Baadhi ya Watanzania ni watu wa ajabu sana, maajabu waliyo nayo mengi yamejifunga kwenye kitu kinachoitwa “mizengwe”, tabia ya kufanyiana roho mbaya hata kama kufanya hivyo hakumnufaishi yeyote, huku wakikiacha chenye manufaa kwao au kukosa kulishughulikia tatizo lililo na madhara makubwa kwao.
Mfano, inatokea kashfa inayotishia uhai wa nchi, Watanzania wananyamaza kama hawaioni au tuseme haiwahusu, ila wanaiweka kama kiporo ili baadaye ikatumike kama fimbo ya kumchapia mtu ambaye, kwa sababu mbalimbali zenye manufaa binafsi na si kwa nchi wala kwa manufaa yao katika ujumla wao, wanaamua kumsakama tu ili wamkwamishe katika mpango anaokuwa amepania kuutekeleza kwa manufaa ya nchi au ya watu wenyewe kwa ujumla! Ni mizengwe tu!


  Watu wenyewe wanapofanya hivyo hawajali ukubwa wa kashfa kwa kuulinganisha na ukubwa wa manufaa watakayoyapata wala kuangalia ni kashfa ipi ya nyuma na ipi ya karibuni. Wanaweza wakakumbuka kashfa ya nyuma, hata iwe ndogo kiasi gani ilimradi tu kuonesha uimara wao katika mizengwe!
 Sababu, kwa mfano, huwezi kusema miaka 50 iliyopita kijiji fulani kilikuwa kimevamiwa na simba na kuwafanya wananchi waliomo walazimike kuwaogopa wanyama hao waliomo kwenye historia, ukaacha kuwaambia wanakijiji hao washirikiane kumsaka simba aliyevamia kijiji hicho kwa wakati huo hata kama ni mmoja. Mizengwe haina mantiki hata kidogo.


 Hapa nchini kwetu kuna kashfa mbili ambazo zimelikumba Taifa letu kwa nyakati tofauti. Kashfa hizo ni za Richmond na Akaunti ya Tegeta Escrow. Richmond ni kashfa ambayo ina miaka kama minane tangu itokee, ilishughulikiwa ikaisha. Lakini, Akaunti ya Tegeta Escrow ni kashfa ambayo bado ipo na madhara yake yanaendelea kutokea na kuonekana.


Jambo la ajabu ni kwamba kimizengwe, inakumbukwa kashfa ya Richmond ambayo imebaki kwenye historia tu wakati kashfa ambayo bado inavuma huku baadhi ya watu wanaohusishwa nayo wakipelekwa mahakamani inafanywa kusahauliwa!
Hayo yanafanyika wakati ikieleweka kwamba ukubwa wa kashfa hizo mbili unatofautiana sana, ambapo ukubwa wa kashfa iliyotangulia ya Richmond haufikii hata robo ya ukubwa wa kashfa inayoendelea kuvuma kwa sasa ya Tegeta Escrow Account, lakini inafanywa hivyo ilimradi tu kuihusisha kashfa hiyo ya zamani na mtu mwenye malengo ya kuwanufaisha wananchi kwa namna fulani kusudi kumkwamisha asifanikishe malengo yake, mizengwe!


 Wakati nchi inajiandaa kumpata rais wa awamu ya tano, wapo watu wanaotajwatajwa kuwa wanafaa kwenye nafasi hiyo, huku baadhi ya wengine wakionesha nia ya kuitaka nafasi hiyo kwa udi na uvumba. Sasa kinachofanyika siyo kumtazama anayefaa zaidi kwenye nafasi hiyo,  ila kikubwa sasa ni kutaka kufanyiana mizengwe ya kwamba fulani akose hata kama anafaa kwa namna gani.


Hapo ndipo mizengwe inakoanzia kiasi cha kuyakumbushia yaliyopita na kumalizika hata kama yalikuwa madogo, huku yakisahaulika yaliyopo kwa wakati huu hata kama ni makubwa zaidi! Mizengwe! Baadhi ya watu wanahusishwa na kashfa za kale wakati kashfa za wakati huu zinazouma na kupuliza zikiwekwa kando!
Hebu tukaziangalie kashfa hizi mbili, Richmond na Tegeta Escrow Account zikoje. Richmond ni kampuni iliyopewa kandarasi ya kufua umeme wa dharura wakati nchi imekabiliwa na tatizo kubwa la nishati hiyo. Tatizo lilikuja kwamba kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kufua umeme wa dharura kama makubaliano yalivyokuwa. Kwa ufupi tunaweza kusema kwamba kampuni hiyo ilitaka kuitapeli nchi.


