Wiki iliyopita tulikuletea sehemu ya nne ya makala haya yanayohoji usahihi juu ya nani anastahili kuchinja. Leo tunakuletea sehemu ya tano na ya mwisho ya makala haya. Endelea….

Ndivyo itakavyokuwa hata kwenye kitoweo kingine na serikali itakusanya kodi zake kwa uwazi zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo huenda wengine wanachinjia nyumbani kwao kwa siri halafu wanapeleka maeneo ya biashara na  kuikosesha kodi serikali.

Usipofuatwa utaratibu huu, unaweza kuathiri sana biashara ya mabucha, hoteli na migahawa, pale ambapo kundi ambalo halishirikishwi katika kuandaa nyama hiyo kwa misingi ya dini yao, litakapoamua kwa hiari, kususia nyama iliyotayarishwa na kundi jingine la dini kwa kutambua kuwa ile ni sadaka iliyotolewa katika imani tofauti.

 

Tusijidanganye sana kwa maneno mepesi yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba wote tunamwabudu Mungu mmoja. Maneno hayo hayatatusaidia kutatua migogoro kuhusu uchinjaji. Kwa sababu kama Mungu ni mmoja ni kwa nini mmoja awekewe masharti na mwingine hapana?

 

Biblia takatifu imekataza kula vyakula vilivyo tolewa sadaka kwa miungu. 1kor 10:19-20  inasema: “Basi niseme nini? ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.”

 

Katika 1Kor 10: 27-28 inasema:  “Na mtu asiyeamini akiwaalika nanyi mnataka kwenda kuleni kila kitu kiwekwacho mbele yenu bila kuulizauliza kwa ajili ya dhamiri. Lakini mtu akiwaambia kitu hiki kimetolewa kiwe sadaka msile kwa ajili yake yeye aliyeonyesha na kwa ajili ya dhamiri.

 

Hapa kwa mujibu wa maandiko haya tayari taratibu zote za Kiislamu zinahusika kwamba nyama inaandaliwa ikiwa ni ibada ya sadaka kwa mujibu wa imani yao, ambapo kwa mujibu wa Biblia ukiwambiwa hiki ni sadaka usile. Sadaka ni tendo lolote linaloonesha heshima ya juu kwa kinachoabudiwa.

 

Biblia Takatifu imekataza pia kula vyakula vilivyosongolewa yaani kunyongwa au kula damu. Tunasoma hayo katika kitabu cha Matendo ya Mitume 15:27-29 “Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.

“Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.”

 

Lakini Waislamu katika mazingira fulani wameamrishwa wale mzoga, damu na nyama ya nguruwe.  Katika Suratul An An –Am, 6:145 “Sema sioni katika yale niliyofunuliwa mimi ( niliyoletewa wahayi ,sioni) kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayo mwagika  au nyama ya nguruwe kwani hivyo ni uchafu, au kile ambacho kwa kukhalifiwa amri ya Mwenyezi Mungu, kimechinjwa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

 

“Lakini aliyelazimika (kula kwa ajili ya njaa au mengine) pasipokupenda wala kuruka mipaka, basi (huyo atasamehewa kwani) Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe (na) mwingi wa kurehemu.”

 

Unaposoma ufafanuzi wa aya hiyo uliyomo ndani ya Qur’an unasema “Hapa wanatajwa wale wanyama walioharamishwa kuwala kama walivyotajwa mara nyingi. Na inatajwa vilevile kama ilivyotajwa mara nyingi kuwa kwa dharura kubwa huhalalishwa kula hivyo vilivyoharimishwa.

 

Kwetu sisi Wakristo hatuna ruhusa ya kula nyamafu wala damu hata katika mazingira yoyote.Ez 4:14, Mdo 15:19-20

 

AHLUL AL-DHIMMI-RAIA WA DARAJA LA PILI WALIPAO KODI KUULIPA UTAWALA WA KIISLAMU

 

Mafundisho ya dini ya Kiislamu yameugawa ulimwengu katika makundi makubwa mawili (1)Dar al- Salaam yaani eneo lililojisalimisha chini ya sharia za Kiislamu, na (2) Dar al- Harb yaani eneo la vita lisilokubaliana na sharia za Kiislamu. Waislamu hujiita ni ummah uliyo bora kuliko wengine wote.

 

Katika Dar al- Salaam, eneo lililojisalimisha chini ya sharia za Allah, raia wasio kuwa Waislamu wanaoishi chini ya utawala wa Kiislamu huitwa Ahlul al- Dhimmi, yaani raia wa daraja la pili. Moja ya jukumu la Ahlul al- Dhimmi ni kulipa kodi kwa utawala wa Kiislamu inayoitwa, Jizyah.

 

Kodi hii hulipwa na Ahlul al- Dhimmi hata katika nchi au maeneo ambayo hayamilikiwi kwa sharia za Kiislamu kama Tanzania, lakini maadamu kuna Waislamu malipo hayo ni lazima yafanyike.

 

Kwa hapa Tanzania nchi isiyofuata itikadi yoyote ya dini, malipo hayo hupitia katika uchinjaji wa wanyama machinjioni, unaofanywa na Waislamu na huku wakitoa risiti zinazomilikiwa na taasisi mbali mbali za Kiislamu kwenye machinjio ya Serikali ambayo kimsingi ujenzi wake unakuwa umegharamiwa na kodi  inayotozwa na Serikali kutoka kwa raia wote wa  nchi bila kujali itikadi zao za kidini.

