Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kueleza taratibu na kiwango cha kodi wanachopaswa kulipa wafanyabiashara wanaofanya biashara yenye thamani zaidi ya Sh milioni 20. Niliahidi kueleza taratibu za jinsi ya kutunza kumbukumbu na muda wa mtu kuwasilisha marejesho yake ya mapato kwa Kamishna wa TRA katika mwaka katika makala hii.

Sitanii, kabla sijaenda mbali nikugusie jambo moja ndugu msomaji wangu. Mimi nimepata fursa kwa siku nilizopo hapa Uswisi. Hakuna baridi. Wenyeji wananiuliza nimefanyaje kuepuka mabarafu. Ila safu za milima zimejaa mabarafu kila kona. Kama kawaida wakati wa kiangazi hapa Uswisi jua linawaka hadi saa 04:00 usiku na kuzama, kisha linachomoza saa 09:00 alfajiri.

Nimepata fursa ya kuwa katika miji mitatu sasa; Geneva, Berne na sasa Zurich. Hakika wenzetu wamejenga miundombinu. Barabara za lami zipo hadi mashambani vijijini kuepusha mahindi, mpunga, ngano, mchicha, kabeji au mazao yoyote unayoyafahamu kufika sokoni na vumbi. Sisi tuking’oa mchicha tunakung’uta vumbi, tunapitisha kwenye maji tunapika, kwa Uswisi mchicha wenye vumbi au tope hauna soko!

Nitaandika makala ya niliyoyashuhudia nikirejea, ila kwa sasa nirejee kwenye somo la kodi. Makala yangu inasema: “Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania.” Nimeendelea kupata mrejesho kupitia e-mail yangu, ujumbe wa simu ya mkononi na uso kwa uso hadi nimebaini tuna tatizo katika biashara.

Sitanii, nimepata taarifa za Rais John Magufuli kumtumbua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere. Kimsingi niseme sikuumia. Huyu bwana hakutaka hata kuwa na simu ya mwandishi wa habari yeyote. Alikuwa bwana mkubwa kweli. Mara kadhaa tumemweleza kodi inavyokwepwa au kubambikwa kwa watu, lakini akaweka pamba masikioni. Amevuna alichopanda.

Muda wa marejesho ya mapato

Mtu binafsi anayefanya biashara yenye mzunguko wa hadi Sh milioni 20 kwa mwaka na analipa kodi kwa kukadiriwa hana wajibu wa kupeleka marejesho ya kodi kisheria. Anapaswa kulipa makisio yake kila miezi mitatu iwapo yanazidi Sh 50,000 kama alivyokadiriwa.

Nieleweke pia kuwa mfanyabiashara ambaye biashara yake inazidi Sh milioni 20 kwa mwaka, huyu kama nilivyoeleza kuwa anapaswa kuandaa hesabu, basi huyu anapaswa kupeleka marejesho ya kodi kila miezi sita.

Hata hivyo, kwa ruhusa ya Kamishna anaweza kuongeza muda wa kupeleka marejesho zaidi ya muda huo wa kisheria. Uamuzi huu wa kuongezewa muda, Kamishna anaweza kuufikia baada ya kupata barua ya maombi kutoka kwa mlipa kodi na atampa masharti mahususi na muda wa kufanya marejesho.

Mambo muhimu unapojaza fomu

Mlipakodi anapojaza fomu za marejesho ya kodi kila baada ya miezi sita, kuna mambo ya msingi anayopaswa kuyazingatia. Ni lazima marejesho hayo yaonyeshe jumla ya mapato yote. Unapaswa kujaza fomu ya marejesho bila kuacha kipengele chochote.

Fomu hizi zinapitiwa kuhakikisha kuwa ulichowasilisha kiko sahihi na kuna adhabu iwapo umewasilisha taarifa za uongo. Ni wazi wafanyabiashara wengi hawawezi kujaza fomu hizi kama wao, hivyo inashauriwa kuwasiliana na ofisi ya karibu ya TRA kwa ajili ya kupata msaada wa jinsi ya kuzijaza.

Baada ya kujaza fomu hii, isaini, weka tarehe na tuma fomu hii TRA. Fomu hizi unapaswa kuzipeleka sambamba na hesabu zilizokaguliwa. Ni vema ukabaki na nakala ya hesabu ulizowasilisha kwa marejeo na kumbukumbu zako.

Kumbukumbu zinazohitajika

Kwa mujibu wa sheria, mlipakodi anapaswa kutunza kumbukumbu zote za mauzo na ununuzi zitakazoiwezesha TRA kukokotoa kiwango sahihi cha kodi anachopaswa kulipa mlipakodi. Nyaraka hizi zinapaswa kutunzwa si chini ya miaka mitano tangu mwaka wa mwisho uliofanya marejesho, labda kama Kamishna wa TRA ametoa maelekezo mengineyo.

Ikiwa kumbukumbu hizo hazikuandikwa katika lugha rasmi ya taifa, Kamishna anaweza kuelekeza mlipakodi kulipia gharama ya kutafsiri taarifa hizo katika lugha ya taifa kwa gharama za mlipakodi mwenyewe.

Fomu ya marejesho ina kurasa saba. Inataka mlipakodi kueleza mapato yake aliyopata katika kipindi husika kutokana na hisa na dhamana katika shirika, mapato nje ya hisa, dhamana na hati fungani, mapato kutoka vyanzo vingine, mapato kutokana na bima, mapato kutokana na bima ya maisha na mapato kutokana na uchimbaji wa madini.

Hupaswi kuchelewesha marejesho TRA kwa kigezo kuwa taarifa ulizonazo hazijakamilika. Ikiwa hauna baadhi ya taarifa, basi fanya makisio na onyesha taarifa zipi wakati wa marejesho zilikuwa ni makisio.

Wiki ijayo nitaangalia taratibu na viwango vya kodi wanazolipa wafanyakazi walioajiriwa katika kampuni, taasisi au shirika, kisha ikiwa nafasi itaruhusu nitajadili kodi ya mashirika.

By Jamhuri