Katika ya pili ya makala haya nilieleza kuwa unaweza kuibuka uvivu wa kufikiri na baadhi ya watu wakahoji juu ya gharama za kuendesha serikali yenye ukubwa niliopendekeza. Kwa hiyo mimi napendekezo iwepo Serikali ya Tanganyika, ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano.

Nilipendekeza pia kuwa mamlaka ya Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziwe na nguvu sawa. Ikiwezekana ziongozwe na marais wakisaidiwa na waziri mkuu. Kisha ndani ya Serikali ya Tanganyika na ya Mapinduzi ya Zanzibar ziundwe serikali za majimbo.

Serikali hizi za majimbo ziongozwe na mawaziri viongozi kama ilivyo kwa Afrika Kusini. Kisha halmashauri ziendelee kuwapo na yawepo mabaraza katika ngazi zote hizo kama ilivyo sasa. Hapa ndipo ninapotaka kupafafanua vyema leo ila kabla sijasasambua hili, naomba nikuahidi mapema tu kuwa suala la umoja wa kitaifa nitalifafanua kwenye makala yajayo.

Hata hivyo, kabla sijakwendelea mbali, ingawa nimejielekeza katika kueleza sababu na mfumo uhitaji wa Katiba mpya, nashawishika japo kwa ufupi kugusia matukio ya kisiasa yanayoendelea nchini. 

Haya matukio tunayoyashuhudia ni ushuhuda tosha kuwa nchi sasa inahitaji Katiba mpya kuliko wakati mwingine wowote. Sijawahi kupata tafsiri sahihi ya maana ya neno siasa.

Binafsi sitaki kijiingiza katika mtego wa kufafanua nini maana ya siasa, ila inanifanya niamini kuwa siasa ni mfumo wa kutolea huduma kwa jamii. Wale wenye uwezo wa kutoa mawazo yao hukasimiwa nguvu za kiuamuzi na kuwasemea wananchi badala ya kukusanya wananchi wote sehemu moja na kuanza kuchangia mawazo yao.

Kufanikisha hilo, naamini zinapaswa kuwapo kanuni za mchezo. Siasa haziwezi kuwa mchezo huru usio na sheria wala kanuni. Hii ndiyo iliyozaa mfumo wa kuendesha siasa kwa kutumia vikundi vya watu wenye mawazo na fikra sawa, kwa maneno mengine vikundi hivi vinaitwa vyama vya siasa. Napenda kuamini kuwa wanachama wa chama fulani, kama ni Chadema, CCM, CUF, UDP, NCCR-Mageuzi au kinginecho, wanapaswa kuwa na mtazamo wa aina moja.

Hii inasaidia wafuasi wa chama husika kupata fursa ya kushawishi waliopo nje ya chama chao kuunga mkono sera zao. Kama yalivyo maadili ya biashara, ni matumaini yangu kwamba hata siasa ukiamua kuhubiri Ujamaa na Kujiteemea, sitarajii sera zako zitekelezeke katika misigi ya ubepari au ndani ya chama chako uwe na wafuasi wasioamini katika sera zako.

Kuna umuhimu wa vyama kuzungumza lugha moja, bila woga wala unafiki. Kuna umuhimu wa vyama kubaki kama kundi, badala ya wachache kutafuta sifa binafsi. Hii niliishuhudia siku Chadema walipoamua kuwavua uanachama madiwani watano kule Arusha. Wapo watu waliodhani Chadema ingepoteza umaarufu, lakini kinyume chake ndicho kilitokea.

Upo mfano wa kibiashara unaoendena na mazingira ya siasa tuliyomo sasa. Kwa mfano itokee unaendesha biashara ya hoteli. Fungua hoteli mbili zipe majina tofauti. Wewe mmiliki wa hoteli hizo andika ubao wa matangazo ya aina ya vyakula unayouza.

Hoteli moja utakayoipa jina la Kyabakari, sema unauza wali uliochacha, samaki waliochina, mchicha ulionyunyiziwa maji machafu, chai iliyotiwa chumvi na mboga iliyotiwa sukari. Kisha katika hoteli hiyo weka vijiko na sahani za dhahabu kuvutia wateja.

