Usiku  na  mchana, usalama na utulivu wa nchi unatoweka kwa sababu milio ya risasi na mabomu inarindima. Makazi salama yanavunjwa na miundombinu inabomolewa. Zahanati na vituo vya afya vinapokea majeruhi na wagonjwa wengi kuliko kawaida. Maiti wanazagaa barabarani na hospitalini, maji na vyakula vinapatikana kwa shida, sababu vita ya wananchi wenyewe kwa wenyewe.

Baadhi ya nchi duniani zimepata kutumbukia katika madhira mabaya kama haya na kupoteza maisha ya wananchi wasio na hatia. Vijana walio nguvukazi ya taifa lolote wameteketea na kuiacha nchi yao katika umaskini zaidi.

Picha ya aina hii inapatikana katika nchi ambayo wanasiasa mazuzu na uchwara, mafisadi na wadhulumati wanapoamua kuungana na mabeberu kuhujumu uchumi wa nchi na kulitumbukiza taifa lao katika tabu, mashaka na mauaji yasiyokwisha kwa wananchi.

Hivi ninavyozungumza kwa mfano, nchi za Iran, Yemen, Sudan, Afrika ya Kati, Libya na DR Congo zimo vitani. Kisa na mkasa, matumizi mabaya ya istilahi za kisiasa. Si mageuzi, mapinduzi au mabadiliko tu, zipo istilahi kama demokrasia, chaguzi, haki za binadamu na kadhalika, zimetumika.

Kuingia katika mapigano au vita ya wananchi wenyewe kwa wenyewe si ufahari. Wala si mtindo (fasheni), au mchezo na burudani. La hasha!  Ni upumbavu uliokithiri katika akili ya mwanasiasa na wenzake ambao wana macho – hawaoni, wana masikio – hawasikii, bali wana akili zilizolala.

Mwanasiasa ni binadamu, si mdudu au mnyama. Binadamu anaongozwa na hulka, dhamiri na nafsi. Mambo ambayo yanamwezesha kujenga tabia ya umoja, kutambua baya na zuri na kujijua na kuwajua wenzake katika kufanya kazi, kutoa mchango wake wa mawazo ili kuleta maendeleo ya jamii.

Hulka ni tabia ambayo mtu anajifunza kutoka katika jamaa yake na jamii yake anamoishi. Ni maadili na mwenendo. Dhamiri ni akili inayomwezesha kutofautisha kati ya mambo yanayostahili kutendwa au kutotendwa katika jamii anamoishi. Nafsi ni hali ya kujijua ni binadamu na kuwajua watu wengine kwamba wao pia ni binadamu.

Wanyama na wadudu huongozwa na silika tu, na baadhi yao wana tabia ya  kujenga umoja kama binadamu. Umoja wao ni wa kufanya kazi si wa kujitambua. Mwanasiasa anapojifanya kama hana hulka, dhamiri na nafsi: bali ana silika ndipo huwa kama mnyama na hajitambui katika jamii, na kuona usaliti na vita kwa jamii ni turufu ya kupiku. Kwake ni sawa tu.

Ikumbukwe kwamba Tanzania ni taifa changa kiuchumi na maskini ikilinganishwa na taifa la Marekani, Urusi, Ujerumani au Uingereza kama watu fulani wanavyolinganisha uchumi na maendeleo ya mataifa hayo na Tanzania. Taifa letu lina miaka 55 (1964 – 2019), ambapo mataifa haya yana miaka kuanzia 200 na kuendelea. Wao wamekwisha kuendelea, sisi bado.

Si  muruwa na si sawa kulinganisha uchumi na maendeleo ya jamii ya mataifa haya na uchumi na maendeleo ya jamii ya Tanzania. Huu ni uonevu uliokithiri. Ni sawa kama kulinganisha nguvu na uwezo wa kushindana kupigana kati ya Habibu Kinyogoli na Angalieni Mpendu. Ni dhahiri Mpendu hafanani na Kinyogoli, atadundwa.

Wanasiasa ni jambo jema kwenu kutoa elimu ya kina kuhusu siasa. Siasa ni sayansi, taaluma na ni mpango maalumu katika maendeleo na maisha ya mtu. Mnapochezea siasa kwa kutukanana na kutoleana kashfa kwenye majukwaa, mnatujengea chuki na uhasama wa kudumu. Si jambo jema.

Mabadiliko ni maendeleo kutoka hatua moja kwenda nyingine. Si fujo na si kejeli. Wanasiasa ni haki yenu kuthamini mabadiliko yanayopatikana na kuyakubali. Baada ya hapo mtuongoze kupata mabadiliko bora zaidi. Chonde msituhamasishe kupinga na kuharibu mabadiliko yaliyopatikana.

Watanzania tuwe wazi kukataa uchongezi. Tuwasikilize wanasiasa kwa utulivu na tuwakubali kwa hoja ya kuleta maendeleo, si kuzuia mipango na taratibu za maendeleo. Mabadiliko ni kama makuzi ya binadamu, yanakwenda kwa hatua, kuanzia mtoto mchanga hadi kikongwe.

By Jamhuri