“Shukrani ni fedha ambayo tunaweza kujitengenezea sisi wenyewe na kuitumia bila kuogopa kufilisika.”

– Fred De Witt Van Amburgh

Siku moja kipofu alikuwa anasafiri. Akakutana na barabara mbaya sana. Akasimama akawaza sana. Akajiuliza nitawezaje kusafiri katika barabara mbovu kiasi hiki wakati sioni?  Pembeni ya barabara kulikuwa na mlemavu ambaye naye alikuwa anataka kusafiri.

Kipofu alisimama kwa muda huku akiwaza ni namna gani atasafiri. Mlemavu akamwita kipofu na kumuuliza unakwenda wapi? Kipofu akajibu, ninasafiri. Kipofu akamwimbia mlemavu: “Niongoze katika ugumu wangu.” Mlemavu akajibu: “Nitawezaje wakati na mimi ni mlemavu hata kujivuta siwezi?” Lakini kama utanibeba nitakutahadharisha na chochote kibaya njiani, macho yangu yatakuwa macho yako, na miguu yako itakuwa miguu yangu.

Kipofu akajibu akasema: “Inafaa tusaidiane.” Kwa hivyo akamchukua rafiki yake mlemavu mgongoni, wakasafiri umbali mrefu kwa usalama, furaha na amani. Mwisho wa safari kipofu akamwambia mlemavu, kwa hakika shukrani ni msaada katika maisha! Nakushukuru sana.

James E. Faust anateta: “Moyo wenye shukrani ni mwanzo wa ukubwa. Ni kielelezo cha unyenyekevu. Ni msingi wa kuendeleza fadhila kama sala, imani, ujasiri, kuridhika, furaha, upendo na ustawi.” Maisha bila shukrani hayana ladha. Mambo makubwa tunayotamani kuyapata pamoja na mafanikio tunayonuia kuyapata yamejificha ndani ya neno ‘shukrani’. Fungua mlango wa baraka katika maisha yako kwa shukrani. Kushukuru ni kuomba tena. Asiyeshukuru leo, kesho akiomba ni vigumu kupewa na akipewa atapewa kidogo. 

Kuna baba mmoja hukoJamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alikuwa anatembea kando ya Ziwa Tanganyika na mtoto wake wa kiume. Mara likaja wimbi kubwa sana likamchukua mtoto wake huyo aliyeitwa JERRY. 

Akapelekwa mbali sana na lile wimbi. Kulikuwa na mvuvi mmoja karibu na lile wimbi. Yule mvuvi akaogelea kumfuata huyo mtoto. Huyo mvuvi msamaria mwema alijitolea hata bila kuwa na mahusiano au kujuana na huyo baba Jerry.

Baada ya kumwokoa yule mtoto bado akiwa hai na kumleta kwa baba yake kulitokea mshangao wa ajabu sana. Badala ya kumshukuru baba wa mtoto huyo alimuuliza mvuvi, mtoto wangu alikuwa na kofia umeiweka wapi? Hakika mvuvi alikosa cha kusema kwani alitambua dhahiri kwamba, baba Jerry hana shukrani. Je, mtoto angekufa na ile kofia ikapatikana ingekuwaje?

Mwanafalsafa William Arthur Ward anasema yafuatayo juu ya shukrani: “Shukrani inaweza kubadili siku za kawaida kuwa siku za shukrani, kubadili kazi za kila siku kuwa furaha, na kubadili fursa za kawaida kuwa baraka.” Mpendwa msomaji na rafiki yangu mwema, tujifunze kushukuru katika maisha yetu. Ukipata shukuru, ukikosa shukuru. Ukishinda shukuru, ukishindwa shukuru. Ukiwahi shukuru, ukichelewa shukuru. Ukiwa na afya shukuru, ukiugua shukuru. Ukisifiwa shukuru, ukikashifiwa shukuru. Ukifurahi shukuru, ukiwa na huzuni shukuru. Ukishiba shukuru, ukiwa na njaa shukuru. Ukiwa na raha shukuru, ukiwa na shida shukuru. Shukuru kwa yote, shukuru popote, shukuru kwa lolote, shukuru kwa yeyote.  Na kwa namna yoyote njema, shukuru. 

Ukweli ni kwamba, tunapaswa kushukuru kwa kila jambo jema katika maisha yetu. Mwandishi Dorris Day anasema: “Shukrani ni utajiri na malalamishi ni umaskini.”

Nitakuwa sahihi kabisa nikisema kwamba, kutoa shukrani ni tendo la ‘unyenyekevu’ lakini pia ni jambo ambalo linalochochea fadhila. Kukosa shukrani ni alama ya kiburi. Tafakari jambo hili: Unashindwaje kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyekuumba kwa sura na mfano wake? Unashindwaje kumshukuru mke/mume wako kwa ushirikiano wake mzuri anaokuonyesha? Unashindwaje  kuwashukuru wazazi wako kwa zawadi ya malezi bora waliyokupatia? Unashindwaje kumshukuru jirani yako kwa uwepo wake? Wahenga walisema: “Asiye na shukrani ni mtumwa.” Jifunze kutumia maneno ya  shukrani  katika  maisha yako. Shukrani ni wajibu.

Timiza wajibu wako kwa kutoa shukrani. Mwandishi Fred De Witt Van Amburgh anasema: “Shukrani ni fedha ambayo tunaweza kujitengenezea sisi wenyewe na kuitumia bila kuogopa kufilisika.” Mwanafalsafa wa Marekani Wiliam Arthur Ward yeye anasema: “Kujisikia kutoa shukrani na kutoitoa ni kama kuandika barua na kutaka kuituma kwa mhusika halafu unahairisha.”

Duniani hakuna majonzi ambayo mbingu haiwezi kuyaponya. Tujiponye majeraha tuliyonayo kwa kushukuru. Mbele ya mbingu yote yanaponyeka. Yawezekana hubarikiwi katika maisha yako kwa sababu umeshindwa kutoa shukrani ya dhati ya kile kidogo ama kikubwa ulichonacho.

By Jamhuri