Hoteli nyingine uiite Kanyigo, weka sahani na vijiko vya bati, kisha andika unauza mchicha safi, wali wa kisasa, samaki waliovuliwa kutoka maji baridi, una wapishi kutoka Marekani, China na Uingereza na sifa nyingine nyingi.

Fungua hoteli hizi mbili kila asuhuhi kisha baada ya wiki moja chungulia hesabu ni kiasi gani unauza kwa kila hoteli, ambazo zote zipo katika mji mmoja na pengine zikiwa zimepakana eneo la stendi na vyakula vinapikwa katika jiko moja bila wateja kujua siri hii.

Usicheke. Kwa mfano huo wapime viongozi wetu ndani ya CCM na vyama vya upinzani, kisha utapata jibu. Leo CCM wanadhani wanajivua gamba kwa msemo wao. Wanakaa wanafukunyuana, wanachonga nyaraka na kufuja mali kama tulivyoshuhudia kwenye ripoti ya CAG. Wao wanawaambia wananchi mawaziri watatoswa na mambo yanaishia hapo. Hapa ndipo ilipolala makala yangu ya leo.

Nchi hii ikiwa na Katiba mpya yenye mfumo wa kueleweka hatutashuhudia matatizo ya sasa. Kwa sasa tunafanya mchezo wa kusingiziana kama watoto wenye kunyang’anyana pipi. Wapo wenye matarajio binafsi wanaodhani njia sahihi ni ama kutukana upinzani au kupambana na Rais aliyepo madarakani na mawaziri wake.

Katiba mpya itayamaliza yote haya. Tutakuwa na mfumo ambao utakuwa na mgawanyo wa madaraka wa kueleweka. Kama walivyokaa wakafikiri na kuona kuwa Spika wa Bunge au Jaji Mkuu kukaimu nafasi ya urais ni kugonganisha mgawanyo wa madaraka.

Vivyo hivyo wabunge kuwa mawaziri ni mgongano wa mgawanyo wa madaraka. Wabunge wabaki kuwa wabunge wa Bunge, Serikali ibaki Serikali na Mahakama ibaki Mahakama.

Tunataka Katiba mpya itamke wazi kuwa mbunge hatakuwa waziri. Watateuliwa watu wenye utaalamu wao, majina yao yatafikishwa bungeni na wakifika watajieleza kama tulivyoshuhudia wagombea ubunge wa Afrika Mashariki, kisha tunawapima wananchi katika kinachoitwa public hearing.

Kupitia bungeni tutajua nani kapasi na anaahidi kuifanyia nini wizara kisha baada ya hapo tunampa kazi anayoiomba. Akishindwa tunambana.

Wabunge watabaki na kazi moja tu ya kuisimamia serikali. Hii itaepusha majungu na matarajio hewa ya watu kuteuliwa kuwa mawaziri. Kila hoja itazungumzwa kwa uzito wake na si kwa mitego ya matarajio ya kutunukiwa nyadhifa.

Sizungumzi kwa mafumbo, ila nalenga kueleza ukweli kwamba utaratibu wa mawaziri kutoka nje ya Bunge utatuwezesha kuwa na uwajibikaji wa moja kwa moja. Hutakuwa na mtu mwenye ujasiri kama Mustafa Mkulo anayeweza kusimama akaagiza mali za Serikali ziuzwe kwa watu binafsi kisha akakanusha. Hili halitakuwapo.

Nikirejea katika hoja yangu ya msingi, ni kwamba nchi yetu haiwezi kupata maendeleo ya mara moja kutokana na ukubwa wake. Kwa wasiofahamu, ukichukua nchi za Norway, Finland, Ujerumani, Uingereza, Denmark, Ufaransa, Italia, Ugiriki, Ubeligji, Uholanzi na vinchi vingine kama vitatu hivi vya Ulaya Magharibi, ukubwa wake ukijumuisha nchi hizo kieneo haulingani na Tanzania. Tanzania inakuwa bado ni kubwa.

Pengine baadhi yetu ambao hatujapata fursa ya kufika Ulaya inawezekana ikachukuliwa kuwa mifano niliyoitoa inakuwa ya mbali zaidi. Nchi ya Rwanda ukubwa wake ni kilomita za mraba 26,338 wakati ukubwa wa Mkoa wa Kagera ni kilomita za mraba 39,168.

