za Tanzania, 2002, kinatamka katika Kiingereza ambacho nakitafsiri katika Kiswahili kama ifuatavyo;-

 

“90 – (1) Mahakama itachukulia kuwa halisi kila waraka unaoelekea kumaanisha kuwa ni Gazeti la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au wa Zanzibar au gazeti au jarida au kuwa Sheria Binafsi ya Bunge, ambayo imechapwa na Mpiga Chapa wa Serikali, na kuwa halisi andishi linaloelekea kumaanisha kuwa andishi ambalo sheria inataka litunzwe na mtu yeyote, mradi andishi hilo limetunzwa kimsingi katika sura inayotakiwa na sheria na imetolewa katika ulinzi unaokubalika.”

 

Hicho kifungu Na. 90 kinaturuhusu kurejea yaliyoandikwa katika magazeti, ya tarehe iliyooneshwa katika mabano, kuhusu tabia mbovu ya polisi kama ifuatavyo: Vigogo wa polisi K’jaro katika kashfa ya uporaji bilioni 5/- (4/3/2013); FFU waacha lindo, waingia disko na SMG (25/04/2013); Polisi ivunjwe. Iwe kitengo ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

 

Yadaiwa kutumiwa vibaya na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Chadema wahoji visu vya Mahita (Mei 7, 2013) Kashfa ya vyeo Polisi – udini, ukabila, rushwa vyatumika (Mei 8, 2013); Polisi wakutwa na fuvu, walitaka kumbambikizia kesi mtu. Walidai awape Sh. mil 25/-   wamuachie (Mei 10, 2013); Polisi waua mtoto kwa risasi (Mei 10, 2013); Polisi wapiga mabomu kanisani (Mei 12, 2013); Polisi wa Mwanza wadaiwa kuwalinda watuhumiwa (Mei 13, 2013); Polisi 16 wakamatwa Dar es Salaam (Mei 14, 2013); Kwa matukio haya Jeshi la Polisi lipo ICU (Mei 19, 2013). Polisi wakamatwa na bangi gunia 18 waisafirisha kwa gari la mkuu wa FFU (Mei 20, 2013); Hadhi ya Jeshi la Polisi imepoteza heshima na imani ya wananchi.

 

Baba livunje urudishe heshima ya nchi! Urudishe heshima ya rais! Bado anasimama waziri bungeni na kulisifia Jeshi hili hili la Polisi (Mei 22, 2013); Kashfa zimelilemea Jeshi la Polisi (Mei 28, 2013); na lini Polisi watatoboa siri? (Juni 2, 2013); Vigogo Polisi watajwa ufisadi wa kukwepa kodi (5/6/2013); na Mbunge ashutumu Polisi kubambika watu kesi (05/06/2013).

 

Si kwamba Jeshi la Polisi halipati kusifiwa linapostahili, mathalan, “Kwa hili hongera Jeshi la Polisi” (Mei 22, 2013); na, “Polisi wakamata shaba ya Sh mil. 300/- (5/6/2013)”

Sasa tutakuta imedhihirishwa kwamba tofauti na kawaida, yanapotokea mauaji yanayohusu Polisi, mauaji hayo yachunguzwe kwa mujibu wa Sheria inayotawala  Uchunguzi wa Sababu za Kifo (Inquests Act) sura ya 24 ya Sheria za Tanzania, 2002.

 

Sheria hiyo inamtaka Afisa Mchunguzi wa Vifo achunguze sababu ya kifo cha mtu ambaye kwa msingi wa maana anadhaniwa kwamba amekufa kutokana na matumizi ya nguvu, au ambaye amekufa akiwa chini ya ulinzi wa madaraka rasmi, au ambaye amekutwa mahali katika mazingira ambayo yanalazimu uchunguzi kufanyika kwa mujibu wa sheria yoyote iliyoandikwa.

 

Uchunguzi wa kifo ukiisha, Afisa huyo anatakiwa kuandika uamuzi kama marehemu ni nani; kama ni kwa jinsi gani, lini na wapi marehemu amefia, kama mazingira ya kifo yanafichua kosa la jinai. Kama jinai imefichuliwa, Afisa huyo anatakiwa uamuzi wake wa uchunguzi autume kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.

 

Sheria hiyo ya Uchunguzi inafafanua kwamba afisa huyo ni mfanyakazi wa Serikali, au afisa aliyestaafu ambaye ameteuliwa na Jaji Kiongozi kwa sababu kwamba mtu huyo ana sifa za kuwa mstaafu, ambaye alikuwa hakimu wa ngazi yoyote; au mstaafu ambaye zamani alifanya kazi kama polisi katika ngazi isiyo chini ya inspekta; mstaafu ambaye zamani alifanya kazi kama Afisa Mtawala wa ngazi yoyote katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mfanyakazi mstaafu wa aina yoyote nyingine ambaye, kwa maoni ya waziri ambaye anashughulikia mambo ya sheria, anaweza kutimiza wajibu wa Afisa wa Uchunguzi wa Vifo na anaheshimika katika eneo la makazi yake; na mfanyakazi mstaafu wa Serikali, ambaye kwa maoni ya Waziri huyo, ana uwezo wa kutimiza wajibu wa Afisa Mchunguzi wa Vifo.

