Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kusema wiki hii nitaangalia taratibu na viwango vya kodi wanazolipa wafanyakazi walioajiriwa katika kampuni, taasisi au shirika, kisha ikiwa nafasi itaruhusu nitajadili kodi ya mashirika.

Sitanii, kabla ya kuangalia kodi hizi naomba uniruhusu mpendwa msomaji nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango. Ni kwa muda mrefu sijasikia serikali ikiwasilisha mapendekezo ya bajeti bungeni bila kuongeza kodi kwenye soda, bia, mvinyo na sigara.

Kwa hakika uchumi wetu ulidumaa kwa sababu moja kuu ya msingi. Kwa miaka mingi tulilenga vyanzo rahisi na dhaifu vya mapato. Hatukujielekeza katika uzalishaji kuwa na vyanzo vipya vya mapato. Biashara tulizipa kisogo, tukadhani nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi, ilhali fedha za kodi zinatokana na biashara.

Katika makala za awali, nilieleza tatizo lililokuwapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukadiria mtu mapato kabla hajaanza biashara. Bajeti ya mwaka huu imenifurahisha kwamba kwa kuanzia imeweka utaratibu wa mtu anayeanzisha biashara kufanya biashara angalau kwa miezi sita, kisha ndipo aende kuandikisha biashara na utaratibu wa kukadiriwa kodi kufanywa.

Hakika hili ni jambo jema kwa ustawi wa biashara katika nchi yetu. Watu wengi wamekuwa wakishindwa kuanzisha biashara kwa kudaiwa kodi kabla ya kuanza biashara. Serikali pia imefuta kodi 54 katika sehemu mbalimbali za biashara, ambazo zilikuwa kero kubwa kiasi baadhi ya viwanda vikashindwa kujiendesha.

Sitanii, ingawa nafahamu wenye viwanda bado wanayo madai yao ya msingi, kama utitiri wa taasisi zinazothibitisha ubora wa bidhaa na mazingira ya kazi kama TBS, OSHA na nyingine, ambazo mwisho wa siku zinakuwa kero kwa wafanyabiashara, lakini hatua zilizochukuliwa na serikali na kuanza kueleza wazi nia ya kulea na kukuza biashara, basi nchi hii itapiga hatua kubwa.

Nimeeleza awali kuwa leo ningezungumzia taratibu na viwango vya kodi wanazolipa wafanyakazi walioajiriwa katika kampuni, taasisi au shirika, kisha ikiwa nafasi itaruhusu nitajadili kodi ya mashirika.

Kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata

Kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE) ni kodi ya zuio inayotozwa kwenye mapato ya mfanyakazi (mshahara). Chini ya mfumo huu, kodi hii inatozwa kwa mwajiriwa kutoka kwenye mshahara au ujira wake.

Unapozungumzia waajiriwa, kisheria unazungumzia wafanyakazi wenye mikataba ya kudumu, muda mfupi, mameneja, wakurugenzi na vibarua. Mwajiriwa anaweza kuwa ameajiriwa na mtu mmoja au wakala wa mwajiri. Kwa mfano mtu anayefanya usafi kwenye jengo fulani, anakuwa na vibarua wanaolipwa ujira wao, basi hawa nao wanapaswa kulipa kodi husika kwa mujibu wa viwango vilivyoainishwa.

Mapato yatokanayo na ajira

Mapato yote yatokanayo na ajira kutoka kwa mwajiri kwenda kwa mwajiriwa yanapaswa kulipiwa kodi. Sheria imeainisha bayana kuwa mapato haya yanajumuisha:-

a)   Malipo ya ujira, mshahara, malipo ya likizo, ada, kamisheni, bonasi, kiinua mgongo, fedha za kujikimu za ukarimu au malipo yoyote yatokanayo na kuajiriwa au kutoa huduma.

b)  Marejesho yanayotokana na matumizi aliyofanya mtumishi au mshirika wa mtumishi huyo.

c)    Malipo yoyote ya kimkataba.

d)  Michango ya, na malipo ya kustaafu.

e)   Malipo ya kupunguzwa kazini.

f)    Malipo yoyote yanayotokana na ajira ikiwamo ukarimu kwa mujibu wa kanuni.

g)   Malipo yoyote yanayoweza kutakiwa kuingizwa katika orodha hii.

h)  Malipo ya ukurugenzi ya ada ya mwaka inayolipwa kwa mkurugenzi asiyekuwa wa muda wote.

Wiki ijayo nitazungumzia malipo yasiyotozwa kodi na viwango vya kodi anazopaswa kulipa mfanyakazi. Usikose nakala yako ya Gazeti la JAMHURI kila Jumanne.

632 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!