“Laiti ingelikuwa, laiti ingelikuwa Katiba haingefupisha muda fulani, mimi ningeshauri hapa huyu bwana awe rais siku zote…”
Kauli hiyo ilitolewa tarehe 26 Juni, 2017 na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, wakati wa kutoa salamu za Eid el Fitr kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijijni Dar es Salaam.
Alitoa kauli hiyo katika kusisitiza maelezo yake kuhusu Rais Magufuli alivyo jasiri wa nafsi yake, anavyofanya kazi vizuri sana, hachelei roho yake kufanya jambo, ni mtu wa huruma na anayewajali wananchi wake.
Maelezo hayo na mengineyo yalizama ndani ya masikio ya waumini wa Kiislamu waliohudhuria sala ya Idd na pia yalidakwa na vyombo vya habari ambavyo vilifikisha ushauri huo kwa wananchi wote nchini.
Kwa maelezo ya Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassani Mwinyi, kauli hiyo ni ushauri wake binafsi kutokana na anavyomuona, anavyompima na anavyomtathmini Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, katika kuchapa kazi na kukubalika na wananchi wengi.

Ushauri huo umepokewa na wananchi katika mitazamo tofauti ikiwamo ya kumuunga mkono na kumpinga. Ukweli mitazamo yote hiyo ni changamoto kwa wananchi kutokana na Katiba ya Nchi; na “Mazoea.”
Wanaomuunga mkono Rais Mstaafu Mwinyi, wanakubali matendo mema na mazuri yanayofanywa na Rais Magufuli. Wanaompinga rais mstaafu huyo ni wale wanaohesabu dosari zinazotokea wakati rais yumo katika michakato ya kujenga amani na usalama wa nchi na wananchi.
Sipendi kwa sasa kuchambua Katiba ya Nchi na “Mazoea” ya wananchi kwa sababu yanafahamika, yanasimamiwa na yanatekelezwa na wananchi wenyewe kila uchao. Ndiyo maana Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi akatumia maneno kwamba laiti ingelikuwa Katiba haingefupisha muda fulani, yeye angeshauri rais huyu awe siku zote.

Naomba tukumbushane Watanzania wenzangu. Rais Julius K. Nyerere alitawala miaka 23. Kila baada ya miaka mitano katika Uchaguzi Mkuu, wananchi walipiga kura za NDIYO na HAPANA kumpata rais. Mara zote alipata ushindi wa kura za NDIYO. Katika utawala wake kulikuwa na tamu na chungu.
Ni Rais Nyerere mwenyewe aliyewaomba wananchi ang’atuke katika kutawala, amekaa madarakani muda mrefu. Alitaka na yeye amuone rais anavyotawala. Tangu nchi yetu kuwa Jamhuri, hakupata kumuona rais anavyotawala. Ombi lilikubaliwa. Akang’atuka.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985, wananchi walimchagua Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuwa rais kwa kura za NDIYO na HAPANA kwa kipindi cha miaka mitano. Ali Hassan Mwinyi aling’ara na kuzima machungu. Wananchi walifurahishwa na kazi zake hata kumwita “Mzee Ruksa”.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990 alichaguliwa tena kwa mazoea ya kura za ndiyo na hapana. Kabla ya uchaguzi mkuu uliofuata (1995), nong’onong’o ilisikika ya kumtaka Alhaj Mwinyi aendelee kuwa rais kama alivyokuwa mtangulizi wake, Mwalimu Nyerere; na ingine ilihesabu machungu yaliyotokea katika utawala wake.

Nong’onong’o hiyo ilishtua fikra za Mwalimu Nyerere, viongozi na wananchi mbalimbali wakiwamo wanaokubali na wanaopinga mazoea kuendelea. Mawazo ya Mwalimu Nyerere na mageuzi ya kisiasa katika nchi za Ulaya zikapiga kumbo kura za ndiyo na hapana na hatimaye kuzikwa.
Jitihada mbalimbali zilifanywa na viongozi na wanasiasa kwenye semina, mikutano ya hadhara na mafunzo ya elimu ya siasa kuelezea ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Aidha kuondoa mazoea na kuweka ukomo wa utawala ndani ya Katiba ya nchi.

>>ITAENDELEA

By Jamhuri