JAMHURI latikisa tuzo za Ejat

BalileWaandishi wa habari wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile na Victor Bariety, mwishoni mwa wiki iliyopita walijinyakulia tuzo za umahiri wa uandishi wa habari nchini (EJAT), zinazotolewa kila mwaka na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Balile aliongoza katika kundi la wazi ambalo hushindaniwa na kazi yoyote iliyofanywa vyema wakati Bariety alishika nafasi ya pili katika habari za Utawala Bora akizidiwa na Gwamaka Alipipi wa Nipashe. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Edson Kamukara wa Tanzania Daima (mwaka jana kwa sasa yuko Mawio).


  Balile aliyemshinda Elius Msuya wa Mtanzania, alizawadiwa kompyuta mpakato, cheti wakati Bariety alipata cheti na zawadi mbalimbali.
“Namefurahi sana,” anasema Balile huku akipongezwa na wadau mbalimbali waliohudhuria huku Bariety akisema, “Tuzo hizi zimenipa mwanga mpya wa utendaji kazi. Kuna thamani kubwa kuteuliwa na kushinda.”


Waandishi wa habari 959 ndiyo waliojitokeza kuwasilisha kazi zao mwaka 2014 ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na mwaka 2009 tuzo hizo zilipoanza kutolewa kwa mara ya kwanza kwa wanahabari ambako 304 waliwasilisha kazi zao.
Mwenyekiti wa Jopo la Majaji tisa waliofanya kazi ya kupitia kazi za wanahabari hao kwa muda wa siku saba, Jaji kiongozi Chrysostom Rweyemamu, anasema kulikuwa na changamoto nyingi katika kazi hiyo.


 Anasema licha ya idadi hiyo kubwa ya wanahabari kujitokeza na kuwasilisha kazi zao, ni 44 tu ndiyo walioteuliwa kwa sababu habari nyingi zilikosa ubora na mtiririko unaoonesha mwisho wa tukio na nyingine kuwa na lugha mbovu na maneno ya kashfa.
“Maeneo yaliyoshindaniwa ni 21 yakiwahusisha waandishi wa magazeti, redio na TV. Mwaka jana hakukuwa na mshindi yeyote wa upigaji picha za TV au video kutokana na kukosa ubora,” anasema Rweyemamu.


Anasema licha ya kundi la picha za TV kushika nafasi ya mwisho, mwaka wamepatikana washindani wawili tu, John Chacha wa ITV na Khamis Suleiman wa  Chanel Ten aliyeshika nafasi ya kwanza na kujinyakulia tuzo.
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini hapa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amewataka wanahabari walioshinda tuzo hizo kutobweteka na kuongeza bidii zaidi kwa kuzingatia kwamba vyombo vya habari vina jukumu kubwa sana la kuwafikishia wananchi habari.


Dk. Bilal anasema jukumu kubwa jingine kwa wanahabari mwaka huu ambao ni wa Uchaguzi Mkuu ni kuripoti habari zinazohusu uchaguzi na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kwa usahihi ili uchaguzi uwe huru na wa haki.

Bariety
“Kazi ya uandishi wa habari inamgusa kila mwanachi, ndiyo maana ukifika muda wa taarifa ya habari kwa desturi zetu tunasogea karibu la TV au redio, na wengine kusoma magazeti na mitandao ya kijamii, hivyo inapaswa kuheshimiwa,” anasema.
Pamoja na mbinu na uwezo wa kupata taarifa kuongezeka kwa kiwango kikubwa, Dk. Bilal amewataka wanahabari kuandika kazi zao kwa lugha sanifu ya Kiswahili inayopaswa kuenziwa na wananchi wote.