 

Hapa ndipo mgogoro unapoanzia. Hata hivyo utaratibu huo hauna tatizo lolote iwapo machinjio hayo yanamilikiwa na Waislamu wenyewe.

 

Kwa hiyo tunapoona kuna migogoro kuhusu uchinjaji wa wanyama kuanzia kwenye machinjio ya Serikali hadi majumbani mwetu, baina ya Waislamu na watu wengine wasio Waislamu, tatizo lipo kwenye kodi hiyo ya Jizyah, ambayo Waislamu huidai kwa nguvu kutoka kwa Ahlul Al-Dhimmi kama itikadi yao ilivyo, ili kutunisha mfuko wa kuendeleza Uislamu katika nchi hiyo.

 

Jingine ni namna uchinjaji huo unavyofanywa ukiwa umezingatia zaidi taratibu za dini moja kwa kuelekeza kinachochinjwa Qibla, huku ikitegemewa kuwa chakula hicho kitatumika pia na wale wasio wa dini hiyo.

 

Je, Uislamu ndiyo bora zaidi kuliko dini zingine? Jibu ni hapana. Dini zote kwa mujibu wa sheria za nchi ni sawa na zinapaswa kutendewa sawa (be treated equally) kama  vile yanavyotambuliwa makaburi, nyumba za ibada n.k.

 

Qur’an inawaamrisha Waislamu wale chakula cha Wayahudi na Wakristo kama tulivyoona hapo juu, sasa ni kwa nini wasiwe watiifu kwa Kitabu chao na badala yake wanaleta taratibu ambazo ni za kibaguzi kwa dhahiri?

 

Naamini hata wale wasio Waislamu wakiamua kutoshiriki chakula cha Waislamu kwa kujua kuwa wananyanyaswa na kundi hilo la imani, amani ya jamii itakuwaje? Mahusiano mema tuliyonayo yatakuwaje?

 

Je, kibiashara kwa wale wenye Mabucha itakuwaje? Kwa sababu nao WAYAHUDI na WAKRISTO wanazo namna zao za kuchinja wanyama ili iwe halali. Tazama Kut 12:5, Kol 3:17. Haya ndiyo Watanzania tunatakiwa tuyatafakari kwa makini na kwa uzito.

 

Waislamu nao kwa upande wao, wakiwa na dhamiri njema, na kwa kuzingatia kuwa wanajua kuwa wanaishi katika nchi ambayo ina dini mchanganyiko, na huku wao wangependa kufanya baadhi ya taratibu kwa misingi ya dini zao.

 

Wangeweza kujenga machinjio zao pembeni au sehemu nyingine kabisa ambako mtu mwingine asiye Mwislamu hawezi kuwaingilia, wakachinja kama maelekezo ya dini yao inavyowaagiza kuliko ilivyo hivi sasa ambako tunashuhudia migogoro na misuguano kila kukicha kwa ajili ya kuchinja.

 

Qur’an imeonya kuhusu mtu yeyote kutamka haraka haraka kuwa hii ni haramu au halali. Tunasoma hayo katika Suratul An Nahl, 16:116 “Wala msiseme kwa sababu ya uwongo usemao ndimi zenu hii ni halali na hii ni haramu msije mkamzulia uongo Mwenyezi Mungu.Hakika wale wamzuliao uongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu”

Unaposoma ufafanuzi wa aya hiyo ndani ya Qur’an unasema “Kukata hukumu ya kuwa jambo hili halali au haramu kunahitaji ujuzi barabara. Asijisemee tu mtu kuwa hili ni halali au haramu asiseme ila awe na hoja ya kusema hayo.”

 

Qur’an imethibitisha pasipo shaka kuwa akichinja Myahudi au Mkristo chakula hicho ni halali kwake. Mbona hata hilo Waislamu hawalikubali japo limeelezewa ndani ya Qur’an na kusababisha migogoro katika jamii? Itakuwaje kwa watu wa dini zingine ambazo hazijatajwa kuchinja ndani ya Qur’an ambazo Serikali yetu inazitambua lakini Uislamu hauzitambui?

 

Gharama zinazotozwa na Waislamu kwa kila mnyama anayechinjwa na wao ni (a) Ngombe mmoja Sh 2000 na (b) mbuzi mmoja Sh 1000 kuku na bata Sh 500. Unapopiga hesabu ya jumla ya  ng’ombe, mbuzi kuku na bata wanaochinjwa Tanzania nzima kwa siku, unaweza kuona kiasi kikubwa cha fedha kinachoingia katika mfuko wa Waislamu kupitia huduma hii.

 

Na hili ndilo tatizo la msingi linalosababisha kuwepo na mgogoro unaohusiana na uchinjaji kwa sababu wanaofaidika na kazi hii kiuchumi wanaona watapoteza mamilioni ya fedha wanazozipata sasa.

 

Rev. DANIEL MWANKEMWA

S.L.P 45290

DAR ES SALAAM.

+255 755 680101, +255 716 305120

[email protected]

By Jamhuri