Summons ni wito maalumu wa mahakama. Mara zote unapofunguliwa mashitaka (unaposhitakiwa) hasa mashitaka ya  madai, basi ili uweze kufika mahakamani na kujua mashitaka yanayokukabili yaipasa mahakama kutuma wito maalumu  ambao kwa jina la kitaalamu huitwa ‘summons’.

Mara nyingi wito huu unapotumwa baadhi ya watu hukataa kabisa kuupokea na wengine huupokea lakini hukataa  kuusaini.  Zipo sababu tatu ambazo huwafanya watu wasipokee wito huu. Kwanza, ni imani kuwa usipopokea wito, basi  shauri ulilofunguliwa haliwezi kuendelea.

Pili, sababu nyingine ni kuamini kuwa ukikataa kupokea wito utakuwa umejitoa katika hatia (liability) ya kutambua  chochote kinachoendelea, hivyo chochote kilichopo mahakamani kitakuwa hakikuhusu.

Tatu, pia wengine hukataa kupokea wito kwa kuamini kuwa kupokea wito ni kukubali shitaka, hivyo ni bora  kuukataa kwa kuwa kufanya hivyo itakuwa ni kukana shitaka.

Je, kesi haiwezi kuendelea kwa sababu umekataa kupokea wito? Jibu ni hapana, kukataa kwako kupokea wito hakuzuii  shauri lililofunguliwa kuendelea. Na hii ni athari ya kwanza kabisa anayoipata mtu aliyekataa kupokea wito. Mtu  anapokataa  kupokea  wito,  basi yule aliyetumwa kupeleka wito huo atatakiwa kuapa kuwa alimpelekea fulani wito na  akakataa kuupokea.

Baada ya kiapo hicho atarejesha taarifa za kukataa kupokewa wito huo mbele ya hakimu au jaji mhusika aliyepangiwa  kesi hiyo.  Sambamba na hilo, ataambatanisha kiapo chake kuonyesha kukataliwa kupokewa wito huo.  Baada ya hakimu au jaji mhusika kupokea taarifa hizo, ataamuru shauri kuendelea upande mmoja (kama ataona inafaa).

Shauri kuendelea upande mmoja maana yake ni kuwa shauri litaendelea bila uwepo wa yule aliyekataa kupokea wito. Kwa hiyo jibu la swali hili ni kuwa kukataa kupokea au kusaini wito hakuzuii kesi kuendelea.

Je, kupokea au kusaini wito ni kukubali shitaka? Hapana, si kweli hata kidogo. Unapokubali kupokea wito au kuusaini  haimaanishi kwa namna yoyote kuwa umekubali shitaka. Hakuna uhusiano wowote kati ya kupokea au kusaini wito na  kukubali mashitaka. Kupokea au kusaini wito maana yake ni kuthibitisha tu kuwa umeona kuwa unaitwa.

Masuala ya kukubali kosa au kukataa yapo mahakamani. Ni pale unapokuwa mahakamani au wakati wa kujibu  mashitaka kwa maandishi ndipo unapoweza kukubali au kukataa kosa. Kwa hiyo hakuna haja ya kukataa kupokea au kusaini  wito kwa sababu hiyo.

Madhara ya kukataa kupokea au kusaini wito ni pamoja na kuendelea kesi bila kuwepo kwa aliyekataa kupokea wito.  Kuendelea kwa kesi upande mmoja ni kupatikana kwa hukumu ya upande mmoja.

Na mara nyingi hukumu za upande mmoja ni lazima tu aliyekataa kufika mahakamani awe ameshindwa. Kwa hiyo madhara makubwa kabisa yanayopatikana ni kushindwa kesi na kupoteza kabisa hata kile kidogo ambacho  alitakiwa kukipata.

Si rahisi kesi ikasikilizwa upande mmoja halafu aliyesikilizwa akashindwa. Bali ambaye hakufika mahakamani ndiye  atakayekuwa ameshindwa.

Madhara mengine makubwa ni kukosa kusikilizwa.  Unapokataa kupokea wito au kuusaini maana yake ni  kuwa hautafika  mahakamani. Usipofika mahakamani maana yake ni kuwa umejinyima haki ya kusikilizwa. Kumbuka uzoefu huonyesha  kuwa siku zote mpeleka mashitaka huwa ana kawaida ya kusema vitu vingi vya uongo na uzushi dhidi ya mshitakiwa.

Unaposhindwa kupokea wito, hivyo kutofika mahakamani, basi hakuna mtu wa kufika na kukana uongo na uzushi  kwa niaba yako. Utaifanya mahakama na umma kuamini kila kinachosemwa na utakuwa umekosa nafasi ya kupinga na  kuonyesha kusingiziwa.

Pia umo katika hatari ya kupoteza mali ikiwa mlalamikaji aliyefungua kesi anadai kitu kutoka kwako. Ikiwa anadai mali kama ardhi, nyumba, gari, baiskeli, mifugo au mali nyingine yoyote,  umo katika hatihati ya kupoteza hata kama ilikuwa  ni haki yako.

Hii ni kwa kuwa haukufika mahakamani, hivyo umetoa nafasi ya ushindi kwa mlalamikaji ambaye katika kukaza hukumu (execution) ataomba kupatiwa ile mali na mahakama itamteua dalali wa kuhakikisha unanyang’anywa hiyo mali na  atakabidhiwa mlalamikaji au mshitaki.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri