Mwanaharakati Martin Luther King Jr amewahi kusema, “Nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzingo mzito sana ambao haubebeki.’’

Katika jamii yetu tunayoishi, tumeshuhudia au tumekutana na tunaendelea kukutana na watu ambao hawana furaha katika maisha yao. Tunakutana na watu wanaojilaumu na kuwalaumu wengine.

Tunakutana na watu wanaotamani kujiua. Tunakutana na watu ambao wanahisi jamii imewatenga. Tatizo ni nini? Tuwasaidieje watu hawa? Tunao wajibu mkubwa wa kuwasaidia watu hawa. Tusiwatenge.

Tuwaonjeshe joto letu la upendo. Tuwaoneshe uso uliojaa tabasamu na matumaini. Kwa sababu watu hawa ni ndugu zetu, ni majirani zetu, ni watoto wetu. Jibu la upendo ni upendo. Dunia inahitaji upendo ili mambo mengine mazuri yawezekane.

Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake wapendane. Aliwaambia hivi, “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yoh. 15:12-13).  

Mwandishi Friedrich Rucket anafundisha hivi, “upendo ni kitu kikubwa sana ambacho Mungu anaweza kutupa, na kitu kikubwa ambacho tunaweza kumpa Mungu.’’

Upendo ni sauti ambayo kiziwi anaweza kuisikia na mwanga ambao kipofu anaweza kuuona. Tupendane. Kwa nini tunahitajika kuishi maisha yanayoongozwa na upendo?

Kwanza ni kuishi vizuri. Tukipendana tutaishi vizuri. Tutaelewana. Tutaonyana kwa upendo. Tutasameheana. Tutashauriana vizuri. Tutasaidiana. Dunia ina njaa ya upendo.

Familia nyingi zina njaa ya upendo. Palipo na vita ya kidini kuna njaa ya upendo. Palipo na vita ya kikabila kuna njaa ya upendo. Palipo na vita ya kisiasa kuna njaa ya upendo.

Mwalimu Julius Nyerere alijua kwamba ili taifa la Tanzania liwe na umoja, lazima mbegu ya upendo ipandwe. Nyerere alipanda mbegu ya upendo Tanzania kwa kivuli cha ujamaa.

Leo hii taifa la Tanzania watu wake wanaelewana kwa kuzungumza lugha moja (ya Kiswahili). Ni kwa msingi huo, Mkurya anamuoa Mchagga na wanaishi maisha ya upendo, Msukuma anaolewa na Mnyiramba na wanaishi vizuri.

Hizi ni juhudi za Mwalimu Nyerere. Aliwaunganisha Watanzania wakawa kitu kimoja. Kwa tafsri fupi ni kwamba Mwalimu Nyerere alifukuza njaa ya upendo Tanzania kwa kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja.

Tufukuze njaa ya upendo kwenye familia zetu kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye nyumba zetu za kitawa kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye nyumba zetu za ibada kwa kupendana.

Tufukuze njaa ya upendo kwenye jamii yetu kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye kazi zetu kwa kupendana. Kuna watu wanahisi kwamba wanaishi hapa duniani kimakosa kwa sababu tu wana njaa ya upendo.

Kuna baadhi ya wanandoa wanahisi ndoa ni msalaba wa zege kwa sababu tu ndani ya ndoa zao hakuna harufu ya upendo.

Martin Luther King Jr amesema, “nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzingo mzito sana ambao haubebeki.’’ Upendo ni mzigo mwepesi ambao unabebeka. Chuki ni mzigo mzito ambao haubebeki.

Nani anafahamu mzigo wa chuki? Pengine unaweza ukawa hufahamu mzigo wa chuki. Niulize nikwambie. Chuki ni sumu isiyo na tiba ya kisayansi wala tiba ya kiasili. Tiba ya chuki ni upendo. Njia rahisi ya kuepuka chuki ni kuishi maisha ya upendo.

Maisha ni upendo. Maisha yanazungumza katika upendo. Ukitaka kuuona upendo, ishi upendo. Uruhusu upendo uyatawale maisha yako. Usiruhusu hata siku moja ipite pasipo kupanda mbegu ya upendo wa kweli, upendo usio wa kinafiki, upendo utokao moyoni na upendo ushindao majaribu.

Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake kwa nasaha hii, “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi’’ [Yn 13:34]. Ni lazima tujitahidi kuyajenga maisha yetu katika msingi wa upendo. Furaha kamili ipo katika kuishi maisha ya upendo.

Ulimwengu wa leo unahitaji kuhubiriwa namna mpya ya kuishi maisha ya upendo. Ni hatari watu wa ulimwengu kuishi bila upendo. Bila kuishi maisha ya upendo, dunia yetu itageuka kuwa jehanamu.

Mungu hutabasamu pale anapoona mwanadamu anaishi maisha ya upendo. Nafsi yako haiwezi kuwa na amani kama haipendi wala kupendwa. Njia bora ya kuishi ni kuishi maisha ya upendo.

Namna bora ya kupendwa ni kupenda. Jaribu kumtumikia Mungu kwa kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo, sambamba na hilo sambaza mbegu ya upendo kwenye jamii ya walimwengu.

