Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, kinakusudia kuzuia pikipiki za miguu miwili na miguu mitatu kutofika katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kutolewa ilani hiyo, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, amesimamisha kwa muda uamuzi huo, akitaka akutane na wadau wote ili kupata suluhu ya jambo hilo.

Hakuna sababu za wazi zilizotolewa na Polisi kuhusu uamuzi wanaotaka kuuchukua, lakini ni wazi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya uvujifu wa sheria na uhalifu vinavyofanywa na madereva na watumiaji wa aina hiyo ya usafiri.

Sote tunatambua faida hasa za ujio wa pikipiki na Bajaj. Miongoni mwa faida zake ni unafuu wa nauli na uokoaji wa muda kwa wanaotumia usafiri huo. 

Mathalani, wakati mabasi makubwa yakikaa vituoni au njiani kusubiri abiria, hali ni tofauti kwa pikipiki na Bajaj. U-haraka wa kupakia na kushusha abiria, na uwezo wake wa kupenya kwenye foleni za magari, kumewafanya wengi waupende usafiri huo.

Kama ilivyo ada ya kizuri kutokosa kasoro, usafiri huu umekuwa janga jipya katika orodha ya majanga yanayolikabili taifa letu. 

Pikipiki zimekuwa chanzo cha vifo na ulemavu kwa watu wengi watumiaji na wasio watumiaji wa usafiri huo. 

Pikipiki zimegeuzwa kuwa kitendea kazi muhimu kwenye ujambazi, ujangili, uporaji na wizi wa aina mbalimbali. 

Usafiri huu unatumika kusafirisha magendo na mali za wizi. Pikipiki zinatumiwa kuingia mistuni kusafirisha mkaa na mazao mengine ya misitu kinyume cha sheria.

Wenye pikipiki wamekuwa na dharau kubwa katika kufuata sheria za usalama barabarani. Hawatii sheria. Wanaendesha kadiri wanavyotaka au wanavyojisikia. Askari wa usalama barabarani wamekuwa wanyonge mno mbele ya watu hawa.

Yote haya yakifanyika, Bunge lenye watu tunaodhani wana weledi wa kukabiliana na hali hii, wakapitisha sheria kupunguza adhabu kwa makosa yanayosababishwa na waendesha pikipiki na Bajaj. 

Sheria hii ni miongoni mwa sheria dhaifu, maana haiwezekani dereva wa lori anayevuka taa nyekundu adhabu yake iwe tofauti na mwenye pikipiki anayefanya kosa hilo – tena wote wakiwa na leseni zinazotolewa kwa kuzingatia dereva kuzijua na kuziheshimu sheria za usalama barabarani.

Sheria hii ambayo kimsingi ni dhaifu, imewapa jeuri wenye pikipiki kufanya wanavyotaka wakitambua kuwa, ama hawawezi kukamatwa, na endapo wakikamatwa na kuadhibiwa, adhabu inahimilika.

Sasa tufanye nini? Suluhisho la haya si kuwaondoa bodaboda na wenye Bajaj katikati ya miji. Kinachotakiwa ni kwa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kusimamia sheria bila huruma. Isiwe hiari kwa mwenye pikipiki kuheshimu sheria, bali iwe lazima.

Jawabu la matatizo ya aina hii si kuyakimbia au kuyafukuza kwa namna ya kuyaahirisha, bali ni kutafuta njia za kisheria za kuyakomesha. 

Ni aibu kwa Polisi kunyoosha mikono kwa ‘wahuni’ wachache na kuwaumiza wengi wanaotumia usafiri huo.

By Jamhuri