Yamesemwa mengi baada ya mzee Arhard Felician Muhandiki kukatwa mguu kutokana na maradhi yaliyompata. 

Kuna baadhi ya watu walifurahia sana tukio hilo wakidhani kuwa hiyo itakuwa nafuu kwao kwa jinsi alivyokuwa amewakalia kooni katika walichokiona kama fursa kwao.
Kwa muda mrefu Muhandiki alijitoa kama mpambanaji wa kunusuru mali ya ushirika iliyokuwa ikipotea kama mali isiyokuwa na mwenyewe. Amepambana sana na wahujumu hao wa uchumi, kiasi cha wahusika kuanza kumuombea mabaya yamkute ili wao wanusurike.
Kwa hiyo walikiona kitendo cha yeye kukatwa mguu kama baraka kwao, wakidhani kuwa kitakuwa kimempunguzia makali aliyokuwa nayo dhidi yao.

Lakini lililotokea halikumrudisha nyuma mzee huyu. Hata baada ya masaibu yaliyompata Muhandiki bado anaona haiwezekani kuwaachia wahujumu uchumi hao waondoke na mali za ushirika na kuwaacha wananchi wakishangaa kama mabwege.

Anasema kwa vyovyote iwavyo ni lazima kieleweke, wahusika wapelekwe kunakohusika na kuyajibu yote yanayowakabili. Tena anaongeza kwamba kinachofikiriwa kilichukuliwa katika uhujumu unaotajwa akijatazamwa kiusahihi, kwa vile aliweza kufika jikoni na kujionea kinachopikwa kule, kwa hiyo ana uhakika kwamba kinachotajwa ni kidogo sana, kisichofikia hata robo ya kile kilichopotea kiuhalisia.

Hiyo inaleta picha kwamba Muhandiki amepania kiuhakika kuwapigania wananchi wenzake kwa njia mbalimbali. Hiyo inapaswa iondoe dhana iliyokuwepo kwamba naye pia alikuwa akitafuta nafasi ya kuwa kiongozi wa ushirika wa KCU (1990) Ltd ili ajinufaishe binafsi.

Ambacho wabaya wa Muhandiki wasichokifahamu ni dhana yao kuwa kwa kupoteza mguu mmoja Muhandiki atakuwa amepoteza sehemu ya akili zake. Inawapasa kufahamu kuwa masuala ya ushirika si kama mpira wa miguu ambao mtu akipoteza kiungo kama mguu watu wanaweza kujiuliza atauchezaje mpira? Hapa kinachotumika ni akili tu, kwa maana ya kichwa wala si miguu.

Kwa hiyo waliodhani Muhandiki amekwisha, kama maneno yanayoendelea kwa sasa kuwa machachari yake yamekwisha, wajue imekula kwao. Mapambano bado ni yaleyale.

Hiyo ni kwa sababu Muhandiki hafanyi kitu hata kama ni cha kwake binafsi kwa kujiangalia yeye tu, bali anaitazama jamii yote inayomzunguka.

Ni vigumu kuyaita mafanikio yake kuwa ni ya kwake peke yake, ila inafaa yaonekane ni mafanikio ya jamii nzima. Mifano ni mingi inayolishadidia hilo.

Ni kama alivyokuwa akiwalipia watoto kusoma shule kule nchini Uganda ili wakapate elimu nzuri kusudi baadaye waje kufanya mambo yaliyo bora kwa familia zao. Si kwamba amewasomesha watoto wake tu, ila hata wa ndugu zake, wajukuu zake na wa marafiki walio karibu.

Inawezekanaje mtu wa aina hiyo akafanye ufisadi wa mali ya umma kama ilivyo kwa kitu cha jumuiya kama ushirika? Kwa kila mtu anayetafakari vizuri anaweza kuona kuwa hilo ni jambo lisilowezekana.

Mtu anayetoa pesa zake binafsi kuchangia mambo mbalimbali ya kijamii kuanzia kanisani, kwenye mambo ya maendeleo kijijini kwake, kwenye kata hata tarafa kuhakikisha jamii inainuka na kusonga mbele, akiwa hatafuti lolote la ziada, na bila kutaka kujitangaza kuwa ni yeye amefanya hivyo, kumsema mambo ya aina hiyo si kumkatisha tamaa tu, bali ni kufuru hata kwa Mwenyezi Mungu.

Nijaribu kutaja kitu nilichokiona mimi kwa macho yangu. Siku moja tulikuwa pamoja kwenye gari lake, tulipofika sehemu fulani karibu na Hospitali ya Misheni ya Kagondo gari likapata pancha. Akasema tutafanyaje? Kwa mbali kidogo tukawaona vijana wa bodaboda akaniambia niwaite. Alitaka kuwatuma waende sehemu fulani ambako kuna gereji ya magari wawaite mafundi waje kutengeneza pancha.

Vijana walipofika na kujua tatizo lililopo wakauliza mzee hauna vifaa? Akawajibu anavyo. Basi vijana hao wakafungua tairi moja na kuweka lile la akiba. Furaha aliyokuwa nayo mzee yule akaamua kuwapatia pesa yote ambayo wangeendea kuwaita mafundi na ambayo angewapatia mafundi pamoja na nauli yao. 

Vijana hao walifurahi sana na kumtania kwamba labda waombe kila akifika pale apate pancha! Maana walisema tangu asubuhi ile mpaka muda huo, mwendo wa saa kumi jioni, walikuwa hawajafanya shughuli yoyote, na yeye aliwalipa pesa ya siku nne wanayopaswa kupeleka kwa mabosi wao wenye pikipiki.

Kumsema mtu wa aina hiyo kuwa analenga kuhujumu pesa ya wakulima – wana ushirika ni kitu gani kama si kumkufuru Mungu?

prudencekarugendo@yahoo.com
0654 031 701

685 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!