Sehemu hii ya pili ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kugunduliwa kwa fuvu la binadamu wa kale la Zinjanthropus (Zinj) katika Bonde la Olduvai mkoani Arusha, wataalamu wawili wa mambokale – PROFESA CHARLES MUSIBA kutoka Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani; na DK. AGNESS GIDNA wa Makumbusho ya Taifa, wanaeleza fahari hiyo ya Tanzania na Bara zima la Afrika.

Profesa Musiba anasema ukitaka kujua umri wa tabaka za miamba au masalia yanayopatikana Afrika Kusini – yawe ya wanyama, yawe za zamadamu – lazima yalinganishwe na masalia yanayotoka Olduvai. Iwe ni Kenya, yanalinganishwa na masalia yanayotoka Olduvai, iwe ni Ethiopia yanalinganishwa na masalia yanayotoka Olduvai.

Kwa mfano, nimwite kama ni ng’ombe ambaye alikuwa ni kama mbogo wa kwanza kabisa, lakini ana pembe kubwa sana, ukizungumzia chimbuko lake ni Olduvai. Ukikuta Kenya au Ethiopia wanaangalia wanyama wanaofanana na mbogo wa asili wa mwanzo kabisa lazima watakuja kumlinganisha na wa Olduvai. Kwa hiyo Olduvai ina umuhimu mkubwa sana duniani, na mimi ningeongezea kwa kusema kwamba Zinj – katika abiria wa kwanza kabisa duniani kupanda British Airways, mzee kuliko wote alikuwa ni Zinj.

Alichukuliwa kwenda kwenye mkutano – British Royal Meeting mwaka 1959 na alilindwa. Ulinzi wake ulikuwa ni wa kushangaza sana. Walipomwonyesha kule na kumtolea maelezo ya kitaalamu watu wote wakashawishika.

Waingereza walikuwa ni wabaguzi sana kwa sababu walikuwa ni wakoloni. Wakati ule kusema chimbuko la binadamu ni Afrika na wakati ule wanasema ni Tanganyika ina maana kwamba ina- compromise [Mwingereza] yeye kwa sababu alikuwa ni mkoloni, sisi alituona kama watoto – kwa hiyo hapo inabidi akubali kuwa yeye na sisi tuko sawa. Wengi iliwawia vigumu sana [kukubali] lakini baada ya kuona hivyo viashiria wakasema hakuna ujanja, kweli chimbuko la binadamu ni Afrika na wakati ule mwanzoni kila mtu akakubali ni Tanzania.

Kuna hiyo element ya muhimu sana, lakini huwa hatuizungumzii kuhusu ubaguzi. Mimi huwa wanafunzi ninapowafundisha nawaambia we are all Africans – kwamba sisi wote ni Waafrika, awe na rangi nyeupe au nyingine lakini sisi wote ni Waafrika.

Asili yetu, chimbuko letu binadamu wote ni Afrika. Mwingine anaweza akasema Kenya, mwingine Ethiopia, mwingine Afrika Kusini, lakini katika mlolongo huo Tanzania [Tanganyika] ndiyo ya kwanza kutoa ushahidi kuonyesha kwamba binadamu wa kwanza wanatoka Afrika.

Rangi mbalimbali

Ni rahisi kuelewa. Wakati wa chimbuko la binadamu linaendelea wahenga wetu ilifikia wakati wakaanza kuwa wabunifu, maana ubunifu ulianzia huku [Afrika]. Wakaanza kutengeneza zana za kila aina. Pale Olduvai kuna Oldowan tools, kuna Chelian tools (zana za mawe).

Walipoanza kutengeneza hizo zana ikawaruhusu kuanza kuhamahama na idadi ya watu ikaendelea kuongezeka wakawa wengi. Ilifikia wakati fulani wakawa wengi. Ukiangalia historia ya binadamu kuna muhula ulifikia karibu binadamu wote watoweke kwa sababu ya mabadiliko ya mfumo wa hali ya hewa na mazingira.

Wakabakia wachache sana. Wakaendelea kuhama, na walipokuwa wanahama wanatoka maeneo kama ya kwetu hapa [Tanzania] wanakwenda Kaskazini. Ukishavuka Ikweta unakwenda juu – walikuwa na vimunduseli vinavyosaidia kuzuia magonjwa ya ngozi, kuzuia kansa ya ngozi (melanin).

Walipokuwa wanaendelea kuhama – melanin inatumika kwa mwili kupata vitamin D na inasaidia kwa wakati huo huo kulinda mwili. Walivyoendelea kuhama wakaenda sehemu za baridi. Wakaingia Ulaya – bado walikuwa ni weusi, lakini kwa sababu muda umepita, tunaongelea miaka mingi sana iliyopita [mamilioni], wakafikia mahali wakaanza kupoteza ile rangi nyeusi ya asili.

