Gamboshi: Mwisho wa dunia (6)

Actors dressed as devils perform during the “gathering of the devils” ahead of Saint Nicholas Day in Podkoren December 1, 2010. On Saint Nicholas Day in Slovenia, a performer representing the saint goes around villages giving out presents to children, and is usually surrounded by performers representing devils. This group of actors from Italy, Austria and Slovenia are performing in Podkoren for the second consecutive year. REUTERS/Bor Slana (SLOVENIA – Tags: ANNIVERSARY SOCIETY) – RTXVAHK

Wiki iliyopita katika sehemu ya tano hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Lile limama lilinichukua likaniangalia kwa makini, likawa linasema: “Kanafanana nasi, umekapata wapi?” Lile litoto likasema: “Nimekaokota huko porini karibu na mpaka wa himaya yetu.” “Sasa unasemaje?” Lile limama likauliza tena litoto nalo likajibu: “Kaache tu mama kaende.” “Nenda ukakaweke kule kwenye mpaka wanakoishi watu wadogo kama yeye.” Haya niliyaelewa kutokana na ule mtambo niliofungiwa na wale rafiki zangu, watu wadogo Msemakweli! Unawakumbuka?

Lile limama likanichukua hewani juu kabisa na kwa kweli dunia yote nikawa ninaiona vizuri kumbe kweli iko kama tufe kubwa na imekaliwa na maji sehemu kubwa. Oh! Inapendeza kweli Kweli! Yule mama alipiga hatua moja, akainama na kuniweka taratibu ardhini.

Nilikuja kugundua kuwa umbali niliowekwa ulipata kilomita 1,200. Haya niliyafahamu kutokana na ule mtambo. Msemakweli kwa akili ya kawaida huwezi kuamini! Lakini ninachoeleza ndio ukweli wa mambo na niliyashuhudia kwa macho yangu haya mawili, na wala siwezi kuidanganya dunia eti ili nionekane mimi nimewahi kuona maajabu! Jamani ni ukweli mtupu na tafadhali mtakaosoma barua hii ieleweke hivyo na muwaeleze watu hivyo hivyo na wala msiwapotoshe vinginevyo.

Baada ya kuniweka chini eneo hilo, lile limama ikawa lilipokuwa linasimama, ile miti ya eneo hilo lote ilipata shida, ilisukwa sukwa kwa dhoruba ya pumzi za huyu mama. Na iliyo mingi majani yake yalipeperushwa na hata baadhi yake iling’oka ikaanguka sehemu za mbali, kiwiliwili chake hatimaye kilipotea angani na nikabaki peke yangu tena.

Baada ya kuzubaa zubaa kwa muda; nilianza kutembea. Nilitembea, nikatembea na baada ya masafa, nikaanza kuona nyumba. Hapa nikapata ahueni na hamasa ya kuwaona jamaa zangu ikaongezeka. Nilitembea kwa muda mrefu nikaanza kuona nyumba mbalimbali. Kilinichokatisha tamaa ni kule kutoona watu eneo hili, sehemu nyingine zilionekana kabisa kuwa ni mashamba ya mazao.

Sasa la ajabu ni wapi waliko watu wa eneo hili? Eneo hili lilikuwa na hali ya hewa kama ya kawaida, kwa hiyo uchovu ulianza kunizingira. Basi nikaona labda niingie moja ya magofu haya nipumzike na kisha niendelee na safari yangu ya kurudi nyumbani.

Nilipoingia kwenye nyumba mojawapo kwa mshangao nilimkuta bibi mmoja wa umri wa kati akanikaribisha kwa mshangao; “Kulikoni babu!” Akanichangamkia. Nikamjibu kwa mshangao: “Asante Bibi”.

Baada ya salamu nilimwelezea mambo yote yaliyonipata tokea uhai wangu, kuugua kwangu, kufa kwangu, na baadaye kupelekwa Gamboshi na maajabu ya huko na jinsi yule bibi alivyonitelekeza kusikojulikana… Nilimweleza yote kwa ufasaha na kinaga ubaga.

Nilipomaliza simulizi yangu kuhusu lile limama na litoto lake, yule bibi akacheka kidogo akasema: “Ndiyo Babu! Mimi ninakufahamu sana.” Akaniangalia kwa huruma kisha akaendelea: “Jina lako ni Bugulugulu Duu. Sawa! Wewe ndiye mkombozi niliyekuwa ninakungojea kwa miaka mingi. Karibu sana mjukuu wangu.” Nikang’aka nikasema: “Hapana bibi, cheo ulichonipa ni kikubwa mno. Na mimi si chochote wala si kitu kuwa na hadhi hiyo.”

Nikaendelea: “Kuna kitabu kimoja cha Waebrania ambacho kinadai kuwako mkombozi wa dunia na watu wote kama nilivyosema hapo awali, mimi si chochote wala si kitu mbele za huyu Bwana. Sasa iweje tena kuwa mimi niwe mkombozi?” Nikasisitiza kukataa.

Ninajua mambo ninayokuambia ni mazito zaidi ya akili yako na hekima zako. Wewe kubali tu cheo hicho”. Yule bibi aliendelea kusisitiza baada ya kunidadisi usikivu wangu. Kisha akaendelea kunielezea historia ya eneo hili. Alidai kuwa hapo zamani watu wote wa dunia hii waliishi eneo hili. Hapakuwa na ubaguzi wa aina yoyote, weupe, weusi, manjano; wote walishirikiana, walikuwa wakitumia lugha moja.