Mkoa huu ukubwa wake ni karibu mara mbili ya nchi ya Rwanda. Wala Kagera si mkoa mkubwa katika nchi hii, nimeutolea mfano kwa kuwa umepakana na Rwanda.

Leo sikiliza sifa wanazomwagiwa Rwanda kwa kupeleka maendeleo kwa kasi kwa maana ya kujenga miundombinu ya barabara, reli, mawasiliano ya kompyuta, kuimarisha utawala bora, kudhibiti rushwa, kuwa na jeshi na watumishi wenye nidhamu, kuongeza mapato na kukusanya matumizi kwa usahihi na mambo mengine.

Nirejee kwa hapa nchini. Mimi nimepata bahati ya kutembelea mikoa yote ya nchi hii. Nikisema mikoa yote namaanisha na ile ya Pemba Kaskazini, Kusini Pemba, Mjini Magharibi, Uguja Kaskazini na Unguja Kusini.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, mwaka 2002 Zanzibar ilikuwa na wakaazi 984,625. Kati yao 622,459 walikuwa wakazi wa Unguja na 362,168 ni wakazi wa Pemba. Kwa sasa inakisiwa kuwa wamefikia wakazi 1,200,000. Tusubiri sensa ya mwaka huu itatupatia jibu sahihi.

Nimeitaja Zanzibar kwa nia ya kuonyesha jinsi eneo la kiuongozi likiwa dogo maendeleo yanavyoweza kuja kwa kasi. Ikumbukwe kama ilivyo kwa Rwanda, Zanzibar ina barabara za lami karibu kila eneo na maji yanatoka hadi majumbani kwa watu kwa zaidi ya asilimia 90. Umeme ukienda Pemba umesambazwa hadi vijijini.

Ni rahisi zaidi kusimamia eneo dogo la kiutawala kuliko ubabe wa kusema Waziri Mkuu anayetokea Nkasi, akiwa Dar es Salaam atoe amri ifika Tandahimba Mtwara, Namanga Arusha, Mtukula Kyaka na Namanyere Kigoma au Mvumi Dodoma. Tunajidanganya. Amri hizi zinabaki kufika huko kupitia magazetini na redioni.

Mwalimu Julius Nyerere hakuwa mjinga. Mwaka 1972 alianzisha mfumo wa utawala uliojulikana kama madaraka mikoani.

Mfumo huu ulikuwa mzuri mno, ila kwa bahati mbaya ulibaki kuwa wa usultani,s kwani waliopelekwa mikoani kusimamia kazi za maendeleo waliishia kuwa wateule wa Rais na si rahisi kwa Rais kuwasimamia wateule hawa siku hadi siku kujua wanafanya nini.

Dawa ni kiongozi mkuu wa jimbo achaguliwe na wapigakura wawe na haki na uwezo wa kumuondosha madarakani asipotenda sawa na alivyoahidi.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, leo anaweza kuamka asubuhi akajaza gari mafuta, akapita kila mkoa wa Rwanda na jioni akalala nyumbani kwake. Sisi hapa kwetu kwa ukubwa wa nchi yetu hata kama Rais wetu atatumia helikopta ya Chadema akasema kila mkoa atakaa kwa dakika 30, kwa mikoa 29 anahitaji saa 14 na nusu bila kuhesabu muda wa kuwa hewani akisafiri. Na hapo akikutana na wilaya kama ya Urambo ambayo ukubwa wake ni zaidi ya Mkoa wa Kagera, atazirahi.

Najua msomaji utatatizwa serikali hizi zitakusanyaje mapato, na nani atakuwa na mamlaka juu ya nani kuhakikisha hakuna mivutano na nchi iende mbele kwa kasi.

Ukurasa huu unazidi kuwa mdogo kwa uzito wa mada ninayoizungumza. Tukutane wiki ijayo nitakapomalizia umuhimu wa kuigawa nchi hii katika majimbo na kurejesha Serikali ya Tanganyika kama mbinu ya kupeleka madaraka mikoani.

Hapa tutakuwa na usimamizi wa karibu, miradi itasimamiwa na kwisha na nchi itapata fedha nyingi kupita kiasi. Usikose nakala ya gazeti la JAMHURI wiki ijayo kwa mwendelezo wa makala haya.

1426 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!