Rais Buhari kuinusuru Nigeria

buhariHakuna ubishi kwamba Marekani ni taifa kubwa kwa kujiimarisha kiuchumi na kiusalama. Kadhalika, hakuna ubishi kwamba rais wa Marekani ndiye anayetafsiriwa kuwa ni kiongozi wa dunia.
Hii inatokana na vyombo vikubwa vya uamuzi kama vile Umoja wa Mataifa (UN) vinaisikiliza Marekani. Hivyo basi, ni rahisi kusema kwamba Barack Hussein Obama ni Rais wa dunia.


Ikulu ya Marekani haikusita kumwalika Jenerali Muhammadu Buhari katika sherehe za kumwapisha Rais Obama kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kushinda kiti hicho, miaka saba iliyopita.
Hii maana yake ni kwamba Rais huyo mteule wa Nigeria, anaheshimika kimataifa kwani mbali ya yeye, mwingine aliyealikwa ni Nelson Mandela, wakiwa ni Waafrika pekee.


 Mara baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Nigeria (INEC), Attahiru Jega, kumtangaza rasmi Buhari, kiongozi wa chama cha upinzani cha Nigeria kuwa rais wa taifa hilo kubwa barani Afrika, Goodluck Jonathan aliyeangushwa, alikuwa wa kwanza kumpongeza.
Rais huyo mstaafu mbali ya kukubali matokeo, alitumia mwanya huo kumpigia simu mpinzani wake, Jenerali Buhari na kumpongeza kwa ushindi huo wa kihistoria. Naye pia amepongezwa kwa kuwatuliza wafuasi wake na kukubali matokeo.


 Historia inasema kwamba tangu uhuru mwaka 1960, kumekuwa na mapinduzi pamoja na matokeo ya udanganyifu kila kunapofanyika uchaguzi, lakini ushindi wa Buhari unafungua ukurasa mpya katika historia ya Nigeria iliyojaa misukosuko.
Hakuna rais aliyewahi kukubali kushindwa katika uchaguzi nchini Nigeria kwani licha ya madai ya udanganyifu, waangalizi wameupongeza uchaguzi huu na hisia zinazotokana na matokeo ya amani.


Ikumbukwe tu hayo yamejiri licha ya mfumo mpya wa kielektroniki unaotumika barani Afrika kuingia dosari mara kwa mara, huku wadadisi wa masuala ya ndani wakisema kuwa inaonekana kuwa Nigeria sasa imekomaa kisiasa.
 Historia bado inamulika na kuonesha kwamba Nigeria imekuwa ikishuhudia mapinduzi kadhaa ya kijeshi tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka wa 1960.


Hofu iliyopo sasa nchini humo ni kwamba huenda wafuasi wa Jonathan na Buhari wanatofautiana kimsingi katika masuala kadhaa ikiwamo ya kidini na vile vile kimajimbo.
Wanigeria wengi wamefurahi kuwa hatimaye wameweza kumng’oa madarakani Jonathan katika ushindani mkali baada ya kuonekana Serikali ilipwaya kwenye kutekeleza majukumu yake kikamilifu.


Buhari anaelezwa kuwa kiongozi mwenye ufuasi mkubwa na heshima nyumbani, hususan katika rubaa ya kaskazini mwa Nigeria.
Bila shaka hilo linatokana na sera zake za kupambana na ufisadi na ukosefu wa nidhamu, wakati alipokuwa mtawala wa kijeshi mapema miaka ya 1980. Itakumbukwa kwamba Buhari alipata kuiongoza Nigeria kijeshi kati ya mwaka 1983-1985 kupitia mapinduzi.


Kampeni ya Jenerali Buhari ilitilia mkazo mambo kadhaa, miongoni mwake utawala bora, kufufua uchumi, maendeleo ya miundombinu, umeme na nishati, kilimo, elimu, afya, ardhi na usafiri, kuwezeshwa wanawake, usalama na ajira.
 
Mwenyewe anasemaje?
Buhari anasema kuwa ushindi wake unamaanisha kuwa taifa hilo linafuata mfumo wa kidemokrasia baada ya kumshinda Jonathan kwa kura milioni mbili, idadi ambayo wachanganuzi wanasema kuwa itazuia harakati zozote za kuanzisha kesi.
Hata hivyo, alifanya kampeni za kidemokrasia kwa lengo la kutaka kusafisha siasa katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika. Lakini je, ni wa kijeshi au kidemokrasia?
 
Buhari ni nani?
Muhammadu Buhari ni Muislamu, mzaliwa wa Jimbo la Katsina, Nigeria kaskazini. Alizaliwa mwaka 1942 na alikuwa kiongozi wa saba wa taifa la Nigeria kati ya  mwaka 1983 na 1985.
Ni jenerali mstaafu aliyepata mafunzo ya kijeshi nchini Nigeria, Uingereza, India na Marekani. Na aliwahi pia kushika nyadhifa za ugavana, kamishna wa rasilimali ya mafuta, mwenyekiti wa shirika la umma la mafuta na pia mwenyekiti wa mfuko wa amana ya mafuta.
Anasemekana kuwa si mkaidi, bali hakubali kukata tamaa kwani licha ya kushindwa katika chaguzi tatu, amerejea kushindania tena urais dhidi ya Rais Jonathan, mfuasi wa dini ya Kikristo, anayetoka eneo la Niger Delta, kusini Nigeria, kwa mara ya pili.
Kushindwa mwaka 2003 na tena 2007, alipata kuhangaika na matokeo ya chaguzi hizo mahakamani bila mafanikio.
Kwa nini Buhari anaelezwa kuwa kiongozi mwenye ufuasi mkubwa na heshima nyumbani, hususan katika rubaa za kaskazini? Bila shaka inatokana na sera zake za kupambana na ufisadi na ukosefu wa nidhamu, wakati alipokuwa mtawala wa kijeshi.