Kule wakaanza kukosa vitamin D kwa kuwa jua likawa halitokei kwa muda wote. Faida ya mtu kuwa na ngozi nyeusi unaweza kupata low density ya vitamin D. Sisi weusi japo tunakimbilia Ulaya kuna disadvantage kwa sababu inakulazimu kutumia vidonge vya vitamin D kufidia ule upungufu unaoupata kwa kukosa jua. Wakati mwingine unatakiwa unywe maziwa kwa wingi, na maziwa ya kule yanaongezwa vitamin D. Hiyo ndiyo inaitwa adaptive responsible.

Ndiyo maana baadaye tukafikia tukawa kwa mfano Ulaya wakawa weupe, walivyoendelea kuhama – kwa mfano ukiangalia India kuna watu ni weusi kuzidi wewe na mimi na hiyo ni kwa sababu wanaishi sehemu ambazo wanapata mionzi ya moja kwa moja mingi kama tunavyoipata hapa Afrika. Kwa hiyo melanin inawasadia kukinga mwili.

Hii ni hadithi lakini ina sayansi ndani yake. Kwa mfano huwa nawaambia Waingereza kwamba Mwingereza wa kwanza alikuwa mweusi. Amepatikana Cheddar man ametoka sehemu ya Cheddar Gorge nchini Uingereza. Kwenye vipimo vya DNA (vinasaba) wamebaini alikuwa na melanin kama za kwetu. Kwa hiyo kubadilika kwa rangi ni kwa ajili ya kujikinga na hali ya hewa.

 

Kwanini Zinj ni muhimu?

Dk. Agness Digna anaelezea fahari ya kuwa na Zinj, akisema dunia nzima imekuwa haina namna, isipokuwa kuitambua Tanzania na Afrika kuwa ndiko kwenye chimbuko la binadamu wote wa sayari hii.

Fuvu la Zinj ndilo linaloitambulisha Tanzania. Ugunduzi wa fuvu hili ulibadilisha uelewa wa wataalamu kuhusu chimbuko la binadamu.

Zinj alipatikana hapa Olduvai, ile sehemu alipopatikana mpaka sasa tunasema ni mahali pekee ambako tunaelezwa tabia ya binadamu aliyeishi miaka milioni 2 hadi milioni 1. Tunasema hapo ni classic site ambayo unapata taarifa zote za zamadamu walioishi miaka kuanzia milioni 2 hadi milioni 1.

Ukitaka kujua binadamu alifanya nini miaka milioni 2 iliyopita mahali pekee ambako dunia nzima inapatambua ni eneo la Zinj. Eneo hili ni muhimu sana kwa sababu masalia ya alipopatikana Zinj yanatoa taarifa nzuri sana kuhusu tabia za binadamu.

Tunajua tabia za zamadamu wa wakati huo walifanya nini. Tunapoishi kwenye nyumba zetu tunakula chakula au tunatupa masalia mahali fulani na yale masalia yanatambulisha tabia zetu – kama tulikuwa tunakula nyama, kama tulikuwa tunakula ndege; au mabaki ya nguo zetu (kwa sisi leo hii).

Kwa eneo alilopatikana Zinj tabia zao mahali pale ni mahali muhimu sana duniani. Panatambulisha tabia za binadamu walioishi kipindi hicho.

Saiti zote katika Bonde la Olduvai (kuna saiti nyingi), kabla hujasema hii saiti waliishi binadamu kipindi fulani – kipindi cha miaka milioni 2 mpaka milioni 1 – lazima ufanye rejea ya saiti ya Zinj.

Zinj amekuwa reference point kwa nchi mbalimbali za Afrika. Kwa mfano mtu anafanya utafiti Kenya, Ethiopia au Afrika Kusini akapata masalia ya kufanana na Zinj, kabla hajasema huyu ni jamii fulani lazima afahamu fuvu la Zinj likoje.

Kwa hiyo Zinj imekuwa reference point ya kutambulisha masalia mengine ya Afrika. Tunaifanya Zinj ni alama ya Tanzania na Afrika kwa jumla kwa sababu baada ya kugundulika hakuna fuvu la aina hiyo na baada ya kupatikana mengine ikawa Zinj ndiyo reference point katika kuelezea mafuvu ya Kenya, Ethiopia, Afrika Kusini na kwingineko duniani.

Tunaadhimisha Zinj, na ujumbe tunaoutoa hapa kwa jamii, nchi na mataifa mengine ni kwamba tunataka kueleza kuwa sisi tunajivunia kuwa Watanzania sababu ndiyo sehemu binadamu wote wametoka.

Tunazungumzia Zinj, lakini tuna masalia mengi sana ukilinganisha na nchi mbalimbali. Tanzania ndipo kwenye chimbuko la binadamu ambako bango letu ni Zinj, lakini ni nchi pekee ambayo unapata historia ya chimbuko la binadamu iliyokamilika. Huwezi kuiona Olduvai Gorge mahali pengine duniani. Ni hapa tu, na hata wanasayansi tunatambua hilo. Duniani kote huwezi kulinganisha mahali popote na Olduvai kwa sababu ina taarifa zote nzuri za maisha ya mwanadamu.

3388 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!