Cha kufahamu ni kwamba, nguvu hizi hazitokei kwa bahati mbaya isipokuwa huamriwa na muhusika mwenyewe. Kadiri unavyouchukia umaskini ulionao unajenga nguvu ya kukutoa hapo. Kadiri unavyojenga hamasa ya kupata fedha ama mafanikio makubwa ndivyo nguvu ya kukufikisha huko inavyojengeka ndani yako. Ukijua unapoelekea ni rahisi kutafuta njia ya kukufikisha huko.

Kuhusu mimi mwenyewe. Kiujumla tangu zamani nilitokea kuyachukia sana mazingira ya ukawaida wa kiuchumi katika familia niliyozaliwa. Hii ilijenga nguvu kubwa sana ya kunifanya nipambane kujikwamua na hali ile. Wakati fulani huko nyuma nilidhamiria kununua basi dogo kwa ajili ya biashara ya usafirishaji abiria. Wakati ninapata wazo hilo, mfukoni mwangu nilikua na Sh laki nane tu.


Bei ya gari nililotaka kununua lilikuwa Sh milioni tisa; sikuwa na rasilimali nyingine yeyote wala rekodi za kibenki kuniwezesha kupata japo mkopo. Nilichofanya niliorodhesha majina 20 ya watu ambao nitawafuata na kuwaeleza mpango wangu wa biashara kisha kuwakopa fedha za kuwezesha biashara hii.  Kila jina moja nilipanga kukopa Sh milioni mbili.

 

Niliweka majina 20 kwa sababu nilitambua kuwa wengi wao hawatanipa Sh milioni mbili zote, wapo watakaonipa pungufu na wapo ambao hawatanipa kabisa. Ndivyo ilivyotokea, kuna walioniazima Sh milioni moja, wapo walionipa Sh 50,000 na kuna walioniambia hawana kitu lakini katika orodha hiyo wapo walionikatisha tamaa wakidai ninaota ndoto za mchana kuwaza kununua gari tena la biashara!


Katika kila niliyemfuata nilimueleza hivi, “….nina Sh milioni saba, nimepungukiwa na Sh milioni mbili. Ukiniazima hizo nitazirejesha ndani ya miezi sita/mwaka/mwezi mmoja….” Wakati nikifanya ukusanyaji huu nilikuwa nikitembea na mchanganuo wa biashara unaoonesha namna biashara hiyo inavyolipa.


Hatimaye nilinunua gari nililolikusudia na kuanza biashara ya usafirishaji kwa kutumia Sh laki nane tu! Huhitaji kuambiwa kilichotokea baada ya hapo, kwa sababu nilikuwa nimejiongezea thamani. Sitaki kueleza katika makala haya changamoto zilizonipata baada ya kukamilisha lengo hili; lakini baada ya hapo mambo yalikuwa nafuu tofauti na mwanzo.

 

Kwanza nilipata mtandao wa matajiri wa magari (kwa sababu nilikuwa na gari), pili ikawa ni rahisi kumwambia mtu niazime kiasi fulani cha fedha kwa sababu anajua si wa kubabaisha na tatu hata taasisi za fedha zinaanza kukugombea kwa sababu unakopesheka.

Mbinu hii niliitumia mimi na ilileta matunda kwangu. Sikupi ‘garantii’ uitumie kama ilivyo kwa sababu inategemea mazingira uliyonayo, kiwango chako cha uthubutu pamoja na ukubwa wa nguvu nilizozitaja (push power na pull power). Lakini kuna mambo nataka uyabaini kutokana na mchapo wangu huu.


Yapo mambo ambayo unaweza kuyatumia kama bidhaa ya kubadilisha na fedha. Mambo haya yanajumuisha, uhusiano mzuri na watu, taarifa sahihi, utu wema, umaarufu, uaminifu unaotambulika kwa watu, uwezo wako kiakili na mengine yanayofanana na hayo. Hata hivyo lazima ijulikane kuwa suala la kupata mafanikio (katika fedha na maeneo mengine) linahitaji uwekezaji endelevu wa mwenendo wa maisha ya kawaida.


Uhusiano na watu unategemea tabia yako kimaisha (upendo, kuwajali watu, kuwaheshimu, n.k.). Taarifa sahihi zinatokana na kujisomea, kuongea na watu na kujielimisha. Vile vile uaminifu unatokana na uwakili wako katika kazi, elimu na mambo mengine. Mambo haya yanaweza kukupatia fedha ikiwa utaamua kuyaunganisha na kusudio lako la kutafuta fedha.

 

Kwenye mchapo wangu nimesema niliorodhesha watu 20 ambao niliwafuata na kuomba wanikopeshe fedha. Kilichonipa ujasiri wa kuwafuata ni jinsi navyoishi nao na ile kujua kuwa wananiamini. Jambo la pili nililolitumia ni kuwa na taarifa sahihi kuhusu biashara ya kusafirisha abiria; kwa maana hiyo wazo langu nilikua naliwasilisha kiujasiri na uthubutu mkubwa.


Huwezi kuwa unaishi maisha ya ovyo, kama ufujaji wa fedha halafu utegemee watu wakuamini katika fedha na kukupa mtaji. Huwezi kuwa mvivu wa kutafuta taarifa (kujisomea, kubadilishana mawazo, n.k.) halafu utegemee kupata ‘deals’ za fedha.

 

Vile vile unatakiwa kuwa makini sana na aina ya watu unaohusiana ama kuwasiliana nao. Haiwezekani uwe unafanya mawasiliano ya ‘ovyo’ kwa asilimia mia moja kwa kutumia simu ama mtandao wa kompyuta halafu utegemee kukutana na watu wa maana. (potential people).


Vilevile, katika kutafuta fedha ni muhimu sana mtu kuachana na visingizio, kwa sababu visingizio ni matokeo ya kukata tamaa hata kama mhusika hujitambui. Kila mtu mahali alipo ana fursa fulani ambayo bado hajaitumia inayoweza kumwezesha kuzalisha fedha. Si lazima fedha uione kwa macho, si lazima uishike mkononi, na si lazima uikamate siku hiyo hiyo; lakini unaweza kuibua mazingira ama mawazo yatakayokuwezesha kuzalisha fedha.

 

Kule kwenye kisa cha Wanaisraeli nimetaja jambo la pili ambalo ni akili kutumia uwezo usiotumika bado inapotokea utegemezi umeondolewa. Watu wengi wamekuwa wakiishi kwa utegemezi ndiyo maana kuna mambo wanakwama ikiwemo kutafuta fedha. Kwa bahati mbaya suala la utegemezi linahusisha fikra, ndiyo maana kuna mtu anaweza kuwa ameondolewa utegemezi lakini bado akawa hajafunguka kutokana na kutofunguka kifikra na kimawazo.

[email protected], 0719 127 901


By Jamhuri