Na mtu unapofanyiwa utapeli siyo kwamba unakuwa umelenga kutapeliwa, kwamba kutapeliwa unakufurahia, hapana, inatokea tu kama mtu anayeibiwa. Hakuna anayependa kuibiwa ila wizi upo na unaendelea katika maeneo mbalimbali.
Kufuatia kashfa hiyo, Bunge likaunda kamati ili kuichunguza kwa kina kashfa hiyo. Ikagundulika kuwa kandarasi iliyotolewa kwa kampuni hiyo ilikuwa imejaa utapeli. Katika taarifa ya Kamati Teule ya Bunge akaguswa vilevile waziri mkuu, taarifa ya kamati ikasema kwamba huyo, waziri mkuu, Edward Lowassa kwa wakati huo, inamuachia alipime suala hilo na kuamua mwenyewe ni lipi la kufanya.


Ni mazingira hayo yaliyomfanya Lowassa aamue kuwajibika, sababu ni kweli kwamba kandarasi ya kufua umeme wa dharura iliyotolewa kwa Richmond ilifanyika wakati yeye akiwa waziri mkuu. Kitendo alichokionesha kilikuwa cha uungwana mkubwa sababu kuwajibika kwa aina hiyo kulishasahaulika hapa Tanzania.
Katika nchi nyingi, tukio la kashfa inayogusa maisha ya wananchi likitokea chini ya uongozi wowote ni lazima aliye juu awajibike. Lakini kwa Tanzania tumeona matukio mengi yaliyojaa kashfa wahusika wakuu wakikataa kuwajibika kwa madai kwamba hawahusiki.
 Mwaka 1996 meli ilizama na kuua karibu abiria wote katika Ziwa Victoria, waziri husika aligoma kuwajibika kwa madai kwamba siyo yeye aliyekuwa nahodha wa meli hiyo!


  Wakati mwingine treni ilirudi kinyumenyume ikaanguka na kuua watu wengi, waziri husika akagoma kuwajibika kwa madai kwamba siyo yeye aliyekuwa akiendesha treni hiyo!
Matukio ya aina hiyo yamekuwa mengi na wahusika wakigoma kuwajibika kwa madai ya kutokuwapo kwenye maeneo ya matukio wakati yanatokea. Kwa hiyo, la Edward Lowassa kukubali kuwajibika ni la kupigia mfano, sababu ni la kipekee.


Kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ni mpango mahususi wa kifisadi, pale hapakuwapo na tatizo lolote isipokuwa mpango wa kunyakua pesa ya umma ambayo ilionekana isingekuwa rahisi kujulikana kwa vile ilikuwa inaonekana imeishalipwa kwa kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL. Na ndiyo maana ikawa inasisitizwa kuwa pesa hiyo siyo ya umma.


Kufuatia ukwapuaji huo wa pesa ya umma iliyokuwa imewekwa kwenye akaunti maalumu ikisubiri usuluhishi kati ya kampuni ya Serikali, Tanesco na kampuni ya kufua umeme wa dharura ya IPTL, ndipo pesa ijulikane iende wapi, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) baada ya uchunguzi wa kina ikatoa taarifa iliyomgusa pia waziri mkuu, Mizengo Pinda, ikimtaka naye awajibike.


Lakini tofauti na alivyofanya Lowassa, kuwajibika mara moja, mara hii Pinda akaweka pamba kwenye masikio na kujifanya haelewi wala kusikia kinachoendelea! Aligoma kuwajibika, sikumshangaa sababu ndivyo nchi yetu ilivyo kwa wakati huu.
Ila ikumbukwe kwamba hakuna mwananchi yeyote anayeweza kuthibitisha kuwa Lowassa alihusika kwenye kashfa ya Richmond mbali na taarifa tu za kwenye vyombo vya habari.


Lakini kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow inayoendelea mpaka sasa, kila mwananchi alimsikia au kumuona kupitia kwenye runinga Pinda akitetea kwa nguvu zake zote kuwa pesa ya akaunti ya escrow haikuwa ya umma.


 La kushangaza ni kwamba pesa iliyodaiwa si ya umma imesababisha watu mbalimbali kufikishwa mbele ya Mahakama wakidaiwa kuichota! Serikali inawashitaki vipi watu ambao hawakuchota pesa ya Serikali? Kwa nini mwenye pesa asiachiwe akawashitaki mwenyewe kama kweli pesa ilikuwa ya kwake?
Na katika wale waliokanusha kwa nguvu zote kuwa pesa ya Tegeta Escrow Account siyo ya umma, wamo wanaotajwa kuutaka urais wa nchi. Hao hawaguswi ila wanaohusishwa na kashfa mfu ya Richmond ndiyo wanaosakamwa! Hayo ndiyo maajabu ya Watanzania.
Kukiacha chenye manufaa kwao wakikikamia kwa sababu ambazo si ajabu nyingine ni mfu na kuacha kukiangalia kilicho mbele yao hata kiwe na madhara ya kuwaangamiza!
 
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512

2045 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!