Kila binadamu aliumbwa na Mungu, lakini si kila mmoja ni mtoto wa Mungu. Njia pekee ya kuhesabika kuwa mtoto wa Mungu ni kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Jina lingine la Mungu ni ‘Upendo’.

Inafahamika kwamba, upendo ni jina la Mungu. Na ‘majivuno’ ni jina la shetani. Huwezi ukaishi maisha yanayotawaliwa na ‘upendo’ ukaitwa mtoto wa shetani, utaitwa mtoto wa Mungu.

Hali kadhalika, huwezi ukaishi maisha yanayotawaliwa na majivuno ukaitwa mtoto wa Mungu, utaitwa mtoto wa shetani. Maandiko Matakatifu yatujuza, “Mungu ni upendo naye akaaye katika pendo hukaa ndani ya Mungu’’ (1 Yohana 4:16).

Tunatakiwa kujenga na kukuza tabia ya kupendana katika maisha yetu. Baraka ya watu wema katika jamii, familia, taifa ni upendo. Upendo ndiyo zawadi aliyonayo kila mtu na  ambayo anaweza kuitoa na kuipokea bila masharti.

Jamii bora haijengwi kwa tofali wala fedha, jamii bora inajengwa kwa upendo. Familia bora inajengwa kwa upendo. Bahati nzuri ni kwamba kila siku kuna sauti inatuambia, ‘Pendaneni’. Sauti hiyo ni hii, “Nawapeni amri mpya…. pendaneni kama nilivyowapenda” [Yn 13:34].

Jibu la upendo ni upendo. Hakuna tabia yoyote inayoweza kuyageuza maisha yako yavutie kama ua la jasmine zaidi ya tabia ya upendo. Ukipenda, utapendwa.

Usipopenda huwezi ukapendwa. Penda, upendwe. Wapo watu wanaishi na majirani zao kama paka na panya. Hawaelewani. Hawasalimiani. Hawataki hata kuonana uso kwa uso.

Wanapishana njia. Mwandishi George MacDonald anashauri hivi, “Upendo kwa jirani yako ndiyo mlango pekee wa kutoka kwenye gereza la ubinafsi.’’ Ndugu msomaji, unapata faida gani unaposhindwa kusalimiana na jirani yako?

Upendo ni marashi. Wapulizie wenzako marashi ya upendo. Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine wawe na furaha. Mtawa wa Kanisa Katoliki, Mother Teresia wa Kalkuta, anafundisha hivi, “Sambaza upendo kila mahali unapokwenda. Mtu yeyote asije kwako bila kutoka akiwa na upendo na furaha.”

Matumizi mazuri ya maisha ni upendo

Maisha bila upendo hayana thamani. Wakati mzuri wa kupenda ni sasa. Kwa nini sasa ndiyo muda mwafaka wa kupenda? Kwa sababu hujui utakuwa na muda wa kuishi mpaka lini. Mazingira hubadilika. Watu hufa. Watoto hukua.

Huna dhamana ya kesho. Kama unataka kuonesha upendo ni bora uoneshe kuanzia sasa. Mwanafalsafa wa Dernmark, Soren Kierkegaard, anasema, “mara unapozaliwa katika ulimwengu huu tayari u mzee wa kutosha kuweza kufa.’’

Tusikubali kufa tukiwa bado tunadaiwa deni la upendo. Unapotamani kuishi, tamani kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Maisha yako yawe na chapa ya upendo.

Upendo ni kutoa na kupokea. Ilikuwa ni saa nne kamili za asubuhi Desember 23, 1923, Mwanadada Sophie Hone alipouawa. Sophie Hone aliuawa kwa kutetea haki za watoto katika mji wa Dunmore.

Katika kitabu chake cha kumbukumbu, Sophie Hone alikuwa ameandika maneno haya, “kusudi la maisha yangu ni kupenda.’’ Chukua muda kutafakari kusudi la maisha yako.

Wamebarikiwa wenye maisha ya kupenda na kupendwa. Matumizi bora ya maisha ni kupenda.Tumeumbwa kupenda na kupendwa. Hatuwezi kuishi bila kupenda na hatuwezi kuishi bila kupendwa.

Tarehe 8 September, 1890, Mt. Theresia wa Mtoto Yesu, alifunga nadhiri zake za kwanza za utawa katika Shirika la Karmel. Mtawa Theresia baada ya kufunga nadhiri alisali sala hii, “Ee Yesu mimi siombi kitu kingine, ila tu upendo.’’

Mt. Theresia anajulikana kwa jina jingine kama, “Ua la upendo.’’ Moyo wenye upendo ni moyo uliojaa fadhila za utakatifu.

Upendo ni uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.  Padre Karol wa Foucauld February 27, 1903, alimwandikia barua  Mgr. Guerin.

Sehemu ya barua yake ilisomeka hivi, “Naililia Injili ya upendo’’.  Upendo ni Injili. Padre Karol wa Foucauld anasema, “Msingi wa ndani wa mioyo yetu, unaamuru kila mtu ampende jirani yake.

Kwa maneno mengine mpende kila binadamu kama unavyojipenda wewe mwenyewe’’.

7714 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!