Shughuli kuu enzi hizo zilikuwa kilimo na ufugaji wa wanyama wa aina zote; ng’ombe, mbuzi, kondoo, farasi, kuku, bata na wanyama wa aina mbalimbali, yule bibi aliendelea kunihadithia.

Siku moja vijana walipofungulia mifugo yao na kwenda kuchunga eneo fulani walishangaa kuona eneo hilo kumeota boga lililostawi vizuri. Wakashangaa na kuitana ili wenzao nao waje kushuhudia maajabu ya kukuta boga limeota sehemu ambayo siku chache tu zilizopita hapakuwa na dalili zozote za kuota mmea wa aina hiyo sehemu hiyo, walishangaa sana.

Wakawa wanasemezana wao kwa wao wakisema: “Limeota boga” kwa mshangao wao, lile boga nalo likawakariri maneno yao likasema: “Limeota boga”. Mshangao wa wale watoto ukaongezeka na wakazidi kusemezana wao kwa wao. “Tena linaongea,” Lile boga nalo likawakariri tena kauli yao. “Na tena linaongea.”

Wale watoto wakacheka kwa mshangao. Na lile boga likacheka pia, watoto wakaendelea kuliuliza lile boga. “Wewe unaitwa nani?” Lile boga nalo likakariri maneno yao kama hapo awali. “Wewe unaitwa nani?”  Wakacheka na lenyewe likacheka tena kama walivyofanya wale watoto.

Siku hiyo watoto waliporudi nyumbani waliwasimulia watu kuhusu maajabu ya boga linalozungumza na kucheka kama watu. Kesho yake watu wote wakaenda kushuhudia boga hilo la ajabu. Siku hiyo lilikuwa limeongezeka zaidi na limeota maua mazuri na lilikuwa limestawi zaidi ungedhani lilikuwa linamwagiliwa maji na mtu fulani.

Habari hizi zikaenea sehemu zote. Siku moja watu wote wa sehemu hizi walikwenda kushuhudia miujiza ya boga la kuongea kama watu. Bibi huyu aliendelea kunisimulia kwa machungu. Habari za boga zikavuma na watu wengi wakazidi kuvutiwa na maajabu haya. Siku moja lile boga liliwaaga watu kuwa eti linataka kurudi nyumbani kwao, kwa hiyo lingependa watu wote waende ili liagane nao na liliwaahidi kuwapatia zawadi kemkemu kadiri ya matakwa yao.

Mimi siku hiyo nilikuwa na tumbo la kukimbia kimbia na mtoto wangu Masalakulangwa alikuwa hajiwezi, kwa hiyo sikwenda. Mungu wangu! Kumbe lile boga lilikuwa zimwi. Ghafla lilibadilika likawa ‘limnyama’ likubwa ajabu na kufumba na kufumbua likawameza wanyama wote, watu wote, ndege wote na likameza mazingira ya eneo hilo!

Baadaye ikawaje baada ya watu hawa kumezwa?” Nikamuuliza. Baada ya kiama hicho, lile ‘limnyama’ lilitokomea porini mpaka baada ya miaka mingi sana. Kijana wangu Masalakulangwa alipokua alianza kuniulizauliza kuhusu asili ya magofu mengi na kutoona watu licha ya mimi na yeye.

Mwanzoni yule bibi alisema kuwa hakutaka kumwelezea ukweli kijana wake. “Lakini kero ilipozidi ikabidi nimsimulie kama nilivyokusimulia wewe Bugulugulu,” Bibi alizidi kunielezea.

“Baada ya muda wa siku nyingi na maswali mengi ya huyu mziwanda wangu, niligundua kuwa nikizidi kumficha ndivyo atakavyozidi kutaka ukweli,” aliongeza. Sasa nikamuuliza kuwa yeye alikuwa na mawazo gani? Aliniambia tena kwa kujiamini kuwa eti ni lazima kufanyike jambo fulani. “Ni lazima kufanyike jambo,” Masalakulangwa alizidi kusisitiza.

Alienda mbali hadi kudiriki kusema eti ni “ujinga nguvu nje ya nguvu za binadamu kutawala dunia hii. Haiwezekani!”

Na juu ya hiyo, eti alikuwa anadai kuwa alitaka kupambana na “dubwasha” hilo. Hata kama lingemshinda kwani angepoteza nini? Hakuwa na rafiki kuwa atampoteza! Hakuwa wala anamiliki radio, wala TV, wala hakuwa anamiliki nyumba aliyoijenga mwenyewe. Hakuwa na baiskeli, pikipiki wala mali, hana mtoto wala mke.

Sina kitu nitakachopoteza lile dubwasha likinishinda mama yangu. Sana sana nitapoteza roho  yangu tu. Sasa roho yangu ikipotea kutakuwa na hasara gani? Je, ni nani ajuaye kwa dhati roho huenda wapi baada ya kifo? “Aliyeiweka roho ndani yangu atajua pa kuipeleka.” Kijana wangu huyu alikuwa anasema kila mara.

Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose sehemu ya saba yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa Na. 0755629650.