Vijana ni wajenzi, wachafuzi wa nchi

Vijana ni nguvu kazi na viongozi wa taifa lolote duniani. Ni walinzi na wana utamaduni wa nchi yoyote duniani. Sifa ambazo wanazo tangu zama hadi sasa. Lakini kihistoria na kisiasa inaeleweka wajenzi wakubwa wa dunia ni vijana na wachafuzi wakubwa wa dunia ni vijana. Sifa zote hizi ni zao.

Vijana wanatambulika na wanaaminika wanayo mawazo mapya na upendo mkubwa kwa watu mbalimbali duniani. Vijana wanapenda kuhangaika, yaani kufanya harakati hapa na pale kutafuta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika taifa lao, kwani mabadiliko kwao ni muhimu.

Wanapofanya harakati zao wanapata mambo mengi, iwe katika kufanya kazi, katika medani za ulinzi na usalama au katika majadiliano ya kisiasa na kadhalika. Wanapofanya haya na kufanikiwa au kutofanikiwa wanavuna ujuzi, wanapata heshima kutokana na kuona, kuelewa na kusoma maandiko.

Mambo wanayokutana nayo yanawapa kiburi, uthubutu na ujasiri kufanya ujenzi wa dunia kuwa salama na amani, au kufanya uchafuzi wa dunia kuwa katika shaka na wasiwasi mkubwa. Na ndipo tunaposema: “Ujana maji ya moto, hufika muda yakapoa.”

Kutokana na harakati zao, Waswahili tunasema: “Ujana una tegemeo, uzee una kumbukumbu.” Fasili ya methali hii ni kwamba, mtu akiwa kijana ana nguvu na uwezo, hivyo anategemewa kufanya mengi na afikiapo uzee hazina aliyonayo ni kumbukumbu za aliyoyatenda wakati akiwa kijana.

Hapa Tanzania tunao vijana wengi katika taaluma na fani mbalimbali ambapo wazee tunawategemea wao kwa huduma na malezi bora. Hekima zao na ujuzi wao ili waweze kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kupitia harakati za kisiasa kwa lengo la kuweka usalama na amani ya taifa letu.

Kijana ni mwanaharakati na mwanaharakati anahitaji mabadiliko. Je, ni mabadiliko ya aina gani muhimu kwa kijana ambayo kwayo anatakiwa kuyaleta hapa nchini? Ni mabadiliko ya kusema ukweli, uthubutu na ujasiri wa nafsi, uwezo na nia ya ujenzi wa nchi kiuchumi na kijamii.

Tanzania ni nchi huru na watu wake ni huru. Sifa ya mtu huru ni kusema ukweli. Watanzania ni wema, wakarimu na waungwana. Hawapendi fujo. Ustaarabu wao uko katika nguvu za hoja na mazungumzo yao yenye kutoa uamuzi mwafaka juu ya ujenzi na malezi ya taifa lao.

Kijana wa Tanzania kuwa na uthubutu, nguvu na uwezo usikufanye ujenge mazingira ya uasi. Kwa maana ya uvunjaji wa sheria kwa nia ya kujaribu kubadili mfumo wa kisiasa wa nchi au kuwapinga wenye mamlaka au kupinga sheria na taratibu zilizopo. Unapofanya haya hujengi Tanzania bali unaichafua Tanzania.

Uasi unakuchochea kufanya vita, tukio ambalo si salama kwako, ndugu zako na kwa jamii za wengine. Vita haina faida, ina hasara na janga kwa taifa. Ujuzi na hekima uliyonayo bado na haitoshi kukupa nguvu kufanya uamuzi wa jambo linalofaa, lazima uwe na busara kuepuka maovu haya.

Vijana si busara kudiriki kunena: “Nikifa basi!” Ni kweli ukifa basi. Kwa vile kufa ni lazima. Lakini usife kwa kutaka ufe. Ni dhuluma ya uhai na nafsi yako, ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu. Usife kwa kukamatwa ugoni, wizi, uongo na kadhalika, ni kosa kwa Mungu.

Vijana wanasikika wakisema: “Tusiogope kufa katika kutafuta haki.” Hii ni kauli ya kiharakati ambayo inahitajiwa fasili na tafakuri pana kabla ya kuitekeleza. Haki gani, kutoka kwa nani na kwa manufaa ya nani? Ikumbukwe kauli ni bora kuliko mali.

Vijana wanapoeleweka kihistoria na kisiasa ni wajenzi wakubwa wa dunia ni pale wanapofanya uamuzi wa busara katika kujenga nchi au taifa lao, wa kufanya kazi kisayansi na kiteknolojia kuinua uchumi, kulinda mali na mipaka ya nchi, kuthamini na kuenzi utamaduni wao wakitumia akili na elimu yao.

Aidha, wanapoeleweka ni wachafuzi wakubwa wa dunia ni pale wanapokosa uaminifu na uadilifu, si wakweli na wenye nidhamu ya woga mbele ya viongozi wao, washauri wao. Na kufanya uamuzi wa ovyo. Hasa wanapowakiri maadui wa taifa lao ndio watu wenye hekima na busara. Na wao wenyewe kutii hawana tafakuri makini.