 

Katika kuuawa watu na polisi, inawezekana kabisa kutenda jinai kinyume na vifungu 196 na 195 vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, 2002. Vifungu Na. 196 na 197 vikisomwa pamoja, vinatamka kwamba mtu yeyote ambaye anasababisha kifo cha mtu mwingine kwa makusudi, kwa tendo au kutokutenda bila halali, atahukumiwa kwamba anyongwe mpaka kufa.

 

Vifungu 195 na 198 vikisomwa pamoja, vinataka kwamba mtu, kwa kitendo kisicho halali au kwa kuacha kutenda kusiko halali, atasababisha kifo cha mtu  mwingine, ataweza kuhukumiwa kifungo hadi cha maisha.

 

Kifo hicho kinaweza kuwa kimesababishwa na kitendo au kutokutenda huko, kutokana na uzembe wa kulaumiwa katika kutimiza wajibu wa kutunza maisha au afya, ikiwa kitendo hicho au kutokutenda huko ki/kuliambatana na kusudio la kusababisha kifo au kujeruhi mwili.

 

Kwa hiyo, polisi akiua mtu, mauaji hayo yachunguzwe na Afisa wa Uchunguzi wa Vifo ili kieleweke kwa kujitetea kadri sheria inavyomruhusu. Na hii inawezekana kwa sababu sheria imeainisha watu mbalimbali ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Afisa wa Uchunguzi wa Vifo popote nchini, yaani tuachane na utamaduni unaoshika kasi wa polisi kujiundia tume kuhusu uhalifu wao.

 

Uchunguzi huo unaweza kufichua kwamba polisi alifyatua risasi akiwa karibu na marehemu ambaye angeweza kumkamata badala ya kumpiga risasi, kwamba silaha iliyotumika ilikuwa ya hatari mno, kwamba polisi mhusika alilewa bangi au dawa za kulevya, na kadhalika.

 

Je, kama polisi hawataaminika kwa makubwa kama kuua mtu, wataaminikaje kuhusu mambo ya chini ya hayo, kama mbinu za kiintelijensia za kushughulikia vurugu za mikusanyiko ya watu, matumizi sahihi ya kompyuta, na upelelezi kwa jumla?

 

Katika makala, “Lini Polisi watatoboa siri”, mwandishi alizungumzia kuumizwa kinyama kwa Saed Kubenea  na Ndimara Tegambwage (Januari 5, 2008), kwa Dk. Stephen Ulimboka (Januari 26, 2012) kwa Absalom Kibanda (Machi 5, 2013) na kuuawa kwa Daudi Mwangosi (Septemba 2, 2013). Mpaka leo, upelelezi haujaibua lolote la maana kuhusu matukio hayo, na wote walioangalia runinga watakumbuka polisi kukanganyika kuhusu sababu za kifo cha Mwangosi.

 

Je, ni Polisi wangapi wamesoma vitabu kama ‘Criminal Investigation Techniques 1978 (Mbinu za Upelelezi wa Jinai); Police Operational Intelligence (1968) (Mbinu za Kipolisi za kufanya kazi ya Ujasusi); na The Police and the Community 3rd ed 1980 (Polisi na Jamii Toleo la tatu). Polisi  gani amenunua vitabu kuhusu polisi kwa pesa zake? Ni vitabu vingapi polisi anakuwa amevisoma mwishoni mwa mwaka? Ni sinema ngapi za upelelezi wa kipolisi anazoziangalia polisi kila mwezi na kadhalika?

 

Kama polisi watajichelewesha kwa yote yaliyo muhimu, Tanzania itabaki kuwa mkaribishaji wa kudumu wa mashirika ambayo historia yake ya kutukuka ni ya tangu zamani, kama Scotland  Yard iliyokuwapo 1849, FBI (Federal Bureau of Investigation) ambayo historia yake inaanzia 1908; na INTEPOL (Internationa Criminal Police Organization) ambayo chimbuko lake ni 1914.

 

Narudia kwamba tuachane na mtindo wa Polisi kujichunguza wao wenyewe, hasa kuhusu mauaji, na kutoa majibu yanayopendelea maslahi yao. Tuzibe nyufa.

 

*Novatus Rweyemamu ni Wakili Mwandamizi anapatikana na kwa simu 0784 312623

Please follow and like us:
Pin Share